INAWEZEKANA: Morocco wana kila nafasi ya kuzima ndoto ya Ivory Coast

Muktasari:

Safari hii, timu kongwe kutoka Afrika kama Ghana na Cameroon, zimekosa nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za Russia mwakani. Timu nyingine ambayo ipo katika hatari ya kukosa nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia ni Ivory Coast.

MSOMAJI, ishara zimeshaanza kuonekana, na tumeshaanza kupata picha ya timu gani ambazo zitawakilisha bara letu la Afrika katika Kombe la Dunia mwakani.

Safari hii, timu kongwe kutoka Afrika kama Ghana na Cameroon, zimekosa nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za Russia mwakani. Timu nyingine ambayo ipo katika hatari ya kukosa nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia ni Ivory Coast.

Ivory Coast bado ina nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Timu hii imeshika nafasi ya pili katika kundi lake ikiwa na pointi moja nyuma ya Morocco. Na mechi yao ya mwisho ni dhidi ya Morocco katika uwanja wa nyumbani wa Ivory Coast.

Lakini, kwa mtazamo wangu Ivory Coast hawana nafasi kubwa sana ya kuvuka mto salama na kufuzu Kombe la Dunia. Katika mechi yao iliyopita dhidi ya Mali timu hiyo ilitoka sare.

Na katika mechi hiyo, Ivory Coast ilikuwa karibu kupoteza huku Mali ikitawala mchezo kwa sehemu kubwa.

Pia, Morocco hivi sasa ipo katika fomu ya hatari. Katika mechi yake dhidi ya Gabon timu hiyo ilionyesha uwezo mkubwa wa kushambulia huku mshambuliaji wake Boutaib akifunga mabao matatu dhidi ya Gabon.

Katika mechi hiyo Morocco pia ilionyesha ina ngome imara huku nyota na straika wa Gabon, Pierre Emerick Aubameyang akishindwa kabisa kupata nafasi za kufunga mabao.

Kocha wa Morocco Herve Renard pia ni kocha wa zamani wa Ivory Coast na anajua kwa undani jinsi timu hiyo inavyocheza na hivyo, ana uwezo wa kuiandaa timu yake vizuri kabla mechi hiyo.

Ivory Coast ni timu ambayo katika miaka 10 ilikuwa na kikosi bora kabisa barani Afrika. Ivory Coast ilikuwa na kizazi cha dhahabu chenye wachezaji kama Yaya Toure, Kolo Toure, Didier Drogba, Eboue, Gervinho, na Kalou. Lakini wachezaji hawa wote sasa wamestaafu na kikosi cha Ivory Coast kwa sasa sio tena tishio tena uwanjani na hata kwenye makaratasi.

Ni kweli wachezaji kama Eric Bailly na Sergie Aurier wana viwango vikubwa huku wote wakicheza katika Ligi Kuu ya England. Lakini, wachezaji hawa bado hawajaonyesha kama wana uwezo wa kuibeba timu hiyo katika mabega yao.

Ni kizazi kipya ambacho kitakutana na Morocco mwezi ujao. Nchi yao inategemea vijana hawa wataipeleka nchi yao katika shangwe za Kombe la Dunia mwakani. Lakini, dalili nyingi zinaonyesha Morocco ina nafasi kubwa ya kuzima ndoto ya Ivory Coast na kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1998 ilifanya hivyo.