Meneja Simba sawa, lakini vipi kuhusu Wambura na Sports?

Muktasari:

  • Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Maofisa Habari, Clifford Ndimbo wa TFF na yule wa Simba, Haji Manara ilielezwa kuwa, ukurasa umefungwa na maisha yanaanza upya.
  • Manara alitamka kwenye mkutano huo kwamba; “Bila kuangalia nani alikuwa na makosa, Simba tumeridhiana na TFF juu ya suala hili.”

SEPTEMBA Mosi mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliitisha mkutano na wanahabari na kuelezea kumalizwa kwa tofauti baina ya wachezaji wa klabu ya Simba na Kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Maofisa Habari, Clifford Ndimbo wa TFF na yule wa Simba, Haji Manara ilielezwa kuwa, ukurasa umefungwa na maisha yanaanza upya.

Manara alitamka kwenye mkutano huo kwamba; “Bila kuangalia nani alikuwa na makosa, Simba tumeridhiana na TFF juu ya suala hili.”

Kauli hii haikuwa na maana zaidi ya kwamba; ‘yaliyopita si ndwele, tugange yajayo’.

Lakini siku chache baada ya maridhiano hayo, TFF ikaibuka na kumshushia rungu Meneja wa Simba, Richard Robert. Kijana huyo asiye na makuu, amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na shughuli zote zihusuzo mpira, pamoja na faini ya Sh 4 Milioni.

Hapa sitaki kujadili uhalali wa adhabu hii, lakini nataka kukumbushia matukio mengine ambayo yalistahili kuadhibiwa lakini ni kama yamepotezewa kimtindo.

MICHAEL WAMBURA

Aprili 6, 2018, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Ebenezer Stafford Mshana alitangaza uamuzi wa kamati yake kutupilia mbali rufaa ya aliyekuwa makamu wa rais wa TFF, Michael Wambura.

Wakati akisoma hukumu hiyo, Wakili Ebenezer, Wambura alibainika kuhusika na makosa ya kupokea/kuchukuwa fedha za TFF za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013.

Kosa jingine lilikuwa kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya Jeck System Limited huku akijua malipo hayo siyo halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013.

Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa 2015.

Kwa makosa hayo, wakili Ebenezer aliitaka TFF imfungulie kesi ya jinai Wambura kwenye mahakama ya kisheria.

Makosa aliyobainika nayo Wambura hayakuwa ya kimpira bali ya jinai ambayo husikilizwa kwenye Mahakama za kisheria.

Lakini, hadi sasa TFF haijafanya hivyo, badala yake inamfungia Meneja wa Simba licha ya maridhiano ya klabu na TFF.

AFRICAN SPORTS

Katika kona ya Mzee wa Upupu ya Februari 20 mwaka huu, ukurasa huu huu tulijadili mkasa wa klabu ya AFC ya Arusha na African Sports ya Tanga za Ligi Daraja la Pili (SDL).

AFC, iliilalamikia TFF kuidhulumu haki yao dhidi ya African Sports ya Tanga.

Malalamiko ya AFC yalikuwa mchezo wao dhidi ya Sports ya Tanga uliomalizika kwa kipigo cha 2-0.

Katika mchezo huo, wenyeji Sports waliwachezesha wachezaji wawili waliotumia leseni ambazo hazikuwa zao, mmoja alitumia leseni ya Athuman Mwile na mwingine alitumia leseni ya Emanuel Mpungumoto.

Wachezaji halisi wenye leseni hizi hawakuwepo siku ya mchezo huo, hivyo Sports walitakiwa kupokonywa pointi zote walizozivuna wakiwa na wachezaji hawa. AFC walikata rufaa lakini rufaa yao TFF lakini ikatupiliwa mbali.

Ukurasa huu wa Mzee wa Upupu ulimtafuta mmoja wa wachezaji halisi wenye leseni zile, Emanuel Mpungumoto, ambaye alisema yeye alishangaa kuona kikosi cha Sports kikiwa na mchezaji mwenye jina lake, wakati hakuwepo uwanjani.

Baada ya kuwashwa na upupu huu, TFF, ikageuka nyuma na kuirudia ile rufaa wa AFC waliyoitupa na kuitolea uamuzi.

Sports ikapokwa pointi tatu na kupewa AFC na kuifanya Vijana wa Arusha wakapata faida ya kupanda daraja. Lakini zaidi ya hapo, hakuna kilichofanyika. Sports walibainika kughushi leseni za wachezaji.

Kughushi ni kosa la jinai ambalo hupaswa kushughulikiwa kwenye mahakama za kisheria, lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yao.

Badala yake anafungiwa meneja wa Simba licha ya maridhiano yaliyotangazwa hadharani kwamba mambo yalishaisha na wachezaji kusamehewa. Tuna kazi kubwa katika soka letu!