Sugua benchi yamkimbiza Giroud Arsenal

Muktasari:

Kauli ya Wenger imekuja wakati Giroud akiwa amechukizwa na kitendo cha kuwekwa benchi muda mrefu.

London, England. Kocha wa timu ya Arsenal, Arsene Wenger amemtaka Olivier Giroud kubaki Emirates hadi mwishoni mwa msimu huu.
Kauli ya Wenger imekuja wakati Giroud akiwa amechukizwa na kitendo cha kuwekwa benchi muda mrefu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, amefungua mlango wa kutoka katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani baada ya kukosa namba kikosi cha kwanza.
Wenger anatambua mchezaji huyo amevurugwa, lakini hataki kumpa ruksa ya kuondoka hadi mwishoni mwa msimu akiamini kuwa atakuwa msaada kwake.
Kocha huyo amekuwa katika mazingira magumu tangu kuanza msimu huu baada ya nyota wake Alexis Sanchez na Mesut Ozil kugoma kutia saini mkataba mpya.
Giroud alikuwa shujaa wa Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopita baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 88 dhidi ya Southampton ‘Watakatifu’.
Mshambuliaji huyo anataka kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kupata fursa ya kuitwa katika kikosi cha Ufaransa kwa fainali za Kombe la Dunia mwakani.