Ramires kuchomolewa kwa mkopo China

Tuesday October 10 2017

 

Rome, Italia. Klabu ya Inter Milan imeongeza kasi ya kumsajili kiungo wa zamani wa Chelsea, Ramires katika dirisha dogo Januari, mwakani.
Ramires anacheza klabu ya Jiangsu Suning ya Ligi Kuu China na amekuwa kwenye kiwango bora licha ya michuano hiyo kutokuwa na ushindani mkali kama Ligi Kuu England.
Inter Milan kutoka makao makuu San Siro, imekuwa ikimfuatilia kwa karibu kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil kutaka huduma yake kuanzia Januari, mwakani.
Taarifa za awali zimedokeza Inter Milan imetuma maombi ya kutaka kumng'oa Ramires mwenye miaka 30 kwa mkopo kwenda kuongeza nguvu katika kikosi hicho.
Ramires inadaiwa amekubali kujiunga na kigogo hicho na baada ya dirisha la usajili kufunguliwa majira ya baridi atamwaga wino.
Uhamisho wa mchezaji huyo utakuwa rahisi kwa kuwa wamiliki wa klabu hiyo Suning Holdings Group pia wana hisa kubwa Inter Milan.
Ramires aliondoka Chelsea baada ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza kabla ya kutimkia China anakocheza kwa kiwango bora.