Afrika wana vipaji, utulivu, je wataweza?

Muktasari:

  • Afrika wanao uwakilishi wa timu zilizosheheni vipaji, pia wamekuwa na utulivu kwenye kambi zao tofauti na nyakati zilizopita, lakini je wataweza kufika mbali?

FAINALI za Kombe la Dunia zimeshaanza nchini Urusi na tunashuhudia mambo mazito huko.

Afrika wanao uwakilishi wa timu zilizosheheni vipaji, pia wamekuwa na utulivu kwenye kambi zao tofauti na nyakati zilizopita, lakini je wataweza kufika mbali?

Humo tunao Misri, Morocco, Nigeria, Tunisia na Senegal waliotakiwa kuwa na kila sababu ya kujiamini kuvuka hatua ya makundi japokuwa

baadhi tayari tunaona wameanza vibaya.

Wapo wachezaji wazuri kama Wahbi Khazri wa Tunisia, Mohamed Salah wa Misri, Mehdi Benatia wa Morocco, Simy Nwankwo wa Nigeria na Kalidou

Koulibaly wa Senegal ni baadhi ya majina aliyochomoza sana hata kabla ya mashindano.

Timu kubwa hazikupata kuona kwa yakini timu za Afrika zikipanda chati.

Walau hali ilikuwa hivyo 1982 pale Kocha wa Ujerumani Magharibi, Jupp Derwall alipoamua kutowashirikisha wachezaji wake kutazama video ya Algeria kabla ya mechi baina ya pande mbili hizo.

Alikuwa na wasiwasi wachezaji wake wangemshangaa kwa kuwaonesha video ya aina hiyo, kwa sababu waliona kwamba timu za Afrika ni dhaifu, wakijua wangefunga mabao mengi na eti wangeweza kufanya hivyo huku wakicheza na cigar midomoni mwao.

Hata hivyo, ushindi wa Algeria wa mabao 2-1 dhdi ya mabingwa hao wa Ulaya wakati huo, ulikuwa funzo kwao na kwa wengine. Tunisia walitoshana nguvu na Wajerumani kabla ya kuwachapa Mexico lakini bado kuna watu hawakutia imani kwa timu hizo.

Wawakilishi wengine wa Afrika – Cameroon mwaka huo walifanya vyema japokuwa walishindwa kufika raundi ya pili na hawakupoteza hata mechi moja.

Hata hivyo, baada ya mashindano hayo, kuanzia 1986, wakianza na Morocco, walau mwakilishi mmoja wa Afrika alifika hatua za mtoano.

Miaka minne iliyopita Algeria na Nigeria walifika hatua ya 16 bora, wakionesha kuimarika zaidi kwa bara hilo.

Mwaka huu ilidhaniwa kwamba kiwango kingezidi kwa mataifa yote matano ya Afrika kuwa na uwezo wa kuvuka hatua ya makundi. Je, yaweza kuwa mara ya kwanza katika miaka 36 ambapo kila timu ya Afrika inavuka kikwazo cha kwanza?

Inawezekana kwa sababu kila kikosi cha Afrika nchini Urusi kina raha na hakuna dalili ya kuzuka visa kama vile vya kudai fedha na bonasi

kiasi cha kugoma.

Lakini Morocco wameanza vibaya kwa kufungwa na Iran, tena bao la kujifunga dakika za mwisho kabisa, na kwenye kundi hulo wapo wababe

Ureno na Hispania. Wana kazi kubwa, lakini wanajulikana kuwa na ngome kali.

Senegal wana mengi ya kutoa japokuwa kama ilivyo kwa Misri, Nigeria na Tunisia, kuna wasiwasi juu ya kuaminika kwa makipa wao.

Timu chache Urusi zina ushirika mzuri wa ulinzi wa kati kama wa Kalidou Koulibaly na Kara Mbodji, tukichukulia kwamba Mbodji atakuwa amepona kabisa kutokana na majeraha ya msimu uliopita. Kiungo cha kati nacho kimekuwa uti wa mgongo wa timu, kikiimarishwa na ushawishi wa Badou Ndiaye na Alfred Ndiaye.

Kadhalika, kikosi hicho cha Senegal kina washambuliaji wakali kama Sadio Mané, Keita Baldé, Mbaye Niang na Ismaila Sarr. Wakiwaka kweli basi ni dhahiri Senegal wanaweza kuvuka hadi hatua ya 16 bora.

Misri wao wanatakiwa kuwa makini zaidi hata kama kundi lao linaonekana si la kifo. Uruguay ni wakali na wamewadungua kwenye mechi ya kwanza

ambayo Mohamed Salah hakucheza. Wakimkosa bwana huyo Misri huwa si wazuri sana kama inavyokuwa kwa Liverpool bila Salah na Mane.

Nigeria wana vipaji hasa, wanakwenda na wakati, wakibadilika kuendana na hali, pale mbele wakiwa na mkali Nwankwo na Odion Ighalo.

Lakini wana upungufu kwenye maeneo kadhaa, hasa golini na beki, wakiwa wanachuana na timu kali kama Argentina na Croatia, pia wanao Iceland waliowafunga England miaka michache iliyopita.

Nchi zote tano za Afrika, kwa hiyo, zinaweza kupata sababu za kujiamini na kuvuka hatua ya mwanzo na kujenga ushawishi kwa bara hilo kuongezewa nafasi za timu kwenye mashindano yajayo.