SHILAWADU: Kwa umbea wamezidi

Muktasari:

Soud na Kwisa ndio waendeshaji wa kipindi cha Shilawadu, ambacho huruka kila Ijumaa saa 3 usiku katika kituo cha runinga cha Clouds.

INASEMEKANA kwamba Soud Brown na Kwisa ndiyo Watanzania wambea zaidi nchini. Hii ni kwa sababu, jamaa hawapitwi na jambo. Kila lifanywalo na staa yeyote wao wanalo na kulisambaza kwa wapenzi na mashabiki wao. Wanauita ‘Ubuyu’ na usemi wao maarufu ni “Tunawaona tunawaona, mnakula tu ubuyu.”

Soud na Kwisa ndio waendeshaji wa kipindi cha Shilawadu, ambacho huruka kila Ijumaa saa 3 usiku katika kituo cha runinga cha Clouds.

Kutokana na umaarufu wake, kipindi hiki kimekuwa ndio kipindi bora zaidi cha umbea nchini na kirefu cha Shilawadu ni ‘Shirika la Wambea Duniani’.

Kipindi hiki kimekuwa kikitazamwa na maelfu ya Watanzania wakitaka kujua ni ubuyu gani umeandaliwa na Shilawadu siku hiyo na hivyo kukipa umaarufu zaidi.

Wiki iliyopita, kikosi kazi kinachoandaa kipindi hicho kilitinga ofisi za Mwanaspoti zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam na kufanya mazungumzo ya kina na mwandishi wa gazeti hili. Unajua jamaa wana ubuyu gani, kaa chonjo.

SHILAWADU SASA

Kwisa ambaye ndiye mmiliki halali wa kipindi hichi, anasimulia jinsi kipindi hiki cha Shilawadu kilipoanzia. Anasema kwamba walianzia katika kipindi cha Weekend Chat Show na baadaye kuamua kufanya mabadiliko kwa kumchomeka Soud Brown ili kuzidi kuweka chachu.

Soud wakati huo huo pia alikuwa katika kipindi cha XXL akihusika na kipengele cha U heard.

“Nilikuwa nafanya kipindi cha Weekend Chat Show ambacho kilikuwa kikienda vizuri, lakini baadaye nikaona bora nifanye mabadiliko kutokana na kukiona kama hakipo sawa na ndipo nikamchukua Soud na tangu ameingia aliongeza chachu zaidi katika kipindi,” anasema Kwisa ambaye masikio yake hayapitwi na umbea wowote.

Kuhusu jina ‘Shilawadu’ lilipoibuka, Kwisa anasema kuwa lilitokana na utani tu kutoka kwa mfanyakazi mwenzao, Adam Mchomvu, mtangazaji wa kipindi cha XXL, ambaye alikuwa akiwaita Shirika la Wambea Duniani.

“Hatuna uhakika wapi hili jina limetokea zaidi tu ya Mchomvu (Adam) kutuita hivyo, lakini baadaye hata mashabiki wakawa wanatuita hivyo. Kwa hiyo Mkurugenzi wa vipindi Ruge akatushauri tujiite tu jina hili moja kwa moja na ndipo mwaka huu tukazindua rasmi kulitumia na kila mtu ndio anatumia jina hili kwa sasa,” anasema.

WATANZANIA WAMBEA

Kwisa anasema kutokana na Watanzania kupenda umbea, ni sababu ya wao kukifanya kipindi kuwa cha umbea peke yake na sio kitu kingine chochote. Hata hivyo, alisisitiza kwamba umbea wao ni msafi usiokuwa na uongo.

“Umbea ambao tunakuwa tunaufanya ni umbea msafi, yaani hauna mambo mengi. Tukipata Umbea tunabalance (tunatoa nafasi kwa pande zote mbili). Kama povu linatoka basi linakuwa povu safi ambalo mtu anakuwa hanung’uniki.”

‘’Pia ni umbea ambao unaisaidia jamii kwa sababu tunagusa hadi watoto waliotelekezwa na ndiyo maana huwa tunasema vitoto vya Shilawadu. Kwa kufanya hivi watu wanakuwa wanahofia kuwa tukifanya tu jambo lisilokuwa sawa, basi Shilawadu watatumulika,” anasema.

