Harambee Stars yapata pigo

Muktasari:

 Migne aliwajumuisha maproo wake katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya Swaziland na Equatorial Guinea, zitakazopigwa Mei 25 na 28 mwaka huu, Jijini Nairobi.

Nairobi: Kocha Mkuu wa Harambee Stars, Mfaransa Sebastien Migne amepata pigo lingine baada straika mwingine kutangaza kujiondoa katika kikosi cha Stars kitakacho ikabili Swaziland na Equatorial Guinea, Mei 25 na 28,  jijini Nairobi.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, straika wa Cape Town ya Afrika Kusini, Masoud Juma, ametangaza kujitoa katika kikosi hicho kwa kile alichodai ana sababu binafsi.
"Kwa masikitiko makubwa, sitoweza kujumuika na kikosi cha Harambee Stars katika mechi za kirafiki zijazo, nimechukua uamuzi huu kutokana na sababu binafsi," ameandika Masoud Juma.
Juma anakuwa mchezaji wa pili kujitoa baada ya straika wa kutumainiwa, Michael Olunga anayekipiga katika klabu ya Girona ya Hispania, kutokana na kubanwa na ratiba za klabu.
Kujitoa kwa Juma, kunamuacha Kocha Migne kwenye wakati mgumu na hivyo atalazimika kuelekeza mategemeo yake kwa nyota wa Kariobangi Sharks, Ovella Ochieng na Piston Mutamba wa Wazito FC, kuongoza safu yake ya mashambulizi.
Aidha, Mfaransa huyo pia itabidi ajipange upya na ikibidi kuamua kumrejesha kikosini, kinara wa mabao wa KPL msimu huu, Elvis Rupia wa Nzoia Sugar.
Huu ni mtihani wake wa kwanza tangu achukue mikoba ya kuinoa Stars. Migne aliwajumuisha maproo wake katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya Swaziland na Equatorial Guinea, zitakazopigwa Mei 25 na 28 mwaka huu, Jijini Nairobi.