Tumechemka vipi? Haambiliki huyu

Thursday October 27 2016

 

PAMOJA na kazi nzuri inayoweza kufanywa na kocha wa timu yoyote duniani ikiwamo kuipa timu mataji ya ndani na ya nje nchi na kucheza soka la kuvutia na kufanya kila linaloonekana bora ikiwamo kupata ushindi mzuri kila mara tena wa mabao mengi, bado si kigezo cha kutofukuzwa.

Nani asiyefahamu uwezo mkubwa aliokuwa nao Kocha Mkuu wa kipindi hicho wa Real Madrid, Vicente del Bosque ambaye aliiwezesha timu hiyo kuwa moja kati ya klabu kubwa zilizokuwa zikitandaza soka zuri.

Real Madrid walikuwa na uwezo wa kuuchezea mpira kadri walivyotaka na kuifanya Fifa kuitawaza klabu hiyo kuwa timu bora ya karne!

Licha ya mazuri yote hayo Kocha Vicente aliondolewa baada ya kushindwa kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufungwa na Juventus huku akiwa amemwacha benchi mshambuliaji bora wa kipindi hicho Ronaldo de Lima. Sababu kama hizo na nyinginezo ndizo zinazoweza kuhalalisha kuondoka kwa kocha Hans Van Pluijm. Nina sababu zifuatazo za kutetea hoja yangu na si lazima ukubaliane na mimi, huu ni mtazamo wangu;

 

uwiano wa Uwiano

Amekuja mwanzoni mwa mwaka 2014 amekuwa akilalamikiwa na wadau mbalimbali na uongozi umekuja kuliona hilo, kwa kile kilichoonekana kutosajili kikosi chenye uwiano sawa kwa maana kutoka nafasi za ulinzi, viungo na washambuliaji. Chini yake msisitizo mkubwa umekuwa kusajili washambuliaji wengi wageni na wazawa huku akisahau kabisa kusajili wachezaji wa eneo la kiungo ambako kuna wachezaji watatu tu Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko na Said Juma ‘Makapu’. Hii ilifanya timu ishindwe kumiliki mpira pale inapokutana na vikosi vinavyosheheni wachezaji wazuri wa kati, lakini mastraika na walinzi amewajaza kibao.

 

Viwango vya wachezaji

Klabu inatumia pesa nyingi kusajili wachezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, wapo wachezaji waliokuja Yanga wakiwa na hadhi ya kuichezea timu ya Taifa pia wakiwa wametoka kugombaniwa kwenye soko la usajili. Wachezaji kama Rajab Zahir, Said Bahanuzi, Hassan Dilunga waliondoka ndani ya Yanga baada ya viwango vyao kushuka badala ya kupanda. Sasa bado wapo Malimi Busungu, Makapu na Matheo Simon ambao viwango vyao havilinganishwi kipindi walipokuwa wakiingia Yanga. Hii imetokana na falsafa za Pluijm ya kutopenda kubadili kikosi kwa kila mechi Yanga inayocheza hata na Panone.

 

Mechi za Simba, Azam

Hata pale klabu ya Yanga ilipokuwa ikishinda katika michezo yake dhidi ya Simba na Azam bado kulikuwa na walakini wa uchezaji mzuri wa wachezaji wake ukilinganisha na pale walipokuwa wakicheza dhidi ya timu ndogo kama Ruvu JKT, Majimaji na nyingine.

Msimu uliopita katika mchezo wa pili dhidi ya Simba, licha ya Yanga kushinda kwa mabao 2-0 kila mechi, bado hali haikuwa nzuri uwanjani kwani Simba pamoja na upungufu waliokuwa nao baada ya Abdi Banda kutolewa waliendelea kuwa wazuri zaidi uwanjani. Michezo mingine iliyowaudhi viongozi wa Yanga msimu huu ni ule wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam ulioisha kwa Azam kushinda kwa penati 4-1, Yanga ikitangulia kupata mabao 2-0 hadi mapumziko ilikuja kuzidiwa kipindi cha pili na kuifanya Azam kusawazisha bao moja baada ya jingine na kuufanya mchezo huo uamuliwe kwa penalti.

Angalia mchezo mwingine dhidi ya Simba ambapo Yanga licha ya kutangulia kufunga kipindi cha kwanza na Simba kumpoteza kiungo Jonas Mkude kwa takriban dakika sitini zote za mchezo, bado Simba ilimiliki kwa kiasi kikubwa mchezo huku ikishambulia na kupanga mipango mingi uwanjani iliyoifanya Yanga kuchanganyikiwa na kuipa nafasi ya kusawazisha bao katika dakika za mwishoni mwa mchezo. Hii ni michezo mikubwa iliyokuwa ikimshinda kocha Pluijm na kuwafanya viongozi kufikiria upya.

