Hizi ndizo kanuni za kijanja kwa mchezaji

Muktasari:

  • Zifuatazo ni Kanuni 10 za Mpira wa Miguu ambazo mchezaji akikizingatia huwa na kazi nyepesi uwanjani.

KILA mchezo hapa duniani huongozwa na sheria na kanuni, ili kuweza kuwafanya washiriki kuwa makini na kile wanachokifanya, basi miiko huwekwa kama angalizo la kusaidia kufanikisha mchezo husika.

Zifuatazo ni Kanuni 10 za Mpira wa Miguu ambazo mchezaji akikizingatia huwa na kazi nyepesi uwanjani.

1. SHAMBULIA MARA UPATAPO MPIRA

Mchezaji hapa anasisitizwa na kukumbushwa, kuwa pale anapokuwa uwanjani wajibu wake mkubwa ni kutimiza dhumuni na lengo la kucheza mpira wa miguu ni Kufunga, huwezi kufunga kama utakuwa hufanyi mashambulizi kila mara.

Kwa maana hiyo wajibu wako mchezaji ni kuanzisha mashambulizi kila upatapo mpira, akili ya kila mchezaji uwanjani bila kujali nafasi unayocheza ni kuanzisha mashambulizi, ndio maana hata magolikipa huwa wanahusika katika kufanya mashambulizi hasa ya kushtukiza.

2. ZUIA HARAKA UNAPOPOTEZA MPIRA

Kuna njia nyingi za kupoteza mpira kwa mchezaji anapokuwa uwanjani, kupoteza mpira kwa kupiga pasi, mbovu, kunyang`anywa mpira mguuni au kama timu inapoteza mpira kwa nyendo za timu kutibuliwa na wenzao, kukosea kwa namna yoyote kwa mchezaji, hivyo ni wajibu wa kila mchezaji kuzuia mashambulizi mara moja kwa kuziba nafasi na kuharibu nyendo za timu pinzani.
Huo ni wajibu mkubwa wa wachezaji uwanjani pamoja na kuwa wapo watu mahususi kwa ajili hiyo kama vile walinzi, walinda Milango na viungo wazuiaji lakini Mara nyingi tumekuwa tukiona hata washambuliaji wakirudi kuzuia wakati wa kona au adhabu inapopigwa.

3. FUATA PASI AU SHUTI GOLINI

Hii ni moja kati ya majukumu makubwa ya kila mchezaji Uwanjani kuhakikisha mpira anaoupiga kwenda golini au kwa mchezaji mwenzake, unamfikia salama , ni lazima kwa yule anayeuachia mpira mguuni kuufuata ili kama unarudishwa kwake urudi salama au kuufuata kwa macho kama kule alikokusudia kuupeleka unakwenda sawa sawa.
Mara nyingi wachezaji husisitizwa hasa wanapokuwa wadogo, kuhakikisha hata pale anapopiga golini kuufuata, ili kama Mlinda mlango anautema basi inakuwa rahisi kufunga ndio maana washambuliaji wazuri ni wale ambao hufuata mpira kila unapopigwa golini.

4. IFUATE PASI UNAYOPIGIWA

Hii ni tofauti na hiyo namba tatu ambapo hapa Mchezaji anakumbushwa kuhakikisha pale mpira unapopigwa kuja kwake anaupokea, ama kwa kuvutika kuuchukua badala ya kuungoja ufike mguuni mwake, ile ya namba tatu ilikuwa kuusindikiza lakini hii ni kuufuata mpira.
Hii huleta faida kubwa ndani ya uwanja, kwa sababu muwapo uwanjani mnakuwa wachezaji ishirini na mbili, kuendelea kuusubiri mpira ufike mguuni mwako maana yake unataka mpira kutokuwa salama kuelekea kwako, hivyo ili kuuweka salama mchezaji anashauriwa kuufuata mapema.

5. USIUACHE MPIRA UDUNDE MARA KADHAA

Mchezaji anashauriwa kuwa makini na mipira mirefu hata mifupi, inayopigwa kuelekea kwake kwa kufikiri kuwa mpira unapodunda ni lazima utamfikia na matokeo yake mpira hupotea.
Wachezaji wengi hufanya makosa kwa kuuacha mpira kudunda, akitegemea kuuwahi mbele ya wachezaji wengine kitu ambacho husababisha mpira kupotea kirahisi.

6. USIUACHE MPIRA UKUPITE KIRAHISI

Ni makosa makubwa kwa mchezaji kuuacha mpira ukupite kwanza ndipo ufanye maamuzi ya kuupata mpira, si sawa kwa mchezaji kuupisha mpira huku hujui nyuma yako anakuja nani.
Wachezaji wengi hufanya makosa ya namna hiyo, kila mara na ndio maana walinzi madhara na kufungisha kwa kudhani kuwa nyuma yake hakuna mchezaji na washambuliaji, hutumia nafasi hiyo kufunga na ndiyo maana tunasema ni vizuri kuishika amri hii ya sita ili kupunguza makosa.

7. LINDA MPIRA UWAPO MIGUUNI

Mchezaji yoyote huelezwa na kufandishwa mazoezi jinsi ya kuhakikisha hanyang`anywi mpira kirahisi, kwa kufanyishwa mazoezi ya nguvu za miguu , kutumia mikono si kwa kusukuma ila kumzuia mchezaji mwingine asichukue mpira.
Unaweza kuuficha mpira kwa kukimbia nao huku ukipiga chenga, au kuzuia mpira ukiwa umesimama pembeni mwa Uwanja ambako ni salama kutochukuliwa na wachezaji wengine.

8. KIMBIA UKIUANGALIA MPIRA

Mara nyingi hutokea kwa wachezaji wasiojitambua kukimbia, na kuyanza kutembea pale wanapokuwa wanarudi golini kwao baada ya shambulizi lao kupotea, hii humfanya anayepanga mashambulizi kuwa huru kuamua wapi apitie kuja golini kwako.
Mchezaji anashauriwa Mara anapopoteza mpira kuhakikisha anakimbia kinyume nyume huku macho yote yakiangalia mpira.

9. CHEZA KWA FAIDA YA TIMU

Hili ni moja kati ya angalizo ambalo baadhi ya wachezaji hujisahau na kucheza kwa uchoyo huku wakitaka kila mara kufanya kitu kinachofurahisha mashabiki huku wakati anapaswa kukumbuka mara zote timu hutafuta matokeo mazuri na sio vinginevyo.

Ilitokea kule Urusi safari hii wakati mchezaji nyota wa Brazil Neymar kuonekana kucheza kwa faida yake zaidi na siyo timu hasa alipokuwa akikaa na mipira muda mrefu bila kuwapa wenzake.

10. ZINGATIA FAIR PLAY

Soka ni mchezo wa furaha na amani soka si mchezo wa kivita, Chuki na uhasama usiokuwa na maana wakati unapokuwa uwanjani unapaswa kuliweka hilo kichwani mwako.
Amri hii inalazimisha wachezaji kucheza kwa afya ya timu na faida kwa maendeleo ya kila mtu, hasa wale wenye malengo.