Dharau: Ferguson alivyokataa kumnunua Zinedine Zidane

Tuesday October 10 2017

 

By MANCHESTER, ENGLAND

KUMBE mashabiki wa Manchester United wamekosa mengi. Siri imefichuka. Bosi wa zamani wa Manchester United, Martin Edwards amedai kocha wa zamani wa United, Sir Alex Ferguson alikataa kumnunua staa wa Ufaransa, Zinedine Zidane kwa ajili ya kutaka kumnunua Mfaransa mwingine, Eric Cantona.

Edwards anadai Ferguson alijulishwa mapema kuhusu kipaji cha Zidane katikati ya miaka ya 1999 wakati huo Zidane akiwa bado kwao Ufaransa akikipiga katika klabu ya Boardeaux.

Hata hivyo, baadaye aliamua kumchunia staa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 22.

Baadaye Zidane alikwenda zake Juventus na kucheza kwa miaka mitano kabla ya kuhamia Real Madrid mwaka 2001. Edwards ana kumbukumbu ya tukio hilo mpaka leo.

“Wakati Zidane alipokuwa bado Bordeaux, skauti wetu mkuu, Les Kershaw, alikuwa ananiambia kuwa lazima tumnyatie mchezaji huyu na nikamwambia Alex.

Alex aliniambia kuwa hata Eric (Cantona) mwenyewe alikuwa amemwambia kuhusu Zidane lakini akaona kama vile Zidane alikuwa anacheza katika nafasi moja na Eric.

“Baada ya kufanikiwa kumpa mkataba mpya Cantona kufuatia tukio lake la kumpiga shabiki wa Crystal Palace katika Uwanja wa Selhurst Park mwaka 1995, Ferguson aliamini kama angemleta Zidane, basi ingeathiri nafasi ya Eric kwahiyo akaamua kumpa mkataba mpya,” aliendelea kutoboa Edwards.

Edwards pia amefichua siri jinsi ambavyo Manchester United ilivyokuwa imepeleka jicho lake pia kwa mastaa wanne mahiri wa England wa zamani ambao ni John Barnes, Paul Gascoigne, Gary Lineker na Alan Shearer lakini ikashindwa kumchukua hata mmoja kati yao.

“Paul Gascoigne ni mmoja wao. Tulidhani alikuwa anakuja lakini akaamua kujiunga na Tottenham. Nadhani kulikuwa na fitina za dakika za mwisho. Baadaye nikafanya mazungumzo na Alan Shearer, na kwa mara nyingine tena nilidhani anakuja. Hata hivyo, Jack Walker (Mwenyekiti wa Blackburn wakati huo) alikuwa ana uhakika kuwa Shearer asingekuja United,” alisema Edwards ambaye alikuwa mwenyekiti wa United kuanzia mwaka 1980 mpaka 2002.

“Walker alikuwa kama vile amejiapisha kuwa ‘Labda nife’ kwa Shearer kuja United na matokeo yake akaenda Newcastle. Gary Lineker (alikuwa Leicester City) kama mnavyojua, alikuwa anakwenda kusaini Everton na wakala wake, Jon Holmes alinipigia simu siku hiyo akaniambia ‘Ndio tunaelekea katika treni kwenda kusaini Everton lakini chaguo lake la kwanza ni Manchester United kama mnamtaka.

“Nilimpigia Kocha Ron (Atkinson, aliyekuwa kocha wa United mwaka 1981-86) akaniambia ‘Nina washambuliaji wanne. Katika nafasi ambayo hatuhitaji mshambuliaji ni hiyo.’ Kwahiyo tukaachana naye. Kuhusu John Barnes (aliyekuwa Watford), kocha wao, Graham Taylor alinipigia kuulizia kama Alex Ferguson anamtaka kabla hajasiani Liverpool.

“Alex aliamua kutomchukua kwa sababu ulikuwa msimu wake wa kwanza kama kocha, kikosini alikuwa na Jesper Olsen na alikuwa anataka amuone Jesper kwanza kama angekuwa bora.”