#WC2018: Majanga! Kylian Mbappe ameumia mazoezini

Wednesday June 13 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Ni Majanga! hofu imetanda katika kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa baada ya winga wake wa kutumainiwa, Kylian Mbappe kuumia katika mazoezi ya Les Blues, baada kugongana na mchezaji mwenzake.
Nyota huyo wa PSG, mwenye umri wa miaka 19, ambaye anatajwa kufanya makubwa nchini Russia, katika mashindano ya Kombe la Dunia, yanayotarajiwa kutimua vumbi kesho.Mbappe aliumia kifundo cha mguu, baada ya kugongana na beki, Adil Rami.
Hii ni habari mbaya kwa kikosi cha kocha Didier Deschamps, hasa ukizingatia wanatarajia kushuka dimbani Juni 16, kucheza mechi yao ya kwanza, dhidi ya Australia, Mjini Kazan. Mbappe alitibiwa na kurudi uwanjani lakini, alionekana kuchechemea habari ambayo sio nzuri kwao.
Mpaka sasa, kikosi cha Les Blues, kimeshawapoteza nyota wawili, ambao ni Laurent Koscielny na Dimitri Payet. Wote ni majeruhi. France wako kundi C, pamoja na Australia, Denmark na Peru.