Wasiotaka Friends of Bandari waumbuliwa

Muktasari:

Sumra amesema wanaamini yale yanayozungumzwa na maofisa wa kundi hilo ni ya kujenga timu na wla si ya kuvuruga. Alitaka wale wanaolikashifu kundi hilo, wakome kwani wana haki ya kutekeleza yale maazimio ya kujenga timu ifanye vizuri kwenye Ligi Kuu ya SportPesa.

MWANACHAMA wa Bodi ya Bandari FC, Salim Sumra amesema wanalitambua vilivyo kundi la ‘Friends of Bandari’ kuwa halali na wamelipa idhini kundi hilo uwezo wa kuongea mambo yanayohusu klabu hiyo.
Sumra amesema wanaamini yale yanayozungumzwa na maofisa wa kundi hilo ni ya kujenga timu na wla si ya kuvuruga. Alitaka wale wanaolikashifu kundi hilo, wakome kwani wana haki ya kutekeleza yale maazimio ya kujenga timu ifanye vizuri kwenye Ligi Kuu ya SportPesa.  
“Tumelipa idhini kundi la ‘Friends of Bandari FC’ kuzungumza mambo ambayo ni ya kuifanya timu yetu iweze kufanya vizuri. Pia hatutaacha watu ambao wanalikashifu kundi hilo kwani wao ndio wavunjifu,” akasema.
Sumra alikuwa akimjibu Mwenyekiti wa tawi la Pwani Kusini la Shirikisho la Soka nchini (FKF), Gabriel Mghendi aliyesema kundi hilo halina uwezo wa kuzungumzia mambo ya klabu. Aliwalaumu maofisa kwa kufanya ‘siri’ mipango ya kuita wachezaji kupigania namba ya kuchezea timu hiyo.
“Sioni sababu yoyote ya Mghendi kuingilia ama kulaumu kundi amblo sisi wenyewe tunalitambua. Kama kweli anataka kuendeleza soka mkoani Pwani, ni kwa nini hatembelei klabu zenye matatizo na kuzisaidia?” akauliza ofisa huyo wa Bandari.
Kuhusu kutowasajili wachezaji kutoka MKoa wa Pwani, Sumra alifahamisha Mwanaspoti kuwa waliwatuma watu kuwafuata wanasoka wawili, mmoja kutoka Malindi na mwingine wa Msambweni lakini hadi sasa hawajajitokeza kufika mazoezi na kufanyiwa majaribio.
“Tumekuwa tukilaumiwa kuwa hatuwasajili wanasoka kutoka mkoa huu wetu wa Pwani. Tunafanya kila juhudi na hata tumewatuma watu wetu wafike Malindi na Msambweni kuwasihi wanasoka hao waje kujiunga na timu, lakini kamwe hawajafika,” akasema.