MWENDO WA POVU TU

“Huwa hatuchagui mtu wa kumtolea povu, yeyote ambaye anakuwa amefanya kitu na tukapata taarifa zake lazima tuwajulishe wanajamii waone kuwa kitu kilichofanywa na mtu wao siyo sahihi na siyo kwa mastaa peke yao, hii inaweza kuwa kwa mtu yeyote,” anasema.

Kwisa anafichua kwamba hana urafiki na mastaa bali huwa wanazungumza tu kama washkaji, hilo ni kutokana na kuheshimu kazi yake ambayo ukiendekeza tu mambo ya kujuana inakufa.

“Urafiki tunao lakini sio urafiki wa karibu sana kwa vile ukileta urafiki katika kazi inakupa ugumu wa kuifanya,”

“Pia muda mwingine huwa tunaangalia uzito wa stori kuwa ni ipi ambayo itagusa watu wengi na ipi haigusi. Uzito wa stori ndio unazidi kunogesha kipindi chetu, ila sio kama tunakuwa tunachagua wa kumtolea povu.”

UMBEA MWANZO MWISHO

Kwisa anasema kutokana na tabia yao ya umbea, mwanzoni ilikuwa ni ngumu kueleweka mtaani.

“Mtaani mara ya kwanza tulikuwa tunachukuliwa kama mashangingi wa kiume kwa sababu umbea wanakuwa wanafanya wanawake,” anasema.

“Ubaya ni kwamba tunafanya kipindi mubashara kwenye TV, hivyo ikawa shida kabisa hasa hasa kwa upande wangu yaani nikionekana mtaani inakuwa shida,” anafichua.

“Pia watu wanatuona kama sisi huwa tunachokonoa vitu vya watu, pia walikuwa wanatuona kama hatuna umuhimu ila kadri stori zilivyokuwa zinatoka wakaanza kutuelewa mpaka leo hii wanatuamini.”

WANANUSAJE UMBEA

“Mara ya kwanza tulikuwa tukiingia machimbo wenyewe katika kusaka ubuyu, lakini siku hizi tuna mawakala wetu ambao wanakuwa wanatupigia simu nchi nzima kutupa ubuyu kwa hiyo kuna wepesi ambao tunakuwa tunaupata sasa.

“Pia muda mwingine unakuta mtu labda mumewe anakuwa anachepuka basi anatutafuta, ili tuweze kumuumbua. Nasi huwa tunazipokea hizo taarifa halafu tunaziangalia kama ni za kweli ndipo tunaweka hadharani,” anasema Kwisa.

“Kwa matukio kama haya ya kifamilia wakati mwingine yanakuwa mengi. hivyo tunakuwa tunapata habari nyingi tofauti tofauti zenye uhakika na ndio maana tumekuwa tuna ubora siku zote.”

WAJANJA KINOMA

Kwisa anasema licha ya kwamba wamekuwa wakifukunyua mambo mengi ya watu, lakini hawajawahi kukutana na kichapo chochote kutokana na ujanja, ila wanakutana na changamoto za mitandaoni.

“Hatujawahi kupigwa na yeyote, lakini tulikutana na changamoto katika nyumba ya Mobeto tulivyoenda kunyapia nyapia kwa sababu tulienda bila taarifa halafu ilikuwa usiku, sasa ghafla tukasikia mtu anataka kutoka ikabidi tukimbie kuhofia maana hatukujua kuwa anatoka na nini,” anasema na kufichua kuwa, hawajawahi kutoa kiki wala pesa katika kusaka habari.

“Hatutoi pesa kwa msanii ili kipindi kionekane kizuri, pia sisi hatutoi kiki ili msanii apande chati. Hatujawahi kupokea pesa kwa msanii ili labda nyimbo yake isikike,” anasema.

