SPOTIDOKTA: Hiki ndicho kilichomtoa Benteke uwanjani

Friday January 6 2017CHRISTIAN Benteke

CHRISTIAN Benteke 

By Dk. Shita Samwel

CRYSTAL Palace imepata pigo baada ya straika wake, Christian Benteke kupata majeraha ya bega wakati wa mechi ya Ligi Kuu England (EPL) katikati ya wiki dhidi ya Swansea.

Benteke alipata majeraha hayo baada ya kugongana na kipa wa Swansea, Lucasz Fabianski katika dakika ya 30 katika eneo la penati katika kipindi cha kwanza hivyo kumlazimu kutolewa mapema uwanjani Selhurst Park.

Kocha wa Crystal Palace, Sam Allardyce amethibitisha kuwa straika huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ndiye kinara wa mabao katika klabu hiyo amepata majeraha ya bega la kushoto.

Ingawa alijaribu kuendelea na kumaliza kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili nafasi yake ilichukuliwa na Frazier Campell. Hili ni pigo kwa klabu hiyo ambayo inapambana isishuke daraja.

Allardyce alisema Benteke hatakuwemo katika mechi ya kesho Jumamosi ya Kombe la FA dhidi ya Bolton Wanderers. Atafanyiwa vipimo zaidi ikiwamo cha CT scan ili kuona ukubwa wa jeraha alilopata.

Jeraha alilopata Benteke

Ni kawaida kabisa kusikia wachezaji wa mpira wa miguu wanapata majeraha zaidi ya miguuni kutokana na miguu kuhusika moja kwa moja katika mchezo huo.

Pia, wachezaji hupata majeraha ya maeneo mengine ya mwili kwa kuwa mchezo wa mpira unahusisha mwili mzima na mara nyingi huitajika kutumia maumbo yao kufanya mambo mengi uwanjani ikiwamo kuruka, kupiga vichwa na kupambana ili kuweza kupokonya mpira.

Benteke aligongana na kipa wa Swansea alipokuwa akijaribu kushambulia kwa kuuwahi mpira ambao kila mmoja alikuwa na nafasi ya kuweza kuuwahi.

Tukio hili ndilo lililosababisha kugongana kimwili na kupata majeraha ya nyuzi ngumu za ligament za begani.

Benteke alionekana kushikilia bega lake la mkono wa kushoto, hivyo ni dhahiri alipata majeraha ya bega la mkono wa kushoto. Ingawa kwa kulitazama kwa jicho la kitabibu bega lile, hakukuwa na hali ya kuteguka wala kuvunjika kwani umbile la bega lilikuwa kawaida.

Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa Benteke ameumia nyuzi ngumu zinazoshikilia kiunganisha mifupa wa bega ambacho ndio kinachounda ungio la bega.

Nyuzi ngumu alizoumia ni zile zijulikanazo kama ligaments ambazo mara nyingi nimekuwa nikizieleza huwa zikipata majeraha mara kwa mara katika maeneo ya miguuni kwa wanasoka wengi.

Kugongana na Fabianski ambaye kwa makadirio ana zaidi ya kilo 72 ni dhahiri kuwa eneo la bega la Benteke ndilo lililopata mgandamizo mkubwa kutokana na uzito wa mwili wa kipa huyo.

Habari nzuri ni kwamba mchezaji huyu hakuvunjika wala kuteguka bega, bali amepata majeraha katika nyuzi za ligament ambazo inawezekana kuwa amepata daraja la kwanza au la pili la majeraha ya ligament.

TaaRIfa za eneo la bega

Ungio la bega limeundwa na mifupa mikuu mitatu yaani mfupa unaotoka shingoni kuja begani ambao uko mbele na mfupa mwingine ambao uko nyuma ya bega.

Mfupa mkubwa wa juu ya mkono kichwa chake hujiingiza katika pango la mfupa wa nyuma wa bega, mifupa hii ndio inaunda ungio la begani na kusababisha kutokea kwa mojongeo mbalimbali.

Mifupa hii ndio inayounganishwa pamoja kwa nyuzi ngumu za ligaments ili kutengeneza ungio la bega (shoulder joint). Nyuzi hizi ndizo zinazoshikilia mifupa hiyo na kutengeneza ungio.

