Winga zinazoteleza VPL

Muktasari:

Majukumu ya mawinga wengi yamebadilika katika soka la kisasa ambapo, sasa timu ikipanda kwenda kushambulia wanaingia katikati na kusaidia katika kufunga. Timu ikipoteza mpira, wanarudi kwa haraka sana kusaidia kukaba.

SOKA la kisasa linaamini katika mashambulizi ya pembeni. Linaamini katika ushirikiano baina ya mabeki wa pembeni na mawinga katika kutengeneza nafasi za mshambulizi na kufunga mabao ya kutosha tu.

Majukumu ya mawinga wengi yamebadilika katika soka la kisasa ambapo, sasa timu ikipanda kwenda kushambulia wanaingia katikati na kusaidia katika kufunga. Timu ikipoteza mpira, wanarudi kwa haraka sana kusaidia kukaba.

Ni mawinga wachache ambao bado wanacheza soka la zamani. Wanaamini katika kucheza pembeni tu na kupiga krosi. Hawaamini katika kuingia katikati na kusaidia kufunga. Hata hivyo, kundi hilo limesalia na wachezaji wachache sana.

Makala hii inakuletea orodha ya washambuliaji wa pembeni ambao, wamekuwa moto wa kuotea mbali Ligi Kuu. Mawinga hawa wanacheza soka la kisasa na lenye mvuto.

 

Saimon Msuva, Yanga

Winga aliyekamilika kila idara Ligi Kuu ni Saimon Msuva. Nyota huyo wa Yanga ametengeneza wigo mpana baina yake na mawinga wengine wa Ligi Kuu. Kwanza Msuva anatengeneza nafasi akitokea pembeni na pia akiwa katikati. Kwa mwezi Oktoba tu alitengeneza mabao sita kwa kutoa pasi za mwisho.

Mbali na hilo Msuva amekuwa imara katika kupachika mabao ambapo, msimu huu amefunga mara sita. Ni mchezaji ambaye ana kasi, nguvu na akili za haraka. Mara nyingine timu inapopanda kushambulia huwa anaingia katikati na kujipanga kufunga. Msuva huwa anawaachia nafasi mabeki wa pembeni ambao, wamekuwa akicheza nao sambamba. Winga huyo anayevaa jezi namba 27 amekuwa hatari pia katika mashambulizi ya kushtukiza.

 

Shiza Kichuya, Simba

Ukiitazama chati ya wapachika mabao unaweza kufikiri ni straika wa kati, lakini kumbe ni winga teleza tu. Kichuya amejipambanua kuwa straika hatari msimu huu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga. Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar tayari amefunga mabao tisa na ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu. Anachokifanya Kichuya ni kujiweka katika nafasi nzuri pindi timu inapokuwa na mpira. Amekuwa akishambulia kwa kupita pembeni na katikati. Silaha kubwa kwa Kichuya ni kwamba, huwa anacheza winga ya kulia wakati anatumia mguu wa kushoto jambo ambalo linamfanya awe na uhuru wa kuingia ndani akiwa na mpira. Ni mara chache kuona amepiga krosi.

 

Hood Mayanja, Lyon

Kwa sasa winga huyu amezinguana na timu yake ya African Lyon na sitashangaa kuona amepata dili la maana kwingine. Mayanja ni hatari japo anacheza pembeni. Ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kuingia katikati kufunga. Ni hatari pia katika mipira ya adhabu. Ni dhahiri kuwa kocha wa Lyon, Bernado Tavares anahuzunika juu ya kukosekana kwake katika kikosi cha timu hiyo.

 

Deus Kaseke, Yanga

Winga, Deus Kaseke wa Yanga ni nyota mwingine ambaye ni gumzo pindi anapotokea pembeni. Kaseke amekuwa akicheza kama winga, lakini mara kadhaa sasa amekuwa akiingia katikati kusaidia mashambulizi. Kipindi cha nyuma Kaseke alikuwa anacheza kama mawinga wa zamani, lakini sasa pindi timu inapopanda na kushambulia kutokea pembeni amekuwa akiingia pia katikati. Uzuri wa Kaseke ni katika kukaba ambapo, kuna uwezekano mkubwa akawa ndiye winga mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kukaba Ligi Kuu.

