Conte alipowafunika makocha wote Top Six

Muktasari:

  • Kwa kulitambua hilo, makala haya yanayohusu makocha hao wa timu za Top Six na idadi ya pointi walizovuna katika mechi 100 walizowahi kuzisimamia katika ligi.


LONDONENGLAND


KWENYE Ligi Kuu England kunazidi kunoga kwelikweli. Makocha wote wa maana unaowafahamu wanaotamba kwenye soka kwa sasa wapo kwenye ligi hiyo. Kutokana na hilo kumefanya ligi hiyo kuwa na timu sita sasa zinazochuana vikali na hivyo kufanya kuibuka kwa ishu ya Top Six.

Kwa kulitambua hilo, makala haya yanayohusu makocha hao wa timu za Top Six na idadi ya pointi walizovuna katika mechi 100 walizowahi kuzisimamia katika ligi.

6. Jurgen Klopp- mechi 100, pointi 171

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amekuwa gumzo kutokana na kutambua namna ya kumzima Kocha Guardiola katika mechi alizokutana naye.

Lakini kuna wakati Mjerumani huyo alionyesha kocha aliyevuna pointi chache zaidi katika mechi 100 alizocheza kwenye ligi.

Klopp alivuna pointi 171 tu katika mechi 100, akiwa ameshinda mechi 48, sare 27 na kupoteza 25. Hata hivyo, huko Anfield wana matumaini naye.

5. Jose Mourinho- mechi 100, pointi 188

Jose Mourinho hakuwa na rekodi nzuri sana katika mechi zake 100 alizowahi kuiongoza timu yake kwenye mechi za ligi.

Rekodi hizo zilikusanywa katika mechi zake za kuanzia Chelsea hadi Manchester United. Katika mechi hizo, alivuna pointi 188, akiwa ameshinda mechi 53, sare 29 na kupoteza mara 29.

Kwa kiwango na thamani ya Mourinho kuvuna pointi hizo katika mechi hizo 100 hayakuwa mafanikio makubwa kwake.

4. Mauricio Pochetino- mechi 100, pointi 197

Mauricio Pochetino amekuwa akiwashangaza wengi tangu alipotua Tottenham Hotspur. Muargentina huyo ameonyesha kiwango kikubwa si tu kwa England, bali Ulaya pia. Msimu uliopita, timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL nyuma ya waliokuwa mabingwa, Chelsea. Pochettino aliweka rekodi nzuri baada ya kuvuna pointi 197 katika mechi 100 alizocheza kwenye ligi, akishinda 57, sare 26 na kupoteza 17.

3. Arsene Wenger- mechi 100, pointi 197

Arsene Wenger alikuwa kwenye presha kubwa ya kutakiwa astaafu mwishoni mwa msimu uliopita. Mashabiki wa Arsenal walimtaka ang’atuke baada ya kushindwa kuwapa taji la EPL kwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka 13.

Lakini bodi ya Arsenal ilipuuza mpango huo na kumpa mkataba wa miaka miwili. Lakini, rekodi ya Arsenal kwa wakati huo ilikuwa bora kuliko Mourinho na Klopp. Wenger alibeba pointi 197 katika mechi 100, akishinda mechi 59, sare 20 na kupoteza 21.

2. Pep Guardiola- mechi 100, pointi 231

Rekodi ya Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola katika kushinda si mchezo unaambiwa. Mhispaniola huyo amekusanya pointi 231 katika mechi 100 alizocheza kwenye ligi.

Alipoteza mechi 13 na kutoa sare 15 katika mechi hizo 100 na kushinda 72. Mwenyewe ameamua kujipachika jina ‘hakosei’. Ameifanya Man City kuwa moto na leo Jumamosi inaweza kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

1. Antonio Conte- mechi 100, pointi 247

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte ndiye kocha aliyekuwa na rekodi nzuri kabisa kwenye mechi 100 alizocheza kwenye ligi. Muitaliano huyo aliweka rekodi EPL kwa kushinda mechi 30 msimu uliopita. Kabla ya hapo alikuwa na misimu mitatu matata kabisa huko kwenye Serie A kabla ya kwenda kuinoa Timu ya Taifa ya Italia. Kocha huyo wa The Blues alishinda mechi 79, sare 10 na vipigo 11, hivyo kumfanya akusanye pointi 247.