NYUMA YA PAZIA: Jose ana kesi tatu za kujibu Old Trafford

JIONI moja ya Mei 2016, mwaka jana, Televisheni ya Sky Ne ws ilikuwa ikimwonyesha Jose Mou rinho akizurura kando ya Hoteli ya Lowry jijini Manchester bega kwa bega na Bridgedia wake, Rui Faria.

Alikuwa anakaribia kusaini mkataba wake na Manchester United kubeba kazi ya kurithi mikoba ya Sir Alex Ferguson, ambaye viatu vyake vilikuwa saizi 12 na waliochukua nafasi yake baada ya yeye kuondoka, David Moyes na Louis van Gaal walikuwa wanavaa saizi namba 9. Viliwapwaya.

Baada ya vikao vingi vizito katika korido za Carrington mabosi wa United kina Bobby Charlton na wengineo waliamua kumpa kazi Jose Mourinho arudishe tu heshima Old Trafford. Maamuzi yao yalikuwa miezi mitatu baada ya Man City kuamua kumpa kazi Pep Guardiola huku msimu wa Ligi Kuu ya Ujerumani ukiendelea. Walimpa kazi Februari Mosi kabla hata Manuel Pellegrini hajafukuzwa.

Kama ilivyo kawaida, wote walipewa pesa nyingi za kutumia. Walizitumia haswa. Jose alivunja rekodi ya uhamisho wa dunia kwa Paul Pogba. Guardiola alitumia pesa nyingi ingawa kwa mgawanyo ambao, usingeweza kuvunja rekodi.

Mwisho wa msimu, afadhali Jose aliondoka na mataji mawili yasiyo na maana, Pep hakuondoka na chochote. Lengo kubwa la matajiri wao ambao wamewaajiri kwa pesa nyingi na wamewapa pesa nyingi za kununua mastaa ni kuchukua mataji mawili makubwa, lile la Ligi Kuu England na Mabingwa Ulaya.

Miezi 12 ya awali ya mikataba yao ililenga katika kujenga vikosi. Miezi 12 ya mkataba unaofuata imelenga katika kutoa matokeo. Sasa tupo katika miezi 12 ya pili na matajiri wanahitaji matokeo. Sio kwamba wakikosa matokeo wanaweza kufukuzwa, hapana, lakini zitaanza kuonekana dalili za nani mwenye nguvu zaidi baina yao.Kesho Manchester City watakuwa wanatoka katika mtaa wao wa Ashton New Rd, Manchester M11 3FF kwenda katika mtaa wa majirani zao Sir Matt Busby Way, Stretford, Manchester M16 0RA kwa ajili ya pambano la kwanza la Ligi Kuu England msimu huu. Kumbuka nimekwambia ni msimu ambao, matajiri wataanza kudai matokeo na si kudai bado unajenga timu.

City anaongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Manchester United. Katika mechi hii, Jose ana kesi kama tatu hivi za kujibu pengine kuliko Pep. Kesi ya kwanza inaanzia katika pengo lenyewe la pointi baina ya timu zao. Imekuaje kuna pengo la pointi nane?

City imetoka sare moja dhidi ya Everton. Timu nyingi zimeshindwa kuizuia kwa ajili ya kuipa nguvu United. Sasa United inabidi aifanye kazi hii mwenyewe. Jose akishindwa kufanya kazi hii mwenyewe basi hapaswi kupiga kelele za kuomba Bournemouth, Chelsea, Swansea, Arsenal na wengineo wamsaidie.

Hii ni kesi kubwa kuliko unavyofikiria. Kama City akishinda mechi hii atamWacha United kwa pointi 11. Safari ya ubingwa itakuwa nyeupe kwa City kwa sababu sioni City hii ikipoteza uongozi wa ligi kirahisi kwa sababu mbili. Kwanza ni ngumu kwao kupoteza mechi tatu mfululizo katika Ligi hii ya wanyonge wengi. Pili, hata wanaomfukuza hawana uhakika wa kushinda mechi tatu mfululizo.

Kama nilivyosema awali, matajiri wanataka ubingwa wa England kwa ajili ya kurudisha heshima. Kama Jose atamaliza msimu wa pili bila ya kuchukua ubingwa wowote, basi kuna mashabiki wataanza kuguna. Hasa unapofikiria kikosi hiki cha City kinachoanza kutesa sasa kina vijana wengi kama kina Leroy Sane, Gabriel Jesus, Kevin de Bruyne, Raheem Sterling na wengineo kinaonekana kama ndio kimeanza kazi ya kutawala soka la England. Wengi ni watoto hapo.

Jose inabidi arudishe pengo hili mpaka pointi tano. Inabidi ashinde kurudisha katika pengo la pointi ambazo ni rahisi kufikia. Vinginevyo tutaanza kunyanyua majamvi kabla ya kufika Sikukuu ya Krismasi, kitu ambacho hatupendi kitokee.

Lakini, kumbuka kesi nyingine ni kuwa Jose mwenyewe anafukuzwa na Chelsea kwa karibu tu. Kama Chelsea akishinda ugenini kwa West Ham na United wakipigwa na City basi watalingana pointi ingawa Jose atakuwa juu kwa tofauti ya mabao.

Kesi ya mwisho kwa Jose ni ile ya Bruyne. Mpaka leo watu tunajiuliza, ilikuwaje akamuuza kwenda Wolfsburg wakati ule akiwa Chelsea halafu akatupa visingizio hafifu. Leo, yule mchezaji ambaye Jose alidai ni mvivu na hana mchango mkubwa ndiye mtu pekee, ambaye anaweza kuamua ubingwa kati ya City na United.

Jose inabidi amnyamazishe City pamoja na De Bruyne kwa pamoja katika kesi mbili tofauti ambazo zinamkabili ndani ya mahakama ya Old Trafford kesho usiku. Pep ana kesi zake lakini si kwa mechi hii. Tutaziongelea siku zijazo.