 

Kimataifa mlionaje

Tunamshukuru alitufikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini bado safari ya kuingia huko haikuwa nzuri sana baada ya Yanga kuwa ikicheza vizuri mchezo mmoja na unaofuata kucheza vibaya, kumbuka dhidi ya APR ya Rwanda mjini Dar es Salaam. Hata mchezo wa pili wa raundi ya pili dhidi ya Esperance ya Angola. Kwenye makundi timu ilikuwa inapaka rangi tu, hakuna matokeo hata pale inapocheza mpira mwingi. Mechi dhidi ya TP Mazembe, Medeama ya Ghana na Mo Bejaia ya Algeria ni uthibitisho wa jinsi Yanga chini ya Hans ilivyoshindwa kubadilika kimbinu na kifalsafa. Bado mnataka aendelee kuwepo?

 

Vyumbani alishindwa

Hali ya umoja na kuelewana kwa wachezaji na Kocha Pluijm haikuwa nzuri sana na hata kufikia yeye mwenyewe kufokeana na baadhi ya wachezaji mazoezini kama ilivyowahi kutokea kwa Amissi Tambwe na Salum Telela. Inasemekana kutokuelewana kwake na Telela ndiko kumemwondoa mchezaji huyo aliyekuwa akinyumbulika kikosini. Alishindwa kuwa na kauli thabiti mbele ya mastaa kama Donald Ngoma ambapo hata pale ilipoonekana mchezaji huyo kucheza vibaya hakuwa akionywa wala kufokewa kama wengine. Ugomvi wa Tambwe na Ngoma unathibitisha hali hiyo. Tayari kulishakuwa na usemi kutoka kwa baadhi ya wachezaji wakimtuhumu kocha huyo kuwa ni mswahili, yaani akisikiliza maneno maneno na kuwaona baadhi ya wachezaji ni bora huku wengine wakionekana si bora. Bila shaka hili liliathiri umoja na ushirikiano baina ya wachezaji wote na hii pengine hatukuwa tukiona wazi nje ya timu lakini moja kati ya matokeo ya haya ni jinsi timu ilivyokuwa ikipoa ghafla huku kukiwa hakuna kiongozi wa kuwambia wenzake ndani ya uwanja.

 

Sura zile zile

Watanzania tumezoea kuishi kwa mazoea ndiyo maana tumejizoea. Pluijm kutokana na woga wake alituaminisha kwamba Yanga imechoka. Tatizo kubwa ilikuwa kutowaamini wachezaji wengine ambao hawakuwa wakipewa nafasi ya kucheza kila mara na hata katika michezo ya kawaida kabisa kama ile ya Friends Rangers na JKT Mlale kwenye Kombe la Shirikisho la Tanzania na hali hii ndio iliyosababisha wachezaji kama Kamusoko, Ngoma, Tambwe, Kelvin Yondani na wengineo kuonekana kuchoka zaidi kwa sababu ya kutumika kila mara. Pia kuwafanya wachezaji wengine wasiotumika mara kwa mara kushuka viwango kwa kasi.

 

Kutowasajili vipenzi

Kweli unamtema mtu kama Salum Telela? Alikuwa kiraka uwanjani, akionekana mpole na mwenye nidhamu ndani ya Yanga na bado ni kipenzi cha wanayanga kwa jinsi alivyokuwa akijitolea kuisaidia Yanga. Aliachwa kwenye usajili huku ikionekana kuwa bado alikuwa na nafasi ndani ya timu akiwa amecheza michezo mingi tena kwenye nafasi mbalimbali kama kiungo mkabaji, mshambuliaji na beki wa kulia huku Hans akimbakiza Said Makapu ambaye huwezi kumlinganisha kiwango na Telela.

 

Timu imepoteza stamina

Kuna tofauti kati ya uchovu wa wachezaji kama wamecheza michezo mingi na timu kupoteza stamina na kasi uwanjani. Hii imeonekana katika michezo mingi ambayo Yanga imekuwa ikicheza huku ikiwa inaongoza, lakini timu zimekuwa zikisawazisha na kuongeza mabao.

Kwa utaalamu wa kocha mkubwa kama Hans tulitegemea kuona mbinu za kocha za kurudisha nguvu na kuondoa uchovu kwa wachezaji haraka zaidi baada ya kutoka kwenye michuano ya Afrika. Bado inaonekana wachezaji kutofanya mazoezi ya kasi kila mara.

 

WALA Haambiliki

Baada ya yote hayo ilifikia kipindi kocha huyo hawezi na wala hataki kabisa kukosolewa, kushauriwa na mwisho yeye ndiye kila kitu hata pale kulipotakiwa kupata ushauri bora usioingilia miiko yake. Kama kocha alishafikia hatua ya kuwahamisha wachezaji kutoka Hoteli moja kwenda nyingine bila ushauriano na uongozi. Hii pekee ilionyesha kuwa, alishafikia hatua ya kutoambiwa wala kushaurika na yeyote, waswahili wanasema ‘Haambiliki’.