Kagera Sugar kimjinimjini zaidi

Muktasari:

Hoteli waliyoweka kambi, ipo mjini kabisa maeneo ya Magomeni, Mikumi jijini Dar es Salaam na wanapata mahitaji yote na ya kisasa.

VIGOGO wa soka Kanda ya Ziwa, Kagera Sugar wameamua kufanya maandalizi yao ya mwanzo wa msimu jijini Dar es Salaam wakiutumia Uwanja wa Karume kwa ajili ya mazoezi na Hoteli ya Shibamu iliyopo Magomeni kwa malazi.

Klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu msimu uliopita, imefanya usajili wa maana msimu huu chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mecky Maxime na meneja wake, Mohamed Hussein.

Kikosi hicho chenye mseto wa wachezaji wazoefu, wakongwe pamoja na vijana wanaochipukia, kimeamua kuweka kambi mjini kutokana na malengo mbalimbali kabla ya kurejea nyumbani kwao, Misenyi, Kagera.

Kule Kagera wana kambi ya maana eneo hilo la Misenyi na ipo ndani ya eneo la Kiwanda cha Sukari cha Kagera na wachezaji wa kikosi hicho wameibatiza jina na Sobibo kutokana na mazingira yake ambayo si ya changanyikeni. Kambi hiyo imezungukwa na mazao kama miwa, migomba, misitu ya asili pamoja na mifugo.

Kwa kuitazama kambi yao ya Misenyi, ni wazi maisha wanayoishi sasa mjini yana utofauti mkubwa kwa sababu hata wakitaka chipsi (vibanzi) wana uwezo wa kutoka nje na kununua jambo ambalo wakiwa kwao haliwezekani kwani kufika maeneo yenye vitu hivyo ni umbali wa takriban kilomita 10.

MAZINGIRA YA KAMBI MJINI

Hoteli waliyoweka kambi, ipo mjini kabisa maeneo ya Magomeni, Mikumi jijini Dar es Salaam na wanapata mahitaji yote na ya kisasa.

Meneja wao Mohammed Hussein anasema: “Kambi haina wasiwasi kwa sababu wachezaji wanapata kila kitu kinachohitajika kama chakula bora ambacho ni muhimu kwa wachezaji na mazingira mazuri ya mchezaji kuweza kupumzika.”

“Muda mwingi wanapotoka mazoezini huwa wanajipumzisha, ukiona wametoka ni kwenda kula au wanapohitaji kuwa pamoja kuangalia mechi kama za Ndondo na mechi za Ulaya,” anasema Hussein.

Maxime anasema: “Mazingira ya kambi tunayoishi hapa Dar es Salaam si mabaya na hakuna matatizo katika maandalizi yetu, watusikilizie kwenye ligi tu.”

USAJILI MAKINI

Kagera imepanga kuwa na wachezaji 26 msimu mpya wa ligi na malengo yao ni kuongeza wengine pindi watakapoona kuna upungufu hasa wakati wa dirisha dogo la usajili.

Imesajili wachezaji wapya 10 ambao ni makipa, Said Kipao na Ramadhani Chalambanda wameungana na Juma Kaseja kuziba nafasi za Hussein Sharrif ‘Casillas’ na marehemu, David Burhan.

Mabeki wapya ni Adeyum Saleh na Juma Nyosso ambao wameziba nafasi ya Erick Kyaruzi, viungo Omary Daga na Mnigeria  Uzuka Ogachukwu wakati washambuliaji ni Venance Ludovick, Jaffar Kibaya, Abdallah Mguhi na Peter Mwalyanzi.

Ambao hawatakuwepo ni 10 waliokutwa na makosa mbalimbali na waliomaliza mikataba yao kama, Danny Mrwanda, Casilas na Kyaruzi.

Mohamed anasema: “Usajili wote ni kutokana na maagizo ya benchi la ufundi lililo chini ya Kocha Maxime, wamependekeza na tumewasajili.”

Mbali na wachezaji hao wapya, Kagera ambayo inaongozwa na nahodha, George Kavila ambaye ni mkongwe akiwa amecheza Ligi Kuu kwa takriban misimu 20, anasema: “Maandalizi ni mazuri na tuna kila sababu ya kufanya vizuri.”

Wachezaji wengine waliopo katika timu yao ni Geofrey Taita ‘Taita Mwana’, Edward Salvatory, Seleman Mangoma, Mohamed Fhaki, Themi Felix, Paul Ngwai Ngayoma,  Hassan Khatib Nakachale na  Eradius Mfulebe.

Wengine ni pamoja na Ally Ramadhan, Kaseja, Mwaita Gereza, Juma Shemvuni, Ame Ali, Edward Christopher na Japhet Makalai.

WAMEPANIA HASA

Katika msimu uliomalizika Kagera imemaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo jambo lililiwashangaza wengi kwani ilimaliza juu ya matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam. Maxime anasema msimu mpya watakuwa moto zaidi.

“Kila kocha anataka mafanikio na apande kila baada ya hatua moja na ndivyo nilivyojipanga msimu huu na ndiyo maana tukafanya maandalizi ya namna hiyo,” anasema Maxime ambaye ni kocha bora wa ligi kuu msimu uliopita.

“Kwa sasa tuko katika maandalizi, tunategemea kukaa hapa Dar es Salaam kwa wiki mbili ambapo wiki ya kwanza itakuwa ni mazoezi na ya pili tutaitumia kwa kucheza mechi tofauti za kirafiki kwa ajili ya kuwekana sawa na kupata uzoefu na baada ya hapo tutakwenda kwetu kuendelea na maandalizi mengine,” anaeleza Maxime ambaye aliichezea kwa mafanikio klabu ya Mtibwa Sugar kwa zaidi ya miaka 15 na baadaye akapewa ubosi wa kuifundisha kabla ya kuhamia Kagera Sugar ambayo pia ameanza kuipa mafanikio.