Sitashangaa Juve ikizikosa fainali za Ulaya

Muktasari:

  • Walihitaji tu pointi moja katika mechi yao dhidi ya Roma ili washinde Ligi Kuu. Walifanikiwa kutoka sare. Ni wazi kwamba Juventus wametawala soka la Italia kwa miaka mingi. Wameshinda Ligi Kuu ya Italia mara saba mfululizo na wameshinda kombe la Italia mara nne mfululizo. Nchini Italia klabu vikongwe kama Inter Milan, Napoli, Roma na AC Milan wote wameshindwa kuwapa Juventus upinzani mkubwa katika Ligi Kuu na Juventus wameweza kupata mafanikio makubwa hata katika Ligi ya Mabingwa. Chini ya uongozi wa kocha Massimiliano Allegri klabu hiyo imefikia fainali ya Ligi ya mabingwa mara mbili katika misimu minne.

MSOMAJI, wikiendi iliyopita Juventus walishinda Ligi Kuu ya Italia. Walihitaji tu pointi moja katika mechi yao dhidi ya Roma ili washinde Ligi Kuu. Walifanikiwa kutoka sare. Ni wazi kwamba Juventus wametawala soka la Italia kwa miaka mingi. Wameshinda Ligi Kuu ya Italia mara saba mfululizo na wameshinda kombe la Italia mara nne mfululizo. Nchini Italia klabu vikongwe kama Inter Milan, Napoli, Roma na AC Milan wote wameshindwa kuwapa Juventus upinzani mkubwa katika Ligi Kuu na Juventus wameweza kupata mafanikio makubwa hata katika Ligi ya Mabingwa. Chini ya uongozi wa kocha Massimiliano Allegri klabu hiyo imefikia fainali ya Ligi ya mabingwa mara mbili katika misimu minne.

Hakika Juventus wamekuwa na kizazi cha dhahabu ambacho kimeibeba timu hiyo katika njia ya mafanikio. Ni wachezaji kama Buffon, Chiellini, Marchisio, Barzagli, na Lichsteiner.

Pia timu hiyo imesajili wachezaji wazuri katika misimu ya hivi karibuni kama Higuain na Khedira ambao wote wamesaidia kuongeza kiwango cha Juventus.

Hata hivyo, wachezaji hawa wote wameshafikia umri mkubwa na kwa baadhi yao msimu huu ulikuwa nafasi yao ya mwisho kushinda Ligi ya Mabingwa.

Lakini, Juventus walitolewa na Real Madrid katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Kwa mtazamo wangu Juventus watahitaji kuanza mchakato wa kubadilisha kizazi chao baada ya msimu huu kama watataka kuendelea kupata mafanikio na kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa.

Ni kweli kwamba Juventus wana wachezaji chipukizi kama Dybala na Costa lakini ngome ya timu hiyo itahitajika kubadilishwa kuanzia sasa.

Lakini, soko la wachezaji limebadilika sana tangu Juventus walipomsajili Chiellini kwa Pauni8 milioni mwaka 2005.

Hakika Juventus ni klabu yenye fedha nyingi sana lakini kama wanataka kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuziba pengo la wachezaji kama Buffon, na Chiellini basi watahitaji kulipa fedha nyingi sana kwa kuwa wachezaji wenye kiwango hicho wanataka kucheza katika vilabu vikubwa zaidi kama Barcelona na Real Madrid.

Kiwango cha kikosi cha dhahabu cha Juventus kimeshaanza kushuka na nafasi ya klabu hiyo kushinda Ligi ya Mabingwa itaanza kupungua kila msimu.

Juventus bado ni klabu kubwa zaidi nchini Italia lakini sitashangaa kama hatutawaona katika fainali ya Ligi ya Mabingwa tena kwa miaka mingi.

Na ni imani yangu kwamba msimu ujao timu kama Napoli yenye kiwango kikubwa na yenye wachezaji wenye umri mdogo ambao bado wanaendelea kimpira itakuwa na nafasi kubwa kutwaa ubingwa wa Italia.

Juventus watajaribu kusajili wachezaji wapya wenye umri mdogo katika dirisha kubwa la usajili. Lakini, kupata kizazi kipya chenye uwezo wa kuvaa viatu vya akina Buffon itachukua muda mrefu.