Robben amwaga chozi uwanjani akiwaaga mashabiki

Muktasari:

Nahodha wa Uholanzi, Arjen Robben ametangaza kustaafu soka ya kimataifa kwa aibu, baada ya kushindwa kuipeleka timu hiyo katika Fainali za Kombe la Dunia.

Amsterdam, Uholanzi. Nahodha wa Uholanzi, Arjen Robben ametangaza kustaafu soka ya kimataifa kwa aibu, baada ya kushindwa kuipeleka timu hiyo katika Fainali za Kombe la Dunia.
Kiungo huyo wa pembeni, amecheza timu ya taifa kwa miaka 14 kabla ya juzi usiku kutundika daluga muda mfupi baada ya kumalizika mchezo wa kufuzu fainali hizo dhidi ya Sweden.
Licha ya kufunga mabao yote mawili katika mchezo huo, Robben atakuwa amestaafu kwa aibu licha ya kucheza kwa kiwango bora katika kikosi hicho.
Mchezaji huyo wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, alibubujikwa machozi wakati akiaga mashabiki mjini Amsterdam, Uholanzi.
Robben alimwaga chozi kabla na baada ya mchezo huo wa Kundi A. Ufaransa inaongoza katika kundi hilo ikiwa na pointi 23 ikifuatiwa na Sweden.
Uholanzi ilikuwa na kibarua kigumu cha kukata tiketi kwenda Russia kwa kuwa ilitakiwa kufunga idadi ya mabao saba katika mchezo huo.
Robben mwenye miaka 33, alishindwa kumfariji kocha Dick Advocaat katika mchezo huo baada ya kushindwa kumpa tiketi ya kwenda Russia.
"Huu ni muda mwafaka kwangu kufungulia milango kwa kizazi kipya. Ni siku ngumu sana kwangu usiku wa leo kwa sababu kabla ya mchezo nilijua itakuwa mechi yangu ya mwisho, haikuwa rahisi," alisema Robben.
Mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea, Real Madrid alisema upande mmoja unamshawishi kuendelea kucheza, lakini mwingine unamtaka kustaafu.
Hata hivyo, alisema ana furaha kumaliza soka ya kimataifa akiwa amefunga mabao yote mawili katika mchezo wa mwisho kwenye historia ya soka.
Pia alisema aliingia uwanjani akitambua itakuwa vigumu Uholanzi kukata tiketi kucheza fainali hizo kwa kuwa mabao saba ni mengi.
Mchezaji huyo amestaafu soka kwa mafanikiwa baada ya kucheza mechi 96, amefunga mabao 37 na kutoa pasi za mwisho mara 29.