Mabondia wa Kibongo bwana

KAMA wewe ni shabiki wa michezo na hasa ngumi, ni wazi utakuwa umezoea kutumia yale majina ya utani ‘a.k.a’ ya mabondia, lakini inawezekana kabisa ukawa haufahamu maana ya majina hayo. Usikonde, Mwanaspoti, linakuletea maana na chimbuko la majina hayo kwa mabondia husika.

SNAKE MAN

Kwa tafsiri rahisi linamaanisha Mtu anayefanya mambo kwa kudokoa na kunesa kama nyoka. Katika ngumi mwenye jina hili ni Rashid Matumla, kuanzia ujana wake alifahamia Snake Boy kabla ya kulibadilisha kutoka na umri kusogea.

“Nilipewa hili jina katika mazoezi ya relwe gerezani ambako ndiko kulikuwa kama kambi ya ngumi miaka ya nyuma,” anasema mkongwe huyo.

“Kwenye kambi hiyo hakuna aliyekuwa akiniweza, kuna wakati nilikuwa nikipigana na mabondia wawili kwa wakati mmoja na ninawapiga, yaani nilikuwa nikinesa kama nyoka, hapo ndipo nikapewa jina la Snake Boy kabla sijalirekebisha kutokana na umri.”

CHAMPION

Maana yake ni Bingwa. Anayelitumia ni Japhet Kaseba. Jamaa huyu hakuwa na bahati sana kwenye ndondi, lakini nyota yake ilianza kung’aa kwenye Kick Boxing (ngumi za mateke). “Jina la Champion halijaja kwa kujipachika, mimi ni Champion kweli, katika Kick Boxing Tanzania, hakuna zaidi yangu,” anasema Kaseba.

CHICHI MAWE

Kwani wewe huyajui mawe? Basi fananisha mawe na ngumi zake. Mwenye jina hili ni Francis Miyeyusho, ni bondia anayekubalika kwa mashabiki wa ndondi, hana papara ulingoni. “Hili jina la Chichi Mawe limetokana na kipaji changu, awali walianza kuniita ‘Ngumi Jiwe’ lakini baadaye mashabiki wangu wakaona wafupishe na kuniita Chichi Mawe. Hata Gym yangu nimeipa jina hilo,” anasema.

 

SMG

Ni jina la bunduki mahiri ya kivita. Anayelitumia jina hili ni Francis Cheka. Sifa yake kuu ni uvumilivu ulingoni.

Alipoingia kwenye ndondi mwaka 2000, mashabiki wakampachika jina la SMG na mwenyewe anasema amelitendea haki jina hilo kwani kuwashikisha adabu mabondia wengi na kuwakata vilimi limi sambamba na kutwaa mataji mengi ya ubingwa ikiwamo la dunia la WBF, ndio kawaida yake.

GOLDEN BOY

Kijana wa Dhahabu. Mwenye jina hili ni Mbwana Matumla. Kwa sasa naye umri umesogea, lakini jamaa kawanyoosha wengi.

Wakati mwingine mashabiki hupenda kumwita Mtaalamu au Fundi wa Masumbwi na mwenyewe anakiri kuwa Golden Boy ni jina lililoendana naye tangu siku ya kwanza alipolisikia akiitwa hivyo.

 

KING

Mfalme. Ndilo jina la utani la Mada Maugo, ambaye pia hupenda kujiita Mbunge wa Rorya au Rais wa Wajaluo. “Nilipewa hili jina na kocha wa mpinzani wangu mmoja nilipokuwa nimekwenda Kenya kwenye pambano, nilimpiga mpinzani huyo (hamtaji) na alipoenda chini hakuamka mara moja, kocha wake akanifuata na kunipongeza akaniambia kuanzia leo wewe ni King (Mfalme) wa ngumi,” anasema Maugo.

KIBERITI

Naamini unafahamu kazi ya kiberiti. Bondia Karama Nyilawila, amepewa jina hilo baada ya jamaa kuzifananisha ngumi zake na moto unaowashwa na kiberiti.

Jamaa ni miongoni mwa mabondia wachache wa Tanzania waliowahi kutwaa ubingwa wa dunia nje ya nchi.

“Hili jina la kiberiti nilipewa na mashabiki wangu, unajua kazi ya kiberiti ni kuwasha moto, hivyo wakati wananipa jina hilo walinifananisha na kiberiti,” anasema.

AFGHANISTAN

“Jina hili (la nchi) linanikumbusha pambano langu la kuhamasisha amani ambalo nilipigana kwenye nchi hiyo ya Kiarabu kipindi ambacho kulikuwa na machafuko. Sikuhofia kwenda kule, niliporudi ndipo nikapachikwa jina la Mzee wa Afghanistan,” anasema Said Mbelwa.

MCHUMIA TUMBO

Jina hili linajieleza lenyewe. Linamhusu bondia wa uzito wa juu, Alphonce Joseph.

Anasema jina la Mchumia Tumbo alijipa mwenyewe kutokana na ugumu wa maisha. “Kila pesa niliyokuwa nikiipata iliishia kwenye kula, ndipo nikajiita Mchumia Tumbo jina ambalo limekuwa na linanitambulisha kwenye ngumi,” alisema. 

MTAMBO WA GONGO

Gongo ni pombe kali sana. Kwa kuwa ngumi zake enzi hizo zilikuwa kali, ndio maana mashabiki wakaamua kumpa jina hilo. Anayekwenda kwa jina hilo ni Maneno Oswald.

“Umaarufu wa Mtambo halisi wa Gongo unajulikana, hivyo umaarufu wangu kwenye ngumi ndio ulifanya mashabiki wanifananishe na mtambo huo. Lakini mimi sijawahi kuinywa pombe hiyo,” anasema.