 

Pastory Athanas, Stand

Nyota huyu wa Stand United ni hatari, ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira na kutengeneza nafasi. Uzuri zaidi ni kwamba amekuwa pia akiingia katikati kusaidia katika upachikaji wa mabao. Kama unamkumbuka vizuri msimu huu ndiye aliyeiua Yanga pale Shinyanga. Pastory amekuwa akijipambanua kila siku ambapo, msimu huu amekuwa na kiwango bora zaidi kuliko msimu uliopita. Pengine nyota huyu anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kufanya makubwa hapo baadaye.

 

Hassan Kabunda, Mwadui

Winga huyu wa Mwadui anaweza kutua Azam katika dirisha hili la uhamisho. Kabunda amejipambanua kuwa mshambuliaji mahiri akitengeneza nafasi kutokea pembeni na kufunga pia. Msimu uliopita alikuwa katika kiwango bora na msimu huu amezidi kuonyesha hakubahatisha. Pia amekuwa akijumuishwa katika kikosi cha Taifa Stars ishara kwamba, tayari ameanza kuaminiwa. Silaha yake kubwa ni kucheza kwa kasi huku akiingia ndani kusaidia kufunga.

 

Joseph Mahundi, Mbeya

Staa huyu wa Mbeya City ni miongoni mwa mawinga wachache wanaofanya vizuri Ligi Kuu. Amekuwa akiimarika siku hadi siku jambo ambalo limekuwa likiipa Mbeya City ahueni. Anajua kutengeneza mashambulizi kutokea pembeni, anapiga krosi na anasaidia katika kufunga. Hata hivyo, amekuwa na changamoto katika kusaidia kukaba lakini bado sio kwa kiwango cha kutisha. Mahundi alipokuwa Coastal Union alikuwa gumzo kubwa zaidi kutokana na namna alivyokuwa akiibeba timu hiyo.

 

Peter Mapunda, Majimaji

Yawezekana ndiye mchezaji pekee wa Majimaji anayefanya vizuri kwa sasa. Anaitwa Peter Mapunda na kabla ya kwenda Majimaji alicheza Mbeya City. Winga huyu amekuwa sehemu kubwa ya mashambulizi ya Majimaji akiwa na wastani mzuri wa mabao kwa mechi. Mapunda ana uwezo mkubwa wa kutembea na mpira, kupiga krosi zenye macho na kufunga.

 

Miraj Athuman, Mwadui

Yawezekana msimu huu hajafunga mabao, lakini bado Miraj anabaki kuwa winga mwenye vitu vingi. Kwanza ana nguvu na uwezo mkubwa wa kuweka mpira chini na kuutoa miguuni mwake huwa ni shughuli nzito sana. Mara kadhaa amekuwa akiingia na kupiga mashuti. Katika kikosi cha Mwadui bado amekuwa na changamoto lakini uwezo wake bado siyo wa kukatisha tamaa. Msimu uliopita alifanya vizuri na Toto Africans ambapo aliibuka pia kuwa mfungaji bora wa timu.

 

Jamal Mnyate, Simba

Unawezaje kuwazungumzia mawinga halafu ukamuacha Jamal Mnyate. Winga huyu amekuwa akicheza soka lenye mvuto na kupiga krosi makini. Amekuwa pia akisaidia kufunga na msimu huu amefunga mabao matatu.

Silaha yake kubwa ni kasi, uwezo wa kutembea na mpira na kupiga krosi. Msimu huu amekuwa akiipa Simba nguvu katika winga ya kushoto na wakati mwingine amekuwa akibadilishana winga ya kulia na Shiza Kichuya.