Sonko anasa mashabiki Dar, Gor na Everton Julai

Muktasari:

Sasa wikiendi iliyopita, akafanya jambo la kushangaza alipowagharamia takribani mashabiki 200 kusafiri Dar kushuhudia pambano kali baina ya AFC Leopards na Gor Mahia kwenye fainali ya SportPesa Super Cup.

Huenda ukafikiri Seneta wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko ni shabiki wa Gor Mahia. La hasha! Ni jamaa tu ambaye anapenda michezo yote kwa ujumla mara nyingi akionekana mitaani kuwapa vijana sapoti maishani haswa kispoti.
Sasa wikiendi iliyopita, akafanya jambo la kushangaza alipowagharamia takribani mashabiki 200 kusafiri Dar kushuhudia pambano kali baina ya AFC Leopards na Gor Mahia kwenye fainali ya SportPesa Super Cup.
Kogalo hatimaye iliibuka na ushindi wa 3-0 shukrani kwa mabao yake Timothy Otieno, Oliver Maloba na John ‘Softie’ Ndirangu, yote yakifungwa kipindi cha pili. Gor sasa itachuana na Everton ya ligi kuu ya nchini England Julai 13 jijini Dar es Salaam kando na kupokea Kshs. 3 milioni.

Alichokifanya Sonko kiliwaacha wengi haswa wafuasi wa siasa na butwaa. Inaeleweka kwamba Sonko yupo kwenye mrengo wa Jubilee wake Rais Uhuru Kenyatta huku wafuasi wengi wa Kogalo wakisapoti mrengo wa NASA unaoongozwa na Mlezi wao Raila Odinga.

Kawanasa kivipi? Wengi wao ni wakaazi wa Kaunti ya Nairobi yake Gavana Evans Kidero lakini mdogo wake Sonko anakiwinda kiti hichi cha ugavana kwenye uchaguzi wa Agosti. Anafahamu fika kwamba mashabiki wengi wa Gor huenda wakampa Kidero kura na kusalia afisini kwa miaka mingine mitano.

Kama harakati za kukatiza sherehe za Kidero, alitoa basi tatu lililosafirisha mashabiki Jumamosi kwa ajili ya pambano la Jumapili. Zaidi ya hapo, aliwapa kila mmoja Kshs 3000 za matumizi.

“Tunamshukuru sana Sonko kwa ukarimu huo. Sisi kama Gor Mahia tumefurahia matendo yake na tunaomba azidi kutusapoti,” alisema shabiki sugu wa Kogalo Jaro Soja baada ya kutwaa ubingwa.

Kwa Jose Marcelo Ferreira, aliwashukuru wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kujikatia tiketi ya kupapurana na Everton mwezi ujao.
“Ukiwa Gor Mahia, unacheza na nia moja tu – kushinda. Ndicho walichokifanya leo wachezaji wangu licha ya mechi mwanzoni kuonekana ngumu.”

Meddie Kagere na Peter Odhiambo walizawidiwa tuzo za mfungaji na kipa bora katika mashindano hayo yaliyoshirikisha timu nane kwa maana ya Tusker FC, Ingwe, Kogalo na Nakuru AllStars za Kenya, Yanga, Simba na Singida United za Tanzania pamoja na Jang’ombe Boys ya Zanzibar.