Jamani eeh, msiende kutalii Australia

JANA bwana, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliiaga timu ya Madola na kuwaambia mapema hawaendi Australia kutalii, wala kusindikiza wengine ila wakapambane.

Timu ya riadha, ngumi, tenisi ya meza na kuogelea zitaondoka leo Alhamisi kwenda Australia katika Michezo ya Madola itakayoanza Aprili 4-15 kwenye uwanja wa Carrara uliopo Goldcoast.

“Hatutaki visingizio, mnakwenda Australia kushinda na sio kutalii au kusindikiza wengine, kila mmoja kwa nafasi yake najua amejiandaa, hivyo sitarajii visingizio,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema serikali sasa haitapeleka wasindikizaji kwenye mashindano ya kimataifa pia akagusia soka ambapo alisema nako kunamulikwa.

“Kwenye Madola msimu huu tulipewa kota ya watu 34, lakini haikufika sababu ya viwango, sasa tulichokiamua hata tukipewa nafasi 50 bora tupeleke mmoja aliyeiva kwa ushindani, kuliko kupeleka 50 wote,” alisema.

Mapema jana, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Alex Nkeyenge alionya timu inapofanya vibaya wachezaji kusingizia maandalizi.

“Bora kama unaona una kichefuchefu au majeruhi useme mapema ili ubaki, lakini sio kushindwa kisha uanze visingizio,” alisema Nkeyenge.

Nahodha wa timu hiyo, Issa Mtalaso alisema kuwa wamejiandaa na hawatowaangusha Watanzania.

“Tunakwenda kupambana, tumejiandaa na tuko tayari kushinda, hatutowaangusha Watanzania,” alisema Mtalaso.

Tanzania itawakilishwa na wachezaji 16 wa kuogelea, riadha, ngumi na mpira wa meza, makocha watano na viongozi saba kwenye michezo hiyo.