Ndanje pumzika mwana

Muktasari:

90-Msiba wa Bonny upo nyumbani kwao kwenye kijiji cha Bulyaga, huko Tukuyu wilaya ya Rungwe. Ni mwendo wa dakika 90 kwa basi kutoka Mbeya mjini ukipanda gari zinazokwenda Kyela na nauli ni Sh3000 tu.

MWANASOKA nyota wa zamani wa Tanzania, Godfrey Bonny ‘Ndanje’, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Ijumaa mkoani Mbeya. Mchezaji aliyewahi kukipiga Tukuyu Stars, Prisons na Yanga aliwahi kuwa tegemeo pia kwenye Taifa Stars na Kilimanjaro Stars. Zifuatazo ni takwimu mbalimbali za maisha yake katika namba.

 

90-Msiba wa Bonny upo nyumbani kwao kwenye kijiji cha Bulyaga, huko Tukuyu wilaya ya Rungwe. Ni mwendo wa dakika 90 kwa basi kutoka Mbeya mjini ukipanda gari zinazokwenda Kyela na nauli ni Sh3000 tu.

 

37-Mchezaji huyo aliyekuwa akichezea nafasi ya kiungo, amefariki akiwa na miaka 37. Maziko yake yatafanyika leo Jumamosi saa 7 mchana ikiwa ni saa chache kabla ya Yanga kurudiana na Ngaya de Mbe ya Comoro kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mjomba wa marehemu, Innocent Sijagonda amesema ndugu wamekubaliana na ombi la Mashabiki wa Yanga Tawi la Mbeya Mjini kwamba mazishi yafanyike leo saa saba mchana. Mashabiki hao wamejitolea Jeneza.

 

2017-Ndugu zake waliondoka kwenye hospitali ya Makandana, Rungwe mkoani Mbeya juzi saa 3 usiku na kumuacha hali yake ikiwa sio nzuri sana, lakini waliporudi jana Ijumaa saa 12 asubuhi wakapewa habari mbaya kwamba ndugu yao ametangulia mbele za haki. Kwa mujibu wa ndugu wa Bonny mchezaji huyo mwaka huu wa 2017 afya yake imekuwa si nzuri, ingawa alikuwa akisimama imara kujitetea pamoja na kufanya mazoezi ya hapa na pale.

 

2012-Mchezaji huyo ambaye imeelezwa ameacha mtoto mmoja, Juni 2012 aliachwa na Yanga baada ya mkataba wake kumalizika. Aliachwa pamoja na wachezaji wengine ambao ni Bakari Mbegu, Shabaan Kado, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Julius Mrope.

Wengine ni Kiggi Makasi, Abuu Ubwa, Chacha Marwa, Atif Amour, Iddi Mbaga, Zuberi Ubwa na Pius Kisambale.

 

2010-Februari mwaka 2010 begi lake pamoja na mizigo ya wachezaji wengine wa Yanga ambao ni kipa Obren Curcovic, Jerrson Tegete na Boniface Ambani yalipotea kwenye uwanja wa ndege wa Nairobi wakati wakielekea DR Congo kucheza na FC Lupopo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hatahivyo walikuja kuyapata baadae kabisa wakati wanarudi Dar es Salaam.

 

2011-Mwezi Juni mwaka huo aliibua sekeseke kwenye mechi ya Yanga na El Merreikh katika Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam baada ya Yanga kumchomeka benchi wakitaka wamtumie kwenye kipindi cha pili, ndiyo Cecafa ikawajia juu kwavile hakuwemo kwenye usajili. Hivyo akalazimika kwenda jukwaani Yanga ikatoka sare ya mabao 2-2.

 

2014-Alipata dili kwenye klabu ya Saraswot ya nchini Nepal, lakini hata hivyo haikumnufaisha sana na wala hakucheza muda mrefu kwavile tayari mwili ulishaanza kugoma. Mwaka huo alirudi Dar es Salaam mwezi Juni na kukutana na Kocha Marcio Maximo enzi hizo akiwa bosi wa Yanga na kushauriana nae mambo kadhaa ingawa haikuwekwa wazi. Lakini mara kwa mara Bonny alikuwa hakauki mazoezini kwa Maximo.

 

6-Jezi aliyokuwa akiivaa na kuitumia mara nyingi alipokuwa ndani ya kikosi cha Yanga, huku nafasi aliyokuwa akiimudu kwa ufasaha ilikuwa namba sita ama nane uwanjani.

 

2008-Alikuwa ndani ya kikosi cha Yanga kilichovunja mwiko wa kufungwa na Simba kwa miaka saba mfululizo wakati Ben Mwalala alipofunga bao pekee katika mechi ya Oktoba 20, 2008.

 

Kikosi kilivyokuwa;

Circkovic, Nsajigwa, Nurdin, Owino, Cannavaro, Bonny, Shamte, Chuji/Mumbala, Ambani/Maftah, Mwalala na Ngassa/Makassy.