Uongozi Yanga unayumba, ujipange

Muktasari:

  • Inawezekana haya yakawa mafanikio makubwa kwa Yanga ndani ya msimu huu, kwani katika mashindano mengine mambo hayapo vizuri.

YANGA imerejea ikitokea Ethiopia ilipojihakikishia tiketi ya kuingia hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Safari ya Yanga kufikia huko haikuwa nyepesi. Ilikuwa na milima kuliko mabonde kutokana na changamoto mbalimbali.

Inawezekana haya yakawa mafanikio makubwa kwa Yanga ndani ya msimu huu, kwani katika mashindano mengine mambo hayapo vizuri.

Hata hivyo, kama ulikuwa hufahamu, Yanga ina matatizo mengi ndani ya ungozi wake. Hakuna utulivu wa kiutendaji lakini pia hakuna pesa.

Kila siku mpya inakuwa na changamoto zake, hakuna tofauti na maisha anayoishi mtu wa pale Jangwani katika kipindi cha mafuriko.

Sasa timu imetinga hatua ya makundi eneo ambalo halihitaji ubabaishaji hata punje. Zinahitajika timu zenye viongozi wanaotambua kile wanachokifanya, wanahitajika viongozi ambao wanajua kupanga mambo yao kiuweledi na sio bora liende.

Kama kweli Yanga inataka mafanikio na kujiondoa katika rekodi ya kumaliza mkiani kama mwaka 2016 na 1998 kuna mambo ambayo klabu hiyo kuanzia kwa wanachama wake hadi uongozi wa juu wa Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga wanatakiwa kujipanga, vinginevyo hawatakuwa na nafasi ya kujitetea.

MAWASILIANO MABOVU

Tatizo chini ya uongozi wa Sanga ni mawasiliano mabovu. Hakuna mfumo mzuri wa kiungozi jambo ambalo linaonyesha kiongozi wa juu pamoja na watendaji wengine wako mbali na timu.

Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, George Lwandamina ameondoka huku akilalamikia mfumo mbovu wa mawasiliano ndani ya timu hiyo. Maisha yamekua kama ya baba au mama na mtoto wa shule kila kitu kinahitaji kufuatiliwa na sio kutanguliza weledi. Hili halipaswi kutokea sasa wakati Yanga inaelekea katika mechi za hatua ya makundi.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) linatambua hadi timu inazofika hatua hii ina uongozi uliojipanga na kikosi imara. Ndio maana unaona hatua hii Caf inatoa fedha nyingi.

MAISHA YA KIZAMANI

Yanga inaishi kama ipo kijijini ingawaje hata huko sasa maisha yamebadilika. Safari ya Yanga kufika Ethiopia haikuwa rahisi, ilikuwa na makosa ya kiutendaji kila uwanja wa ndege ilipokatiza ilizuiwa. Pale Kenya mambo yaliharibika na ilitakiwa kurudishwa jijini Dar. Shukrani kwa utemi wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi aliyemtisha yule dada wa pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuwa timu ikirudi, basi ndege yao italipa mabilioni na yule dada akaogopa, kama si hivyo mambo yangekuwa tofauti ingawaje ilikuwa sahihi timu kuzuiwa isivuke hapo. Haikutosha ilipofika Uwanja wa Kimataifa wa Bole pale Addis Ababa, Ethiopia ikakutwa katika msafara wa timu hiyo kuna majina ya watu 21 tu waliotakiwa kuvuka. Waethiopia hawataki ujinga mambo yangekwama kama tunavyowarudisha raia wao katika malori huku Bongo.

Matatizo yanazalishwa na mawasiliano mabovu au kuna watu katika sekretarieti hawajui majukumu yao. Timu ikiwa pale Bole mkuu wa itifaki wa Chama cha Soka cha Ethiopia aliwaambia Yanga hilo ni tatizo lao kwasababu wao waliwasiliana nao bila kujibu ujio wao. Hakuishia hapo, kwa kuwa jamaa hawakutaka matatizo na serikali yao hasa idara ya uhamiaji waliishtaki Yanga kwa Caf juu ya ukimya wao ili likitokea la kutokea wasiwe na lawama. Yanga imshukuru Rais wa Shirikisho la Soka Ethiopia, Juneid Basha aliyepiga simu akitaka wote waruhusiwe.

Yanga ijiangalie kwa kujifanyia tathimini sasa juu ya mambo yao. Iko safi kiasi gani kutokana na hatua iliyopo sasa haitaki masihara au watu wababaishaji. Ukikosea adhabu iko wazi na hakuna simile.

HAKUNA KOCHA

Timu inatinga makundi kocha wake yuko Zambia tena kukiwa na sintofahamu kuhusu kutaka kurudi Zesco. Sanga sio mgeni wa hilo, anajua kinachomuondoa Lwandamina, ni kitu cha muda mrefu. Amechukua hatua gani?

Kuna kundi la kamati ya mashindano halitaki kocha aondoke. Wanataka kuona haki inatendeka juu yake dhidi ya uongozi. Hili ni jipu linalotakiwa kupatiwa ufumbuzi ili mambo yakae sawa. Kuna hatari sakata la Lwandamina likaupasua uongozi wa Yanga

MAKOSA YA NYUMA

Mara ya mwisho Yanga kutinga hatua ya makundi ilikuwa mwaka 2016 lakini kwa taratibu za Caf kabla ya mechi hizi, maafisa wawili wa klabu wataitwa Misri kupewa kanuni na taratibu za kushiriki.

Mwaka huo, Yanga ilishindwa kumtuma mtu na badala yake timu ikafika Algeria na kila kitu kilichokuwa kinatumiwa na timu hiyo kilizuiwa.

Swali la Caf lilikuwaa dogo tu mlikuwa wapi wakati tunatoa semina? Hakuna kiongozi wa Yanga aliyekuwa na jibu na kubaki kulilaumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Safari hii TFF imeshawajulisha juu ya uwepo wa semina hiyo, ngoja tusubiri malimwengu.

Mechi za hatua ya makundi kwa mujibu wa kalenda ya Caf kati ya Mei 4-6 tarehe ambazo Yanga inatarajiwa kuwa na mkutano wake mkuu wa klabu uliopangwa Mei 5. Ratiba kamili timu hiyo itajulikana hapo lakini inawezekana viongozi wa Yanga hawakuwa na uhakika na timu yao kutinga makundi.

Ratiba inatoka leo Jumamosi na kama Yanga itaanzia nyumbani, basi maana halisi ni kuwa mkutano huo utasogezwa mbele au kurudishwa nyuma kwa sababu mbili: Kawaida ya Yanga hupenda kufanya mikutano yake Jumamosi lakini pia hata mechi zake za kimataifa kama itaanzia nyumbani kwa mujibu wa tarehe za Caf, basi hupenda kucheza Jumapili.