Hata hivyo, Kwisa anafichua kwamba skendo zinawajenga wasanii. “Msanii akipata skendo nzuri haina kiki, skendo mbaya watu ndiyo wanapenda na wanafuatilia. Hivyo, mtu akiwa na skendo mbaya halafu hapo hapo akatoa video watu wanamfahamu mara moja,” anasema.

MALENGO YAO

“Malengo yetu ni kuwa kampuni kubwa, kama hapa Mwananchi. Tunataka tuwe na watu wengi zaidi ambao watakuwa wanafanya kazi na sisi na kuifanya kuwa shirika kweli kweli kama ambavyo mashirika yanakuwa.

“Tunataka tujitanue zaidi ya hapa. Pia tunataka tuzifanye hizi bidhaa zetu za ubuyu, matamasha na tisheti ziuzike zaidi ili kuweza kufanikiwa zaidi na zaidi. Pia tunaishukuru Clouds Media kwani wamekuwa hawatuchaji chochote katika matangazo yetu,” anasema.

MAFANIKIO

“Hivi sasa tunaishi maisha tofauti na mwanzo, pia hela ndogo ndogo hazitusumbui. Pia tunashukuru kupitia sisi kuna watu wanataka kutangaza bidhaa zao.

“Bado hatujaweza kumiliki majumba ya thamani na magari lakini tuna imani kabisa kuwa tutafanikiwa katika hayo. Pia sio tufanikiwe sisi tu, ni lazima hawa wenzetu nao wafanikiwe kama nikiendesha gari na wao pia waendeshe.

“Umaarufu tulionao umetubadilishia maisha tofauti na ilivyokuwa zamani. Tunataka kupitia kazi hiituache ukumbusho na sio tufe maskini,” anasema.

TIMU YAO

“Ili kipindi kikamilike tunakuwa watu kama 10 ambapo kuna Graphic Designer ambaye anakuwa anatengeneza habari za mitandao ya kijamii. Yupo pia mpigapicha za mnato, mpigapicha katika matukio, kuna mwendesha kipindi, yupo mwongozaji, warusha matangazo na mtu wa radio na tunakuwa tunaruka mubashara kupitia Choice FM,” anasema.

“Pia tuna meneja na tumeamua kuweka mtu wa kupokea simu kwa sababu tunakuwa tuna oda kutoka mikoani hasa wakiwa wanataka bidhaa zetu,” anasema Kwisa na kudai yeye na Soud watafunga ndoa na wenza wao siku moja tena mubashara ndani ya Shilawadu.

MTAYARISHAJI AFUNGUKA

Mtayarishaji wa kipindi hicho, Benedict Noel, anafunguka alianza na washkaji hao tangu enzi za kipindi cha Step Up Player ambacho pia kilikuwa chini ya Kwisa, lakini hakikuwa kipindi pendwa kama Shilawadu.

“Nilianza nao tangu enzi za Step Up Player nikiwa katika kundi lao. Tulipambana na hatukuwahi kukata tamaa. Kipindi hiki kimekuwa pendwa kuliko Step Up,” anasema.

“Sikuwahi kabisa kusomea haya mambo ya Graphics, lakini kilichotokea Kwisa alinifundisha kila kitu. Mpaka leo hii mimi kufikia hapa ni Kwisa ndiye aliyenitengeneza,” anasema.

Akiwazungmzia vijana hao ambao anafanya nao kazi, anasema kuwa ni vijana wakarimu, lakini kwa upande wa Kwisa ni kama ndio ubongo wao kutokana na kuwa na maarifa mengi pamoja na kuwa na ubunifu ambao unaweza ukaisaidia kampuni yao.

“Kwisa kwetu sisi ni kama ubongo, yaani anaweza akakuambia fanya hiki na hiki usifanye. Ukifanya wakati alikukataza utaona kabisa kuwa unakosea, lakini kile ambacho alikuambia ufanye ukifanya unaona kabisa unafanikiwa,” anasema.

“Soud ni mkimya muda mwingi sio wa masihara masihara, lakini muda mwingine akiamua kuchangamka utaboreka kutokana na kuwa na matani mengi ambayo yanaweza kukukera ila huwa hafanyi muda wa kazi,” anasema.