NMG FC yupania kuiona Liverpool

Muktasari:

Timu hiyo ya kampuni inayochapisha magazeti ya Mwanaspoti, Daily Nation na Taifa Leo, inapiga mazoezi kila Jumanne, Alhamisi na Jumamosi uwanjani Railways Club jijini Nairobi na pia kucheza mechi kadhaa za kirafiki.

KIKOSI cha soka cha Nation Media Group (NMG FC) kimeipania tiketi ya kuzuru Jiji la Liverpool huko Uingereza kwenye mechi za Standard Chartered zitakazotimka
katika Uwanja wa Anfield mwezi Mei.
Timu hiyo ya kampuni inayochapisha magazeti ya Mwanaspoti, Daily Nation na Taifa Leo, inapiga mazoezi kila Jumanne, Alhamisi na Jumamosi uwanjani Railways Club jijini Nairobi na pia kucheza mechi kadhaa za kirafiki.
Tayari imethibitisha kushiriki wake wa mashindano ya Road To Anfield yaliyo chini ya Benki ya Standard Chartered ambao ni wafadhili wakuu wa klabu ya Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu England (EPL).
NMG FC itachuana na timu nyingine 35 katika kivumbi kitakachotimka kwenye Uwanja wa Shule ya St. Marys jijini Nairobi ambapo bingwa atajikatia tiketi ya kuwakilisha taifa kule Anfield Mei 17.
Pia bingwa atapata fursa ya kufunzwa na magwiji wa Liverpool ambao ni mabingwa wa mara 18 wa EPL.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Lamin Manjang, amethibitisha mashindano ya mwaka huu yatashuhudia bingwa akienda Anfield moja kwa moja kumenyana na mabingwa wengine toka nchi mbalimbali.
“Tukiwa wafadhili wakuu wa Liverpool tunajivunia fursa kama hii kuwapa wateja wetu nafasi ya kuzuru klabu hii mojawapo kubwa duniani. Tunataka timu za Kenya zitie bidii mwaka huu tuibuke mabingwa wa dunia kama tulivyofanya mwaka 2015,” alisema Manjang.