MTAA WA KATI: Conte anapozijaribu akili za wachezaji wa Chelsea

Said Pendeza

Muktasari:

Costa ndiye aliyekuwa kinara wa mabao katika kikosi hicho cha Chelsea.

CHELSEA ilifunga mabao 85 Ligi Kuu England msimu uliopita, 27 kati ya hayo yalitokana na Diego Costa. Hiyo ina maana mabao 58 tu mengine ndiyo yaliyofungwa na wachezaji wengine klabuni hapo.

Costa ndiye aliyekuwa kinara wa mabao katika kikosi hicho cha Chelsea.

Mabao yake aliyohusika kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge yamechangia pointi 15 kati ya pointi 93 ilizovuna Chelsea kwa msimu mzima hadi wanabeba ubingwa.

Kwa maana hiyo bila ya pointi za Costa, Chelsea isingebeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Wangeishia tu kupata pointi 78 na mabao 58. Pointi hizo na mabao hayo yangewafanya wamalize msimu nafasi ya tatu, nyuma ya Tottenham Hotspur na Manchester City.

Hata hivyo, bado Kocha Antonio Conte anamwona Costa hakuwa na msaada kwenye timu yake na kumwambia hana chake kwa msimu ujao. Kitu kibaya zaidi, ni ile namna aliyotumia kupeleka ujumbe huo kwa Costa.

Amempa ujumbe kwamba hamhitaji kwa kumtumia SMS kwenye simu yake.

Mchezaji ambaye amekufungia mabao 20 na asisti saba. Mchezaji ambaye uwepo wake uwanjani umekuchangia timu yako pointi 15.

Unamwambia humtaki, tena kwa kumtumia meseji tu. Ni dhahau kubwa. Kibinadamu, Conte alipaswa kuketi na Costa na kumweleza malengo yake ya msimu ujao, kistaarabu tu na kumwaambia itakuwa vyema akafikiria kufungua milango ya kuhamia kwingine.

Hata hivyo, Conte hakutaka kujichelewesha, akanyanyua simu yake tu, akaandika meseji na kutuma. Kwisha.

Sawa, pengine Costa ni mchezaji mwenye matukio mengi ya utovu wa nidhamu. Lakini, umemwona amepambana mara ngapi uwanjani kwa ajili ya kocha wake? Msimu mmoja kabla ya Conte, Chelsea ilipokuwa chini ya Jose Mourinho, kocha huyo alitibuana na daktari, Eva Carneiro, kisa tu aliwahi kuingia uwanjani kumtibu Eden Hazard alipojiangusha.

Moto ukamwakia na wachezaji wote hawakuwa tena upande wa Mourinho. Timu ikavuna matokeo mabovu, hadi Mourinho akafutwa kazi. Msimu uliofuatia, wachezaji wale wale wa Mourinho wamebeba ubingwa wa Ligi Kuu wakiwa na Conte.

Sasa Conte anajaribu kurudia makosa aliyowahi kuyafanya Mourinho kwa wachezaji wa Chelsea. Hakuna mchezaji wa Chelsea asiyefahamu upambaji wa Costa kwenye timu hiyo, kisha anaondolewa kwa dharau. Jambo hilo ni wazi kabisa linamshtua Cesc Fabregas. Litamshtua Hazard, Willian, Nemanja Matic na hata Pedro. Watamwona Conte hana shukrani.

Wachezaji wa Chelsea kwa sasa wamekaa tu kimya, hawasemi kitu. Hawatasema kitu hadi hapo Conte atakapoondoka. Kwa sababu ilikuwa hivyo hivyo wakati wa Mourinho. Conte ajitazame namna anavyokabiliana na wachezaji wa Chelsea.

Si watu wa kuwaamini kabisa, wanaweza kukugeuka muda wowote ule. Anyanyue tu simu yake amuuliza Andrea Villas-Boas atamhadithia, kama anadhani Mourinho atamdanganya.