Kocha wa Everton avurungwa mapema

Muktasari:

Kocha huyo alitoa kauli hiyo huku akiwa katika presha kubwa ya kutupiwa virago, baada ya timu hiyo kuboronga kwenye mechi zake zilizopita msimu huu.

London, England. Wakati wachezaji wa Everton wakichunguzwa kwa utovu wa nidhamu, kocha wa timu hiyo Ronald Koeman, amesema bado yuko ngangari.
Kocha huyo alitoa kauli hiyo huku akiwa katika presha kubwa ya kutupiwa virago, baada ya timu hiyo kuboronga kwenye mechi zake zilizopita msimu huu.
Hakuna kocha mwenye presha ya kufukuzwa kama Koeman, lakini ameibuka na kudai yuko fiti na hababaishwi na tetesi za kutimuliwa kwa kuwa ana amini Everton itapata mafanikio muda mfupi ujao.
Mmoja wa wamiliki Farhad Moshiri na Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Bill Kenwright wameingia hofu kuhusu mwenendo wa timu hiyo, baada ya kupata matokeo mabaya tangu kuanza msimu huu.
Ni jambo la kawaida kupata presha kutoka kila pembe kwa sababu timu haifanyi vizuri. Lakini hali hiyo si kwamba unaipenda, unatakiwa kuendelea na kazi. Pia sitaki kuwatwisha mzigo wachezaji kwa matokeo haya,” alisema Koeman.