WC2018: Mexico itamkosa beki Diego Reyes

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa za shirikisho la soka nchini Mexico, juhudi za kuhakikisha, beki huyo wa kati wa FC Porto, anarejea uwanjani mapema kabla ya kutimua vumbi kwa kipute cha Kombe la Dunia, zimegonga mwamba.

Moscow, Russia. Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kipyenga cha kwanza kuashiria kuanza kwa mashindano ya Kombe la Dunia 2018 kupulizwa, imethibitishwa kuwa Mexico itamkosa beki wake wa kutumainiwa, Diego Reyes, anayeuguza jeraha la mguu.
Kwa mujibu wa taarifa za shirikisho la soka nchini Mexico, juhudi za kuhakikisha, beki huyo wa kati wa FC Porto, anarejea uwanjani mapema kabla ya kutimua vumbi kwa kipute cha Kombe la Dunia, zimegonga mwamba.
Beki huyo aliwekwa pembeni katika mechi mbili za kirafiki, dhidi ya Scotland na Denmark na ni kwamba, Kocha wa Mexico,  Juan Carlos Osorio, alikuwa na uhakika kuwa beki huyo atarejea lakini ni kama maji yamezidi unga.
Hii ni habari mbaya kwa mashabiki wa soka nchini Mexico kwani huyo ndiye aliyekuwa roho ya safu ya ulinzi ya timu inayokwenda Russia. Reyes atarithiwa na beki wa Pachuca, Erick Gutierrez (22).
Mexico, inatarajiwa kuanza kampeni yao, siku ya Jumapili dhidi ya mabingwa watetezi Ujerumani, ikiwa na pengo la mabeki wawili wenye uzoefu, Reyes na Nestor Araujo (goti).