Kweli kabisa, wanasoka wapiganie haki zao

Tuesday May 15 2018Boniface Ambani

Boniface Ambani 

By BONIFACE AMBANI,NAIROBI

MABADILIKO. Ndicho kinachoweza kusemwa kwa sasa kuhusiana na kinachotaka kutokea katika michuano ya soka la Ligi Kuu Kenya kwa sasa na huenda likaenda hadi Afrika Mashariki hususani Tanzania.

Wachezaji wa klabu kadhaa za ligi hiyo Jumamosi walianzisha mgomo baridi ili kushinikiza klabu ambazo hazijawalipa mishahara wachezaji wake kwa muda mrefu, kulipa stahiki hizo.

Kuna habari kuwa zipo klabu ambazo zinakwenda mwezi wa 10 sasa bila ya kuwalipa wachezaji wake jambo lililosababusha sasa Chama cha Wanasoka wa Kenya (Kefwa-Kenya Footballers Welfare Association), kuingilia kati suala hilo kwa kuratibu mgomo huo.

Duru zinaarifu kwamba klabu za Chemelil FC, Thika United pamoja na Nakumatt FC ndio zipo taabani zaidi kifedha kiasi cha bodi ya Nakumatt kuamua kuiuza klabu hiyo.

Ni Klabu ambayo ilikuwa na wachezaji wazuri mno, lakini baada ya misukosuko ya kifedha, wachezaji wake mahiri waliondoka. Waliobaki Kwa kweli maisha hayajakuwa mazuri, wanazidi kuumia.

Wakati hayo yakijiri, kocha wa Thika, Nicholas Muyoti, alitupa taulo na kufunga virago vyake baada ya kuona mambo hayaendi sawa klabuni hapo.

Wakati hali hii ikiendelea, wachezaji wengi hawataki kujitokeza kutoa vilio vyao. Wanaogopa wakisikika wakilalamika wataweza kufukuzwa katika klabu zao. Ni balaa mtupu.

Wachezaji hapa nchini na hata Tanzania nilikocheza soka pia wanaumia kwa hali hii. Hata Bongo zipo klabu zinazocheza bila ya kuwalipa vyema wachezaji wake, ingawa kule kwa sasa angalau kuna udhamini wa Vodacom na hata Azam Media.

Si haba lakini klabu kadhaa wachezaji wake wana hali ngumu tofauti na mashabiki wanavyowachukulia.

Kote kote, wachezaji wengi ni wazazi, wanazo familia zinazowategemea kwa mahitaji ya kijamii; chakula, matibabu na hata ada za shule.

Soka wanacheza tena kwa kujituma, lakini hawalipwi huku viongozi wa klabu zao wakizidi kuendesha magari ya kifahari na kujenga majumba pia.

Ukiondoa wachezaji wachache wanaolipwa vizuri na kuishi kwa kufurahia jasho lao hasa Tanzania, kuna kundi kubwa lina umaarufu wa majina tu lakini kwao ni shida nyingi.

Ninajua klabu nyingi za Afrika Mashariki hazina vyanzo vya uhakika wa mapato nje ya fedha za milangoni wakati wa mechi, lakini mambo haya yataendelea hadi lini?

Kabla ya mechi zote kuanza wikiendi iliyopita, wachezaji walikaa uwanjani dakika tano za mwanzoni ikiwa ni salamu kuwa ndani ya wiki chache zijazo kama timu hazitawalipa wachezaji wake, basi ligi haitachezwa.

Angalia Tanzania, majuzi baadhi ya mastaa wa Yanga waliripotiwa kususa kusafiri na timu kwenda Algeria kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger, kisa wanadai malipo yao, yaani wengine hadi fedha za usajili.

Matokeo yake Yanga ikafungwa mabao 4-0. Hivi Simba, Yanga, AFC Leopards na Gor Mahia zitabaki hivi hadi lini?

Ni klabu ambazo zina mtaji mkubwa wa mashabiki ambao wanaweza kutumiwa kuziingizia klabu hizo fedha nyingi tu kama zinavyofanya klabu za Ulaya.

Lakini cha ajabu viongozi wengi wa klabu hizo wamekalia kujali maslahi yao tu. Yaani mambo yakiendelea hivi, itakuwa hekaya za Abunuasi.

Wachezaji watazidi kuumia viongozi wakizidi kujenga majumba.

Kidogo Tanzania kwenye udhamini wa Vodacom katika ligi kuu yao, pia ule wa Azam Media, unazisaidia klabu zao kupunguza machungu.

Lakini hata huko ukiondoa wachezaji wachache wanaolipwa vizuri, wengi wao vipato vyao havilingani na ule umaarufu walio nao.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa wakati mashabiki wanaamini wanasoka wote ni kama wanaishi peponi, kuna wanaokufa na tai shingoni.

Huu ni wakati ambao viongozi wote wa klabu iwe Kenya ama Tanzania, au Afrika Mashariki yote ni lazima waamke na kufanya kazi ya ubunifu kuboresha uchumi wa klabu zao kuweza kuwalipa wachezaji sawa na mahitaji halisi.

Binafsi kinachoniudhi ni kuona viongozi wa klabu hawajali maslahi ya wachezaji wakati wengi wao walikuwa wachezaji siku za nyuma.

Mbona sasa hawawasaidii wenzao ili nao kwa ujumla wao wafaidike na jasho lao? Mabosi wa klabu zetu amkeni, hili la Kenya liwashe moto kote.