KIWANGO: Makipa waliotikisa Bongo

Muktasari:

  • Angban ndiye aliyeibeba Simba kwenye mabega yake tangu nusu ya msimu uliopita na kwenye mechi za michuano ya Kombe la FA.
  • Katika mechi za duru la kwanza za msimu huu, kipa huyo aliyewahi kuichezea Chelsea ameruhusu mabao sita tu kutinga nyavuni mwake, akiwa kipa aliyecheza mechi nyingi zaidi katika duru la kwanza.

KLABU ya Simba juzi kati tu, imemleta kipa wa kutoka Ghana, Daniel Agyei. Kipa huyo mpya ameungana na Mu-Ivory Coast, Vincent Angban ambaye ana msimu wa pili Ligi Kuu Bara.

Angban ndiye aliyeibeba Simba kwenye mabega yake tangu nusu ya msimu uliopita na kwenye mechi za michuano ya Kombe la FA.

Katika mechi za duru la kwanza za msimu huu, kipa huyo aliyewahi kuichezea Chelsea ameruhusu mabao sita tu kutinga nyavuni mwake, akiwa kipa aliyecheza mechi nyingi zaidi katika duru la kwanza.

Umiliki wa makipa mawili wa kigeni, unaweza kuchukuliwa labda Tanzania ina uhaba au tatizo la wachezaji wa nafasi hiyo, kama ilivyo kwa nafasi ya ushambuliaji.

Hapana! Tanzania haijawahi kuwa na tatizo la makipa tangu nchi iwe huru mwaka 1961. Hata Simba haijawahi kushindwa kutoa makipa hodari, kwani kwa miaka mingi klabu hiyo ndiyo iliyokuwa kinara kwa kutoa makipa bora waliuotamba timu ya taifa, Taifa Stars.

Kwa ufupi ni kwamba Tanzania kwa miaka nenda rudi ilikuwa ikitamba kwa kuwa na makipa bora ambao wakati mwingine ilikuwa ikiwapa wakati mgumu makocha wa klabu ama timu ya taifa, Taifa Stars kumpanga nani mbele ya wenzake.

Labda tu ni kwamba kwa miaka ya karibuni, tangu Juma Kaseja alipoanza kuyumba kumesababisha Tanzania kukosa Tanzania One, ila ukweli kwa vipaji vya nafasi hiyo ya ukipa Tanzania imejaliwa asikwambie mtu.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya makipa waliowahi kutamba nchini na ambao unaweza kuwaweka katika kundi la makipa wa muda wote Tanzania;

OMAR MAHADHI

Huyu ndiye anayatajwa kama kipa bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania tangu uhuru kwa namna alivyokuwa na kipaji cha hali ya juu.

Kipa huyo alianzia soka lake katika timu ya African Sports na Mkoa wa Tanga kabla ya kunyakuliwa na Simba mwaka 1975 na kuichezea Taifa Stars kwa mafanikio makubwa. Kwa waliomshuhudia kipa huyo wanadai, alikuwa na umbile la kawaida tu, lakini jinsi alivyokuwa mkali langoni, aliwafanya wenzake kusubiri mbele yake. Alitetemesha sio Tanzania tu, bali mpaka barani Afrika alichuana na makipa waliokuwapo miaka hiyo.

Ndio maana haikushangaza katika Michezo ya Afrika (All Africa Games) ya mwaka 1973 iliyofanyika Nigeria, aliteuliwa kwenye timu ya Kombaini ya Afrika. Mahadhi aliteuliwa sambamba na straika aliyetamba miaka hiyo aliyekuwa Yanga, Maulid Dilunga kuunda kikosi hicho cha Afrika kilichofanya ziara mataifa mbalimbali duniani ikiwamo Mexico na nchi za Ulaya.

Mkali huyo alifariki duniani miaka ya 1980 na mpaka leo jina lake linatajwa kutokana na umahiri wake na kama hujui tu alikuwa langoni wakati Simba wakiiitia aibu Yanga kwa mabao 6-0 Julai 19, 1977.

ATHUMAN MAMBOSASA

Kipa mwingine mahiri aliyewahi kutokea nchini. Kipa Mambosasa aliyefariki miaka ya 1980, alisifika kwa umahiri wake wa kulinda lango akisaidiwa na urefu wake. Ndiye aliyekuwa kwenye kikosi cha Tanzania kilichoshiriki fainali za kwanza na mwisho za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.

Katika kikosi hicho Mambosasa aliambatana na makipa wengine Juma Pondamali ‘Mensah’ na Idd Pazi ‘Father’.

Kabla ya kutua Simba na kuidakia kwa mafanikio, akiungana na kina Omar Mahadhi, Mambosasa aliwahi kupitia Pan Africans kwa muda mfupi. Miaka inaenda na kupitia, lakini jina lake linaendelea kudumu akiwa mmoja ya makipa hodari kuwahi kutokea nchini, licha ya mapungufu aliyokuwa nayo kama wanadamu wengine.

JUMA PONDAMALI ‘MENSAH’

Utasema nini juu ya kipa huyu wa zamani wa Yanga, Pan Africans, Pilsner na AFC Leopards ya Kenya, aliyekuwa ngumi mkononi. Yaani ukimzingua anakuzingua.

