Zile 2-1 za Simba, aisee Mgosi amepatia bwana

Muktasari:

  • Hata hivyo Mgosi alivyotafutwa alijitetea si kama kajigeuza Sheikh Hassan Yahya, ila huwa ni kawaida yake kutokana na kuwa na maono fulani.

MASHABIKI wa Simba wapo katika furaha kubwa baada ya timu yao kuifunga Yanga mabao 2-1, lakini kama kuna mtu ambaye amewashtua ni Meneja wao, Mussa Hassan ‘Mgosi’ kwa utabiri wake sahihi alioutoa.

Mgosi alinukuliwa na Mwanaspoti akisema Simba ingeshinda mabao mawili, lakini alisema kama Yanga ingejitahidi ingelala 2-1 jambo lililokuwa kweli na kufanya mashabiki kuhisi nyota huyo wa zamani wa Simba amegeuka mtabiri.

Hata hivyo Mgosi alivyotafutwa alijitetea si kama kajigeuza Sheikh Hassan Yahya, ila huwa ni kawaida yake kutokana na kuwa na maono fulani.

“Ninapotoa utabiri huwa nina hakika kwa sababu nakuwa na maono na vinavyotokea, hii si mara ya kwanza, hata kipindi kile nacheza ilikuwa hivyo, nikiwaambia wenzangu mechi ya leo tutashinda inakuwa hivyo na nikiwaambia tunafungwa huwa hivyo,” alisema.

“Pamoja na kulelewa na mama yangu, mimi naamini baraka nyingi kutoka kwa babu na bibi zangu, nikiamini kitu kinakuja na nakuwa na ujasiri wa kuzungumza ndiyo maisha yangu,” alisema Mgosi.

Kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed ‘Nduda’ ambaye ni mtu wake wa karibu na alicheza na Mgosi alisema: “Mgosi ndio tabia yake kutabiri ni rafiki yangu namjua, wakati tunacheza naye Mtibwa akisema leo nafunga ujue atafunga kweli na akisema tunashinda inakuwa hivyo sisi tumeshamzoea.”

Mavugo Mzuka umepanda

Laudit Mavugo aliyefunga  bao la kwanza lililokuwa la kusawazisha la Simba kabla ya Shiza Kichuya kumalizia la ushindi, alisema anafanya vizuri kwa kuaminiwa na Kocha Joseph Omog na kwamba mzuka kwake ndio kwanza umepanda.

“Unajua mwanzoni sikujiamini nilipoteza morali baada ya kuja hapa nikakosa nafasi jambo lililochanganya akili yangu kwa kiasi kikubwa na kama unavyojua mtu akikaa benchi sana anapoteza makali,” alisema Mavugo.

“Lakini sasa napata nguvu kwa sababu naminiwa kucheza hivyo sitawaangusha kabisa, sina ugeni tena nimeshazoea mazingira ya hapa na kila kitu, hakuna kitakachonishinda. Sasa ni wakati wangu kutoa zawadi kwa wana Simba.”

Kaduguda bado Haamini

Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ amekiri kwamba kwa uzoefu wake tangu alipoijua Simba, bado haamini kama itaumaliza vema msimu kwa sababu mara nyingi tiu hiyo huharibu mwishoni.

“Simba tunaongoza ligi lakini bado nina wasiwasi kwa sababu nina uzoefu na klabu hii, inaweza kuwa vizuri na kuongoza ligi kwa kipindi kirefu mwanzoni na inakuja kuanguka katika mechi za mwishoni na hivyo inatubidi tuwe makini,” alisema.

Kaduguda aliyekuwa Katibu Mkuu enzi za Hassan Dalali na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009-2010 bila kupoteza mechi alisema hali hiyo ya Simba kuyumba inachangiwa na makundi, hivyo kuhimiza umoja kipindi hiki.

Kichuya adondosha 18

Kama hujui ni kwamba kwa sasa imekuwa kama kawaida kila mechi ya Simba na Yanga mashabiki kudondoka na kuzimia uwanjani kama ilivyotokea juzi Jumamosi.

Kazi nzuri ya Shiza Kichuya iliwawadondosha watu 18 Uwanja wa Taifa na kulazimika kupatiwa matibabu, lakini wanne kati yao walipelekwa Hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi.

Daktari, Nassor Matuzya, ambaye ni Katibu wa Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (Tasma), aliyekuwa miongoni mwa watoa huduma uwanjani hapo,  alisema kati ya wagonjwa hao, 10 walikuwa mashabiki wa Simba na wanane wa Yanga. Dk Matuzya alisema mashabiki hao tisa walikuwa wanaume na wengine kama hao ni wanawake.