Ferdinand aishukia Liverpool

Muktasari:

Wekundu hao walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-0 baada ya dakika 30 nchini Hispania na kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Liverpool imedhihirisha kwamba haiwezi kulinda ushindi baada ya kupoteza uongozi wa mabao 3-0 dhidi ya Sevilla, kwa mujibu wa Rio Ferdinand.
Wekundu hao walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-0 baada ya dakika 30 nchini Hispania na kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, kasi waliyosukumwa na Sevilla walijikuta wakishindwa kuvumilia na kuruhusu wenyeji kusawazisha mabao yote na mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Akizungumza katika kipindi cha BT Sport, Ferdinand alisema: "Kinachoonekana ni kuleta wasiwasi kikosini  na makosa ya mchezaji mmoja-mmoja, kila bao walilofungwa Liverpool lingeweza kuzuilika.
"Mkwaju wa penalti ya Moreno, adhabu aliyotoa Moreno, mpira wa kichwa wa Klavan, angeweza kuupiga na kuuondoa hatarini kwa kuupoteza kabisa uelekeo.
"Huu ni wakati muhimu, siku chache kabla ya wikiendi ni muda wa uongozi kutulia na kuamksha morali ya timu upya kwa ajili ya kuwa na matokeo chanya katika ligi.
"Wanaonekana kuwa na kasi nzuri katika ushambuliaji, lakini timu nzuri inakuwa na muunganiko pande zote, kwa sasa Liverpool haijui jinsi ya kujilinda.
"Ni wazuri kwa kucheza kama walivyofanya kipindi cha kwanza, lakini baadae unatakiwa kubaki nyuma kujilinda, kupunguza presha, lakini walishindwa kufanya hivyo."
Liverpool inaweza kushinda mchezo ujao wa Kundi E watakapocheza na Spartak Moscow wakiwa nyumbani na kufuzu kwa hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza baada ya miaka tisa.