Mastaa waliomkimbia Samatta tangu atue Genk

STAA wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anataka kuikimbia klabu yake ya Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji barani Ulaya. Klabu za Levante ya Hispania na Schalke ya Ujerumani zimeonyesha nia ya kumnasa staa huyu mwenye umri wa miaka 25. Endapo atafanikiwa kuondoka Genk, basi Samatta atakuwa ameungana na kundi la mastaa kadhaa aliocheza nao ambao wametimka klabuni hapo tangu Januari 2016.

Wilfried Ndidi (Nigeria, Leicester City)

Kiungo wa kimataifa wa Nigeria ambaye alitua katika klabu ya Genk mwaka 2015 akitokea katika timu ya Nath Boys Adacemy ya kwao Nigeria. Ndidi aliibuka kuwa mmoja kati ya viungo bora katika Ligi Kuu ya Ubelgiji na mwishowe klabu ya Leicester City ya England ikamtumpia jicho na kumuona kama mchezaji mwafaka wa kuziba pengo la kiungo wake, N’Golo Kante aliyehamia Chelsea katika dirisha la majira ya joto mwaka 2016. Ndidi alitua Leicester kwa dau la Pauni 17 milioni Desemba 3, 2016. Ni mmoja kati ya wachezaji waliouzwa kwa pesa ndefu. Ni rafiki mkubwa wa Samatta na wameendelea kuwa na mawasiliano mpaka sasa.

Leon Bailey (Jamaica, Bayer Leverkusen)

Rafiki mwingine mkubwa wa Samatta. Kwa sasa Bailey ni mmoja kati ya mawinga adimu barani Ulaya huku thamani yake ikitajwa kufikia Pauni 50 milioni. Bailey alijiunga na Genk mwaka 2015 akitokea katika klabu ya Trencin ambayo ilikuwa Ligi Kuu ya Slovakia. Mwishoni mwa msimu wa 2015–2016 huku akiwa kama winga anayepika mabao ya Samatta alichaguliwa kuwa mchezaji bora kijana katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Bao lake la michuano ya Europa dhidi ya Rapid Wien Septemba 15, 2016 lilichaguliwa kuwa bao bora la michuano hiyo msimu wa 2016–17. Kama ilivyo kwa Ndidi, Bailey naye aliondoka Januari hiyo hiyo ya 2017 akinunuliwa na klabu ya Bayer Leverkusen kwa dau la Euro 20 milioni huku klabu za Manchester United, Manchester City, Chelsea, Arsenal na Liverpool zikimtolea udenda.

Christian Kabasele (Watford, England)

Beki wa kimataifa wa Ubelgiji ambaye alizaliwa Kinshasa DRC Congo. Kabasele alicheza na Samatta kwa kipindi cha miezi sita tu. Awali alikuwa amenunuliwa na Genk akitokea katika klabu nyingine ya Ubelgiji, Eupen. Baada ya kuonyesha soka safi klabu ya Watford ilimnunua kwa dau la Euro 4 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016. Kabasele aliichezea Ubelgiji mechi yake ya kwanza ya kimataifa Novemba 9, 2016 dhidi ya Uholanzi. Mwaka huu aliitwa katika kikosi cha awali cha Ubelgiji kilichoshiriki katika michuano ya Kombe la Dunia kule Russia lakini hakufanikiwa kuchaguliwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23.

Neeskens Kebano (DR Congo, Fulham)

Kama ilivyo kwa Kabasele, huyu ni staa mwingine aliyecheza na Samatta kwa kipindi cha miezi sita pale Genk kabla ya kutimkia kwingine. Kwa sasa Kebano ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa klabu ya Fulham ambayo imepanda Ligi Kuu pale England na tazamia kumuona msimu ujao akisuguana mabega na mastaa wengine wakubwa. Alitua Genk akitokea katika klabu nyingine ya Ubelgiji, Charleroi aliyoichezea kuanzia mwaka 2013 hadi 2015. Agosti 26, 2016 miezi sita tu baada ya kucheza sambamba na Samatta pale Genk aliuzwa kwa dau la Pauni 3.8 milioni kwenda Fulham ambayo ilikuwa daraja la kwanza. Kebano ni staa wa kimataifa wa DR Congo lakini alizaliwa katika Jiji la Montereaux, Ufaransa Machi 10, 1992.

Timothy Castagne (Ubelgiji, Atalanta)

Mmoja kati ya mastaa ambao walikulia katika Genk tangu wakiwa watoto. Tangu awasili Genk Samatta alikuwa akilindwa na Castagne katika safu ya ulinzi. Hata hivyo, staa huyu aliamua kubadilisha upepo katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana baada ya kuamua kutua klabu ya Atalanta ya Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa dau la Euro 4 milioni. Kabla ya kutua Serie A, Castagine alikuwa anatakiwa na klabu ya Nice ya Ufaransa lakini Atalanta wakapiga bao kwa sababu walikuwa wanamuhitaji kwa udi na uvumba kwa ajili ya kuziba pengo la beki, Andrea Conti aliyetimkia AC Milan.

Jean-Paul Boetius (Uholanzi, Feyenoord)

Mmoja kati ya wachezaji waliokuwa marafiki wakubwa wa Samatta kiasi kwamba wakati fulani staa huyu wa Kidachi alikuwa anafundishwa Kiswahili na Samatta. Ushkaji wao uliimarika baada ya staa huyo kutua Genk kwa mkopo Januari 31, 2017 akitokea katika klabu ya FC Basel ya Uswisi. Alicheza kwa kipindi cha miezi sita na kuwa rafiki mkubwa wa Samatta lakini akamuacha katika mataa baada ya kuamua kurudi katika klabu yake ya utotoni ya Feyenoord pindi dirisha la uhamisho lilipofunguliwa mwishoni mwa msimu huo. Alisaini mkataba wa miaka mitatu ambayo awali ilikuwa imemuuza kwenda Basel mwaka 2015.

Omar Colley (Gambia, Sampdoria)

Beki wa kimataifa wa Gambia ambaye ni mchezaji wa karibuni zaidi rafiki wa Samatta kutimka Genk. Huyu ndiye ambaye katika kipindi cha Mwezi Mtukufu alifunga safari na Samatta mpaka Mji wa Makka kwa ajili ya kutimiza moja ya nguzo muhimu ya Kiislamu. Alinunuliwa na Genk kwa dau la Euro 2 milioni akitokea klabu ya Djurgarden ya Denmark na hivyo kuwa mchezaji wa tatu ghali zaidi katika historia yao kuuzwa klabuni hapo. Alitua Genk katika dirisha la majira ya joto mwaka 2016 lakini katika dirisha hili kubwa ameuzwa kwenda katika klabu ya Sampdoria ya Italia kwa dau la Euro 7.7 milioni ambalo linamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya nchi ya Gambia.