I’M SORRY: Pep awaomba msamaha wachezaji wake baada kipigo cha Real Madrid

KATIKA toleo lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alizungumzia mfumo ambao Bayern ingeutumia kuivaa Real Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wakati huo Madrid ikiwa chini ya kocha wa kiwango cha juu, Carlo Anceloti. Endelea…

Wiki iliyopita yaani Aprili 26, 2014, Real Madrid ilichukua taji la Mfalme mbele ya Barcelona huku Madrid wakicheza kwa kutumia mfumo wa kujihami zaidi wa 4-4-2 uliowasaidia kuwadhibiti wapinzani wao na kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza.

Carlo Anceloti, akiwa mmoja wa walimu wa kiwango cha juu aliamua kuikabili Bayern kwa staili hiyo hiyo, alikuwa tayari kutoona ulazima wa kuutawala mchezo badala yake aliamua kujihami zaidi kwa sehemu kubwa ya eneo lao ambako Pepe na Sergio Ramos walikuwa kivutio.

Madrid walianza kwa nguvu na wachezaji wakafanya kila kitu ambacho kocha aliwataka wafanye, Kroos alitawanya mipira kutoka wingi moja hadi nyingine huku akiendesha mashambulizi ya Bayern kupitia pande zote mbili.

Robben aliwapeleka kwa kasi kuanzia eneo la kati, mabeki nao walimpata Mandzukic kwa krosi walizokuwa wakizipiga huku uchezaji wa Bayern wa kulinda maeneo ukawa na maana katika kuzuia mashambulizi ya kushtukiza ya Madrid.

Hata hivyo, Madrid hawakuhitaji shambulizi la uhakika la kushtukiza ili kupata ushindi, bao pekee katika mechi hiyo lilipatikana kupitia kwa Karim Benzema aliyeujaza mpira wavuni katika dakika ya 19.

Ni pigo kubwa kwa timu iliyojikuta ikikosa ubora wake katika kipindi cha wiki tatu kwa sababu ya wachezaji wake kina Lahm, Kroos na Robben, hata kipa wao tegemeo Neuer alirudi lakini bado hakuwa katika ubora, alikuwa akifanya makosa ya hapa na pale baada ya kuumia siku 11 zilizopita katika mechi dhidi ya Borussia Dortmund.

Pep alijaribu kuwarudisha wachezaji wake katika ubora kwa kipindi cha siku 10 kati ya kipigo dhidi ya Dortmund na kabla ya mechi na Madrid. Jumanne ya Aprili 15, aliwaita wachezaji wake wote.

Alisimama katika ukumbi wa mikutano wa Sabener Strasse taa zikiwa zimezimwa, alianza kuzungumza kwa kuwataka msamaha wachezaji wake kutokana na kuzungumza Kijerumani kibovu, “ingawa najua wote mtaweza kunielewa.

Alianza kwa kuwaelezea anapofika nyumbani kwake kila siku baada ya mazoezi hufungua chupa ya mvinyo na kuanza kunywa na mkewe wakati wa chakula cha jioni. Kauli hiyo iliwafanya wachezaji wacheke hasa kwa kuwa hapo hapo alifungua chupa kubwa ya mvinyo na kuanza kunywa taratibu.

“Wakati wote nikifanya yote haya huwa nawafikiria nyinyi, nafikiria jinsi ya kuwasaidia, nini ninaweza kukifanya ili muweze kucheza vizuri zaidi na zaidi na vipi ninaweza kuwafanya muwe salama, naleta taswira ya yote ninayoweza kuyafanya ili kuwaunga mkono.”

Zaidi ya hilo kawaambia jambo moja ambalo hawezi kuwafanyia, “Siwezi kukimbia uwanjani kwa niaba yenu.” Baada ya kusema hayo kawaonyesha video fupi ambayo iliwaonyesha tofauti ya kasi yao ya mchezo kabla ya kutwaa taji la ligi na baada ya kutwaa taji hilo. Kilichoonekana ni waliacha kukimbiza kwa kasi yao.

“Ni jambo la kawaida na linamtokea kila mtu ambaye anakuwa amefanikisha jambo lakini ni lazima tukumbuke kama hatutakimbizana kwa kasi hatutokuwa lolote.

“Kama tutakuwa tukiwaambia wachezaji wenzetu watuletee mipira miguuni badala ya kutafuta vyumba mbele yetu hapo tutapoteza ubora wetu na kujikuta tukiwa timu dhaifu.”

Baada ya hapo aliwasha taa na kuandika namba zifuatazo. Mechi 27= mabao 13, Mechi 3= mabao 7.

Huu ni uwiano wa mabao ambayo timu ilifungwa katika ligi hadi hapo ilipofika, mabao 13 tu katika mechi 27 kabla ya kubeba taji na baadaye mabao saba katika mechi tatu. Baada ya hapo timu ikakwama.

Itaendelea Jumamosi ijayo…