England washindwe wenyewe! Cheki kambi yao Russia

Tuesday June 12 2018

 

ENGLAND wapewe nini tena? Wapewe upele wajikune?

Cheki, kwenye kundi lao, wamepangwa na Ubelgiji, Tusinia na Panama. Kuna nini tena hapo? Watashindwa kweli kuwamo kwenye Top Two ili kutinga hatua ya 16 bora kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia?

Ukiweka kando hilo, kikosi hicho kinachonolewa na Gareth Southgate wamefikia kwenye hoteli matata kabisa na hakika wachezaji wake hawawezi kuwa na msongo wa mawazo kuwafanya wasifanye mambo ya maana katika fainali hizo. Kocha amechagua kuiweka timu yake katika Hoteli ya ForRestMix iliyopo huko Repino.

Hoteli hiyo haina mbwembwe nyingi sana ila ina mambo yote muhimu ambayo wachezaji wa England, akiwamo supastaa wao Harry Kane atahitaji kupumzisha akili yake ili akafanye mambo matamu huko uwanjani.

Ukiingia ndani ya hoteli hiyo utakutana na mandhari murua kabisa ambayo hata uwe na msongo wa mawazo kiasi gani, akili yako itatulia.

Ndani ya hoteli hiyo kuna uwanja mdogo ambao England watautumia kufanya mazoezi ya kupiga penalti kwa sababu ni kitu ambacho kimekuwa kikiwashinda mara nyingi kila wanapokwenda kushindana kwenye michuano mikubwa. Kuna gym, bwawa la kuogelea lenye urefu wa mita 25 pamoja na sauna.

Kuna baa na migahawa ya kutosha tu kama minne hivi, huku ukitaka kwenda St Petersburg ni mwendo kama wa saa moja. Waingereza wenyewe wanaamini kama watatumia vyema mazingira hayo basi wanaweza kufika mbali kwenye michuano hiyo pengine hata robo fainali kama si kwenda kuubeba ubingwa wenyewe kabisa.

Hoteli yenyewe imezungushiwa uzio wenye urefu wa futi 6 na inchi 7, huku kukiwa na ulinzi wa polisi pamoja walinzi wengine muda wote, hivyo kama utataka kuona mazoezi yao wakiwa ndani ya eneo hilo, basi pengine utumie drone.