Fainali ya FA; Mtibwa, Singida mambo ni moto

Muktasari:

  • Kamati hiyo ilikutana mwishoni mwa wiki na kuweka mikakati ya kukuifanya fainali hiyo iwe tamu kuliko ile iliyochezwa mwaka jana Dodoma na Simba kuifunga Mbao FC mabao 2-1 ndani ya dakika 120.

MTIBWA Sugar na Singida United zitalichangamsha Jiji la Arusha katika fainali ya Kombe la FA Juni 2, sasa katika kuhakikisha inanoga Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Arusha (ARFA) imekutana fasta kujiweka sawa.

Kamati hiyo ilikutana mwishoni mwa wiki na kuweka mikakati ya kukuifanya fainali hiyo iwe tamu kuliko ile iliyochezwa mwaka jana Dodoma na Simba kuifunga Mbao FC mabao 2-1 ndani ya dakika 120.

Mwenyekiti wa ARFA, Peter Temu alisema umuhimu wa ugeni unaotarajiwa kutua Arusha na heshima waliopewa ya kuwa wenyeji wanataka kuona kila kitu kinaenda sawa.

“Kuna wadau wanataka kuwa wadhamini wadogo wa fainali hiyo, hivyo ndio maana tunapitia muongozo wetu kutoka TFF wa kuona nani anafaa kuingia nani hafai,” alisema Temu.

“Tunaamini ugeni huu utawanufaisha wote ndio maana tunakumbushana kutokana na umuhimu wa mchezo utakaotoa mwakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika,’ alisema Temu

Naye Msimamizi wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Abdalah Kajembe alisema uwanja huo upo katika hali bora na wiki mbili kabla ya fainali hizo utafungwa kurekebisha mambo madogo.