England yapata pigo

Muktasari:

Loftus-Cheek  alipata maumivu baada ya kugongana na mshambuliaji wa Brazil Neymar katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Wembley, England.

London, England. Kiungo anayechipukia Ruben Loftus-Cheek amemshitua kocha wa England, Gareth Southgate, baada ya kupata maumivu ya mgongo.
Loftus-Cheek  alipata maumivu baada ya kugongana na mshambuliaji wa Brazil Neymar katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Wembley, England.
Hakuna taarifa rasmi kuhusu jeraha la kinda huyo ambaye alicheza kwa kiwango bora mchezo uliopita waliotoka sare na Ujerumani ambapo alikuwa mchezaji bora.
Kocha wa Crystal Palace anakocheza kwa mkopo kutoka Chelsea Roy Hodgson, alisema ana matumaini mchezaji huyo hakupata maumivu makubwa.
Crystal Palace inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu England dhidi ya Everton unaotarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki hii.
Kinda huyo mwenye miaka 21, aliumia dakika ya 36 na nafasi yake ilijazwa na kiungo wa Manchester United, Jesse Lingard.
Kocha wa England alisema Loftus-Cheek hakupata maumivu makali ya mgongo yanayoweza kumuweka nje ya uwanja muda mrefu.
Southgate alisema anatarajia kiungo huyo mshambuliaji atarejea uwanjani mapema kwa kuwa hakupata jeraha kubwa.
Mchambuzi wa soka na nguli wa zamani wa Man United,  Ryan Giggs, alisema ana hofu kama mchezaji huyo ana nguvu za kutosha kucheza mechi za klabu na timu ya taifa.