Majeraha aliyopata Benteke yanahusisha nyuzi za ligaments ambazo majeraha yake yanaainishwa kwa daraja kwanza, la pili na la tatu.

Ungio la bega hutoa mijongeo mbalimbali ikiwamo kunyoosha mkono pande zote yaani mbele, nyuma, pembeni na hata kuuzungusha mkono kama panga boi.

Ungio la bega ni ungio ambalo huwa na kazi nyingi ukilinganisha na maungio mengine, hivyo kutokana faida hiyo ungio hili hupata majeraha ya kuteguka, kuchanika misuli na kuvutika na kukatika kupita kiwango kwa nyuzi za ligament.

Kuna umuhimu wa CT scan?

Kipimo hiki ni aina ya picha ya mionzi maalumu ya X-ray yenye kamera maalumu ambayo hupigwa ili kumsaidia daktari kutazama kwa undani hali ya tishu laini na tishu ngumu (mifupa) ambayo huwezi kuiona kwa jicho la kawaida.

Kutumia picha za CT scan, daktari anaweza kubaini hitilafu zilizojitokeza ikiwamo uvimbe, kuvilia kwa donge la damu, kuvunjika kwa mfupa na kukatika/kuchanika kwa nyuzi za ligament na tendon na kuchanika kwa misuli.

Kipimo cha CT scan ni muhimu sana kufanyika kwani ndicho ambacho kinawezesha kupata taswira nzuri ya uhakika ili kutoa matibabu kwa uhakika kuendana bainisho la jeraha.

Baada ya kupigwa picha hii itakua ni rahisi kutathimini ukubwa wa jeraha la alilopata Benteke na kuweza kukadiria muda wa kupona.

Matarajio ya jeraha

Kwa sasa Crystal Palace inasubiri kwa hamu kubwa taarifa ya kitabibu baada ya kupiga picha za CT scan. Kabla ya kipimo hiki ni vigumu kusema lini atarudi uwanjani. Lakini tayari kocha wake alisema kuwa hatakuwemo katika mchezo wa FA kesho Jumamosi na nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Loic Remy.

Katika uanishaji majeraha ya nyuzi hizi kuna daraja la kwanza, hapa ligament inakuwa imejeruhiwa kiasi huku ikivutika kuzidi kidogo lakini bado inatoa msaada katika bega kulifanya kuwa imara. Huchukua wiki 1-2 kupona.

Kwa daraja la pili hapa ni ligament inakuwa imejeruhiwa kiasi huku ikivutika kiasi cha kuwa dhaifu au tepetepe, aina hii hujulikana kama kuchanika kiasi kwa ligaments. Huchukua wiki 2-4 kupona.

Wakati kwa daraja la tatu ligaments huwa imekatika kabisa na inaweza kuachana vipande viwili, hivyo ungio la bega linakosa uimara. Jeraha hili huchukua wiki 4-12 kupona.

Vile vile uwezekanao upo wa kujeruhiwa zaidi ya nyuzi moja kwa mpigo, na inapotokea hivyo madhara makubwa huweza kutokea ikiwamo uharibifu wa mishipa ya damu na mishipa ya fahamu inayoenda katika misuli ya mkononi.  Hali hii inaweza kusababisha kukatwa kwa mkono.

Mara nyingi matibabu yake hayahitaji upasuaji isipokuwa kwa jeraha la ligaments daraja la tatu.

Ulaji mwingi wa vyakula vya protini, matunda, mboga za majani, na kushikamana na ushauri na programu za matibabu husaidia jeraha la ligament kupona na kuimarika.

Mazoezi ya kupasha kabla ya kuingia mchezoni na mazoezi ya kunyoosha viungo yanapunguza hatari ya kupata majeraha ya ligaments.

Tusubiri ripoti ya picha ya CT scan ili tujue ukubwa wa jeraha alilolipata Benteke.

Kwa sasa mchezaji huyo amepewa mapumziko zaidi na kuendelea na matibabu mepesi ikiwamo ya kudhibiti maumivu kwa kuvikwa kifaa tiba cha kutuliza bega ingawaje Mwenyekiti wa Crystal Palace, Steve Parish amewataka watu wasijewe na hofu kwa kiasi kikubwa.