Al Masry, Simba shoo ya kibabe

Muktasari:

  • Kocha huyo Mfaransa amethibitisha ana uwezo mkubwa wa kuwasoma wapinzani wake na kuwaundia mbinu za kuwamaliza.

ILIKUWA ni kama filamu ya Kibongo na mwongozaji ni Pierre Lechantre. Mchezo wote aliuchora mwenyewe. Simba ilifanya kile alichopanga na kikafanikiwa.

Kocha huyo Mfaransa amethibitisha ana uwezo mkubwa wa kuwasoma wapinzani wake na kuwaundia mbinu za kuwamaliza.

Alifanya hilo kwa ustadi na kama sio utulivu mdogo wa Laudit Mavugo na Shiza Kichuya, Al Masry ilikuwa inapoteza mchezo.

Lechantre anasema timu yake itajilinda kwa dakika 60 za mwanzo na ndicho kilichotokea.

Kipindi cha kwanza Simba haikujali sana kuhusu kushambulia, ilitulia nyuma na kuwazuia Al Masry. Walifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa.

Alichoahidi baada ya dakika 60 ndicho alichokifanya Lechantre. Katika muda huo alimpunguza beki Yusuf Mlipili na kumwongeza straika, Laudit Mavugo. Dakika chache baadaye akampunguza James Kotei na kumpa nafasi Shiza Kichuya.

Simba ikafunguka na kuanza kushambulia. Wachezaji wa Al Masry hawakuamini macho yao. Kila wakizuia Simba walikuwa wanakuja kwa kasi zaidi.

Ikabidi waanze kutumia mbinu mbadala ya kujiangusha ili kupoteza muda.

Dakika 11 kabla ya mchezo kumalizika, Mavugo alipata mpira ndani ya eneo la hatari lakini alishindwa kuwa na utulivu mkubwa na kufunga. Shuti lake liliishia kwenye mikono ya kipa wa Al Masry.

Dakika ya mwisho ya mchezo, Kichuya alipata mpira ndani ya eneo la hatari lakini presha ilikuwa kubwa na akashindwa kuupeleka wavuni. Habari ikaishia hapo.

Simba ikaondoshwa kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa faida ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa mabao 2-2.

Kwa kifupi nyota wa Simba walionyesha ukomavu mkubwa. Emmanuel Okwi alikuwa na utulivu wa hali ya juu. Alilazimisha mashambulizi japo mara nyingi alipoangushwa mwamuzi wa mchezo huo, alipeta.

John Bocco pamoja na kuwa na maumivu ya mbali kwenye mguu wake bado alicheza vizuri. Alicheza mipira na alikuwa na kasi.

MLIPILI NA BANCE

Vita moja kubwa iliibuka kwenye mchezo wa juzi Jumamosi. Ilikuwa ni baina ya beki wa Simba, Yusuf Mlipili na straika mkongwe wa Al Masry, Aristice Bance.

Pamoja na Bance kuwa na nguvu nyingi, Mlipili aliyesajiliwa kutoka Toto Africans, alimkaba kwa akili kubwa. Baadaye Bance aliamua kutumia nguvu nyingi zaidi, Juuko Murshid na Erasto Nyoni wakaingilia vita hivyo.

Bance hadi mchezo unamalizika alikuwa amepiga shuti moja tu lililolenga lango. Muda mwingi alipochukua mpira, watatu hao walimtuliza mapema tu.

MANULA MBISHI

Simba ina kila la kujivunia ina kipa wa mashindano ya kimataifa. Ni Aishi Manula na kwenye mechi dhidi ya Al Masry alikuwa nyota wa mchezo.

Dakika tatu tu za mwanzo, Al Masry ilikuwa tayari imefanya mashambulizi matatu lakini yote yaliishia mikononi mwake.

Alifanya uamuzi sahihi. Alipotoka kudaka mpira aliudaka. Alipotaka kupangua mpira alifanikiwa pia. Pamoja na washambuliaji wengi wa Al Masry kuwa na kimo kirefu, hawakuwa na madhara makubwa.

VIGOGO SIMBA NOMA

Viongozi wa Simba wanafahamu fitna usiambiwe na mtu. Kabla ya mchezo walikuwa na utulivu mkubwa, lakini akili zao zilifanya kazi kwa haraka.

Kwanza walishtukia fitna ya chakula hotelini na wachezaji walishtukia. Walichofanya mabosi hao ni kutumia chakula kutoka kwenye migahawa ya nje.

Kabla ya kwenda uwanjani walitumia akili ya kugomea basi walilopewa na maofisa wa Al Masry, kwa hofu ya kuhujumiwa.

Hofu kubwa ya mabosi wa timu hiyo ni basi hilo kuwa na vioo visivyofunguka jambo ambalo lilitoa ishara mbaya kuwa huenda maofisa hao wamechezea hewa ya oksijeni iliyopo ndani ya gari hilo.

Kitendo cha kugomea basi hilo kiliibua mzozo mkubwa na maofisa wa Al Masry ni kama walipaniki na kutaka kulazimisha Simba ipande basi hilo jambo ambalo viongozi wa Wana Msimbazi hao waligoma kabisa.

ULINZI MKALI

Uwanjani Port Said kulikuwa na taswira moja ya kipekee. Maofisa wa Usalama walivalia sare zao za tofauti na kuketi kwenye viti kuzunguka uwanja mzima.

Maofisa hao walivalia trakisuti za bluu na nyeusi pamoja na kofia na muda wote wa mchezo walikuwa wakitazama jukwaani ili ikitokea tu shabiki ameruka kuingia uwanjani wamzuie mapema.

Hii ni tofauti na jijini Dar es Salaam ambapo maofisa huwa sehemu chache tu na sio uwanja mzima.

Upande mwingine mashabiki wa Al Masry walishangilia muda wote wa mchezo kwa staili mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumiwa pia na mashabiki wa timu za Ulaya.

Staili yao kubwa zaidi ilikuwa ya kuwasha tochi za simu na kumulika uwanjani, pia mashabiki walisimama kwa awamu na kufanya uwanja upendeze zaidi.

Kifupi Simba imetolewa, ila Waraabu jasho limewatoka na hawakuamini walichokiona kwenye Uwanja wa Port Said na huenda timu nzima ilienda kulala na viatu kwa jinsi walivyokimbizwa nyumbani kwao na Wekundu wa Msimbazi.