Achana na vituko vyake vilivyokuwa vikimfanya afungiwe kila mara kwa makosa ya kuwapiga waamuzi ama wachezaji wenzake, lakini Pondamali alikuwa fundi bwana.

Ndiye aliyedaka kwenye mechi muhimu dhidi ya Zambia mwaka 1979 ambayo iliivusha Tanzania kwenda Nigeria kwenye fainali za Afcon 1980, ambapo huko alikuwa gumzo na kuacha simulizi la aina yake kwa udakaji wake wa mbwembwe.

Alikuwa na uwezo wa kudaka mpira kwa mkono mmoja, kumrudishia mshambuliaji mpira na kuudaka tena mpira kwa mbwembwe za kipekee kiasi cha kukera.

Kwa wanaozikumbuka fainali hizo za Afcon 1980 alipoenda na Taifa Stars na kupata nafasi ya kudaka mechi zote na katika michuano ya Kombe la Chalenji zilizofanyika Sudan wanakumbuka vitimbi vyake.

Tangu amestaafu soka karibu miaka 20 iliyopita, hajatokea kipa aliyekuwa na mbwembwe uwanjani na vituko visivyoisha kama Pondamali aliyepewa jina la utani la Mensah akifananishwa na aliyekuwa kipa mahiri ya Ghana, Robert Mensah.

IDD PAZI ‘FATHER’

Simba inatajwa kuwa klabu pekee iliyokuwa na bahati ya kuwa na makipa hodari ambao wamebaki kuwa gumzo hata baada ya kuachana na soka ama kufariki dunia.

Idd Pazi ‘Father’ ni miongoni mwa makipa bora kabisa waliowahi kutokea nchini, ambapo licha ya kuidakia Simba, pia aliwahi kuzichezea Majimaji Songea, Pilsner, na Al Merreikh ya Sudan.

Alikuwa miongoni mwa makipa walioenda Afcon 1980, ametwaa mataji kadhaa akiwa na Simba na Taifa Stars, huku akiwa ndiye muasisi wa jina la Tanzania One alilopachikwa kwa umahiri wake wa kulinda lango enzi zake.

Umakini wake langoni na kuwapanga makipa wake ulimtofautisha na wenzake, huku akiwa kipa wa kwanza kufunga bao kwenye mechi ya watani, akifanya hivyo mwaka 1985 kabla ya Juma Kaseja kuifikia rekodi hiyo mwaka 2012 Yanga ilipokufa 5-0.

Kwa sasa amepumzika masuala ya soka akisikilizia afya yake, kabla ya kukumbwa na maradhi alikuwa kocha wa makipa wa Simba.

MOHAMMED MWAMEJA

Utasema nini kwa kipa huyo wa aina yake aliyewahi kutamba na klabu za Coastal Union na Simba.

Alikuwa na umbile linalowatisha washambuliaji wa timu pinzani, kuna straika mmoja niliyewahi kumhoji alisema, Mwameja alipokuwa langoni alikuwa analiziba goli kiasi kwamba alikuwa akipata wakati mgumu kujua afungie wapi.

Ndiye aliyelirithi jina la Tanzania One na kukaa nalo kwa muda mrefu kuliko kipa yeyote, huku rekodi zake zikisisimua kwa kuweza kuifikisha Simba fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa mpaka leo na timu yoyote.

Mwameja alikuwa na uwezo mkubwa wa kudaka michomo mikali na kupanga mabeki wake na pia alikuwa na uwezo wa kuwaongoza wenzake uwanjani, pia alikuwa na mikwara iliyowafanya wachezaji wa timu pinzani kupata woga kwake.

Kwa sasa anajishughulisha na mambo ya biashara akiwa ameachana kabisa na soka, lakini jina lake linaendelea kukumbukwa kwa umahiri wake langoni enzi zake. Kuna nyakati amekuwa akimsaidia kipa Peter Manyika katika kituo chake kwa kuwanoa makipa chipukizi.

JUMA KASEJA

Hana mwili mkubwa kama makipa wenzake waliotanguliwa kutajwa hapo juu, lakini umahiri wake langoni umemfanya Juma Kaseja mpaka sasa kukosa mpinzani, hata kama hajapata wasaa wa kucheza katika miaka kadhaa iliyopita.

Uwezo wake wa kudaka michomo, kupangua penalti na kupanga mabeki wake na hata wakati mwingine kupandisha mashambulizi kulimfanya kipa huyo kuendelea kuwa gumzo, akiwa ndiye anayeshikilia mpaka sasa jina la Tanzania One, licha ya kutokuwapo kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa muda mrefu.

Hivi karibuni alisaini kuidakia timu ya mshikaji wake, Mecky Maxime, Kagera Sugar baada ya kuigomea Mbeya City aliyokuwa akiidakia msimu uliopita.

Kaseja ana vitu adimu kulinganisha na makipa wa zama hizi, jambo ambalo linamfanya kuendelea kutajwa kama kipa bora wa zama hizi, hasa ikizangatiwa kuwa kwa sasa Stars haina kipa namba moja wa kutumainiwa kama ilivyokuwa enzi zake.