Rwanda yatakata Chan

Muktasari:

Mashindano ya Chan yanashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee Afrika

Casablanca, Morocco. Rwanda wameungana na Nigeria katika usukani wa Kundi C wa mashindano ya Mataifa ya Afrika CHAN 2018, baada ya kuifunga Equatorial Guinea 1-0 kwenye Uwanja wa Ibn Batouta, Tangier.
Rwanda sasa imefikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili wakishinda dhidi ya Equatorial Guinea na kutoka sare Nigeria.
Katika mchezo huo bao pekee la Rwanda lilifungwa na Thierry Manzi katika dakika ya 67 na kujihakikishia ushindi huo wa bao 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea.
Rwanda sasa inahitaji kushinda au sare katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Libya utakaofanyika Jumanne ijayo.
Vinara wa Kundi C, Nigeria ilichapa Libya 1-0 katika mchezo wao wa pili. Matokeo hayo yanaifanya Libya kubaki nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu wakati Equatorial Guinea ikiwa imeaga mashindano kwa kushikilia mkia wa kundi.