Waleteni hao Comoro

Wanyama akishangilia bao

Muktasari:

Katika mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, vikosi hivyo vya taifa vitakuwa na kazi ya kuanzisha mbio za kuelekea fainali hizo zitakazochezwa Morocco mwakani na Wanyama amesisitiza mwanzo mzuri dhidi ya Comoros utawapa nguvu za kushiriki shindano hilo.

VICTOR Wanyama ambaye ndiye nahodha wa timu ya soka ya taifa, Harambee Stars na pia kiungo wa Southampton ya Ligi Kuu England, amesema hawana jingine zaidi ya kushinda mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Comoros ya kusaka tiketi ya fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Katika mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, vikosi hivyo vya taifa vitakuwa na kazi ya kuanzisha mbio za kuelekea fainali hizo zitakazochezwa Morocco mwakani na Wanyama amesisitiza mwanzo mzuri dhidi ya Comoros utawapa nguvu za kushiriki shindano hilo.

“Ni muhimu kushinda nyumbani sababu matokeo kama hayo hurahisisha mambo kabla ya mechi ya marudiano. Tunaamni tuna uwezo wa kufuzu kushiriki Afcon na hivyo tunahitaji kuuchukulia kila mchuano kwa uzito mkubwa bila ya kujali wapinzani wetu ni wa hadhi gani,” Wanyama alisema.

Aidha alisisitiza kwamba ili Stars kuwa thabiti, wanachohitaji ni mechi nyingi za kupimana nguvu ikiwa kweli watahitaji kuwa kwenye viwango vya kupambana hadi tamati.

“Hakuna mechi rahisi na ndio sababu ninaomba tuandaliwe mechi nyingi za kurafiki ili kujitia makali na natumaini hilo litazingatiwa na kuanza kutekelezwa mapema,” alisema mara baada ya mazoezi ya juzi Alhamisi jioni.

Ni matamshi yaliyoungwa na mkubwa wake kiungo wa Inter Milan, MacDonald Mariga ambaye pia amesisitiza ushindi na wala si kitu kingine.

“Tupo tayari kwa mechi hiyo mpango mzima ukiwa ni kupiga ua Comoros. Japo sijacheza kwa muda, nafahamu nwenzangu walioko kikosini wamekuwa pamoja kwa muda wa kutosha na hivyo nahisi wako kwenye viwango vizuri,” Mariga alisema.

Kocha wao, Adel Amrouche, amewaonya vijana wake kutowapuuza Comoros kwa kuwaona limbukeni akisisitiza lazima wawape heshima zao na kucheza kwa kujituma.

“Jamani hatupaswi kuwachukulia hivi hivi hawa wapinzani wetu kwani hatuwezi kujua wanachoweza kufanya na kuishia kutushangaza,” alisema.

“Siku chache zilizopita walitoka sare ya bao 1-1 na Burkina Faso kwenye mechi ya kirafiki na hilo linatosha kukuelezea kwamba si kikosi cha kupuuzwa.”

Naye kocha wa Comoros, Djamal Mohamed, amesema wanatarajia gozi kali ila akasisitiza hawaiogopi Stars na wapo Nairobi kwa ajili ya kusaka alama tatu.

“Tunafahamu kwamba Kenya ni kikosi kikubwa kwenye soka, lakini tutahakikisha tunajaribu mbinu zetu zote kuona tutakachofanikisham hatuna woga, tunataka ushindi,” alisema Mohamed.

Hata hivyo Mohamed alielezea wasiwasi wake wa fowadi Dennis Oliech ambaye anamwona kuwa tishio kubwa kwa kikosi chake lakini akashikilia kuwa atatumia mbinu ya ushirikiano kwenye kikosi chake kumzima.

Mechi hiyo imeratibiwa kupigwa kuanzia saa 10:00 jioni.