Dili likitiki fresh kinoma

Muktasari:

Mwaka jana, klabu za Ligi Kuu England zilitumia Pauni 1.4 bilioni kwenye dirisha la usajili, zikiweka rekodi ya kutumia pesa nyingi zaidi.

MSIMU wa Ligi Kuu England ulifika tamati rasmi jana Jumapili. Kutokea kwa jambo hilo, ina maana kinakuja kipindi kingine cha usajili wa wachezaji, ambao watakuwa bize kutoka timu moja kwenda nyingine kwa ajili ya michuano ya msimu ujao.

Mwaka jana, klabu za Ligi Kuu England zilitumia Pauni 1.4 bilioni kwenye dirisha la usajili, zikiweka rekodi ya kutumia pesa nyingi zaidi.

Mwaka huu, pesa inayotarajiwa kutumika inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na timu kuwa kwenye mikakati imara ya kuandaa vikosi vyao kwa kufanya usajili wa wachezaji wa maana na wenye uwezo wa kuleta mabadiliko kwenye timu zao. Wakati hilo la usajili likiendelea, kuna baadhi ya wachezaji wanaaminika huenda jana walicheza mechi zao za mwisho za Ligi Kuu England wakiwa na timu wanazochezea kwa sasa na huenda msimu mpya ukianza, hawatakuwa wakitinga tena jezi za vikosi hivyo.

Jack Wilshere (Arsenal)

Mkataba wa Wilshere huko Arsenal utafika tamati mwezi ujao, hiyo ina maana atakuwa huru kwenda kujiunga na timu yoyote kwenye dirisha lijalo la usajili.

Ripoti zinadai kiungo huyo aligomea ofa ya mkataba mpya wa Arsenal ambayo ilimwambia mshahara wake utapunguzwa kutokana na kuwa majeruhi mara kwa mara.

Kocha mpya huko Arsenal huenda asiwe mvumilivu kama alivyokuwa Wenger na huenda mechi ya jana dhidi ya Huddersfield ilikuwa ya mwisho kwa Wilshere kuvaa jezi za Arsenal.

Toby Alderweireld (Tottenham)

Beki wa Kibelgiji, Alderweireld anajiandaa kuihama Tottenham Hotspur wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na timu hiyo. Beki huyo mwenye umri wa miaka 29 mkataba wake umabakiza mwaka mmoja kufika mwisho, hivyo Spurs inaweza kuchukua uamuzi wa kumuuza ili kupata chochote kuliko kubaki naye hadi hapo atakapoondoka bure.

Chelsea na vigogo wengine wa Ligi Kuu England wameonyesha nia ya kutaka saini yake, huku wababe hao wa Stamford Bridge wakitenga Pauni 45 milioni za kumsajili.

Alvaro Morata (Chelsea)

Kabla ya mechi ya jana ugenini kwa Newcastle United, straika wa Chelsea, Alvaro Morata alifunga mabao 15 katika michuano yote. Akiwa ndio kwanza ana msimu mmoja tu kwenye kikosi cha Chelsea, ripoti zinadai staa huyo anaweza kutimkia Juventus, mahali alikowahi kuwapo na kucheza kwa mafanikio. Jumatatu iliyopita kulikuwa na taarifa mchezaji huyo ameshafikia makubaliano binafsi kwa ajili ya kurudi Juventus. Kutokana na hilo linalozungumzwa, huenda mchezo huo wa jana ndiyo mwisho kwenye Ligi Kuu England kwa Morata.

Jack Butland (Stoke City)

Kipa Jack Butland kwa kipindi cha karibuni ameonekana kuivutia Wolves, ambayo itakuwa kwenye Ligi Kuu England msimu ujao. Lakini, Kocha Lambert alitania na kusema hiyo pesa inayovumishwa huko kuwa ofa ya kumsajili kipa huyo, Pauni 35 milioni, itatosha kulipia mkono mmoja tu wa kipa huyo.

Hiyo ina maana Stoke City inataka kuendelea kuwa na huduma ya kipa huyo hadi kwenye michuano ya Championship itakayoshiriki msimu ujao.

Lakini, hakuna ubishi Butland kwa ubora wake wa msimu huu, hawezi kushuka na timu na pengine mechi ya jana itakuwa ya mwisho kwa upande wake kuvaa jezi za wababe hao wa Britannia.

Anthony Martial (Man United)

Kwa mujibu wa taarifa za kutoka Italia zinadai Kocha Jose Mourinho atamruhusu Anthony Martial kuhama Manchester United kwenye dirisha lijalo la usajili.

Juventus inaripotiwa kuhitaji huduma yake na Martial mwenyewe akionekana kuwa tayari kuondoka kwenye timu hiyo ili akapate nafasi ya kucheza huko kwingineko.

Man United jana ilitarajia kumenyana na Watford kwenye mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu England na pengine, Martial anaweza kuwa alicheza mechi yake ya mwisho kama atakuwa amepata bahati ya kupangwa na Kocha Mourinho, ambaye mara nyingi amekuwa akipendelea zaidi huduma ya Alexis Sanchez na Jesse Lingard.

Wilfried Zaha (Crystal Palace)

Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England kwa mwezi uliopita, Zaha amekuwa akihusishwa na Chelsea, Tottenham, Liverpool na Manchester City katika kipindi hiki dirisha la usajili likitarajiwa kufunguliwa muda mfupi ujao. Palace ingependa kubaki na huduma ya mchezaji huyo, lakini kwa kiwango chake ndicho kinachofanya kuwapo na ugumu wa jambo hilo na hivyo kuwa kwenye rada za timu nyingi ndani ya England.

Kama mambo yanayosemwa yatatokea kweli, basi huenda Zaha alicheza mechi yake ya mwisho kwenye ligi hiyo jana huko Palace kutokana na ukweli msimu ujao anaweza kuwa na jezi za wababe wengine EPL.