jose Mourinho aliwavuruga mastaa hawa

Muktasari:

Mourinho alidai Shaw kile anachokionyesha akiwa mazoezini ni tofauti kabisa na anapokuwa uwanjani kwenye mechi, hivyo bado ana safari ndefu na anapaswa kuboresha kiwango chake. Kiungo Nemanja Matic amesema Mourinho ni kocha anayehitaji zaidi na zaidi kutoka kwa wachezaji wake, hivyo amedai suala la Luke Shaw si shambulio binafsi kwa mchezaji huyo.

MANCHESTER, ENGLAND

LUKE Shaw ni mchezaji wa mwisho kukutana na domo la Jose Mourinho akimkosoa hadharani mbele ya waandishi wa habari baada ya kucheza kwa kiwango cha chini kwenye mechi ya ushindi dhidi ya Brighton katika Kombe la FA.

Mourinho alidai Shaw kile anachokionyesha akiwa mazoezini ni tofauti kabisa na anapokuwa uwanjani kwenye mechi, hivyo bado ana safari ndefu na anapaswa kuboresha kiwango chake. Kiungo Nemanja Matic amesema Mourinho ni kocha anayehitaji zaidi na zaidi kutoka kwa wachezaji wake, hivyo amedai suala la Luke Shaw si shambulio binafsi kwa mchezaji huyo.

Hata hivyo, beki huyo wa kushoto Mwingereza Shaw si mchezaji wa kwanza kushambuliwa kwa maneno hadharani na Kocha Mourinho kwa kuwaeleza waandishi wa habari na badala ya kwenda kuzungumza na mchezaji husika kwenye vyumba vya kubadilishia nguo au ofisini kwake.

Ricardo Carvalho

Beki Mreno, Carvalho alikuwa kama kibegi cha Mourinho baada ya kuhama naye kwenye timu kadhaa alizowahi kuzinoa. Walibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa pamoja katika klabu ya FC Porto, kabla ya kwenda wote Chelsea kisha Real Madrid. Hata hivyo, si mara zote mambo yalikuwa mazuri baina ya wawili hao.

Carvalho alionekana kupatwa na hasira baada ya kupoteza namba mbele ya William Gallas kwa mara ya kwanza kwenye msimu wa 2005/06, na Mourinho hakutaka kuficha mambo akaamua kumchana hadharani Carvalho kupitia vyombo vya habari.

“Ricardo Carvalho anaonekana kuwa na matatizo ya kuelewa vitu. Pengine anapaswa kufanyiwa vipimo vya akili,” alisema Mourinho.

“Sikufurahishwa na maneno yake niliyosikia ambayo ameyatoa kwenye magazeti. Ricardo amefanya kazi na mimi kwa miaka minne, hivyo sielewi kabisa hayo maneno yake, nadhani anahitaji kwenda kuonana na daktari.”

Pepe

Beki wa kati ambaye kwa muda mrefu aliichezea Timu ya Taifa ya Ureno sambamba na beki wa kati Ricardo Carvalho. Lakini, Pepe ambaye pia aliitumikia Real Madrid kwa miaka 10 na kufanikiwa kushinda mataji matatu ya La Liga na matatu mengine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiwa mchezaji mwenye sauti kubwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo huko Bernabue, Pepe aliona achukue nafasi hiyo kumtetea kipa Iker Casillas baada ya Kocha Mourinho kuamua kumpiga benchi Mhispaniola huyo.

Kwa uamuzi huo wa Pepe kumtetea nahodha wake, Mourinho aliona hilo si jambo zuri na kusema: “Pepe ana matatizo. Na jina lake ni Raphael Varane,” hayo yalikuwa maneno ya Mourinho wakati alipoanza kumtumia beki Mfaransa, Varane.

“Hiyo ndiyo stori nzima. Si sirahisi kwa mtu mwenye umri wa miaka 31 na mwenye uzoefu wa kutosha kuweka benchi na kinda wa miaka 19. Ndiyo hivyo, tatizo ni hilo. Maisha ya Pepe yamebadilika.”

Sulley Muntari

Kiungo Muntari ulikuwa usajili wa kushtukiza wakati Inter Milan ilipolipa Pauni 12 milioni kumnasa kutoka Portsmouth mwaka 2008, lakini alikwenda kucheza mechi 27 tu za Serie A katika misimu yake miwili huko San Siro, huku msimu wa pili akifanikiwa kunyakua mataji matatu makubwa kwa msimu mmoja. Mwanzoni mwa msimu tu, Mourinho alitibuana na Muntari kwa imani yake ya kidini, baada ya kuonekana kupinga uamuzi wa mchezaji huyo kufunga Mwezi wa Ramadhani. Mourinho alidai funga inamfanya mchezaji asiwe na maarifa zaidi ya kucheza kwa nguvu ndani ya uwanja jambo lililomfanya kumchezesha kwa nusu saa tu kiungo huyo wa Ghana kwenye mechi dhidi ya Bari.

Baadaye Mourinho alikwenda kusema hadharani: “Muntari alikuwa na matatizo kidogo kuhusu Mfungo wa Ramadhani. Kutokana na joto lililopo kwa sasa sidhani kama anahitaji kuwa kwenye swaumu. Ramadhani haikuja kwenye kipindi kizuri kwa mchezaji, hasa anayepaswa kucheza mechi.”

Eden Hazard

Hazard alifurahia misimu miwili ya kucheza chini ya Mourinho kabla ya mambo kutibuka. Chini ya kocha huyo Chelsea iliweza kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England katika awamu yake ya pili, lakini awamu yake ya kwanza ya Mourinho klabuni hapo, alibeba taji hilo pia zaidi ya mara moja. Licha ya wawili hao kuwa vizuri kufikia hatua ya Mourinho kumpandisha kiwango Hazard akidai yupo kwenye viwango vya kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, walitibuana baada ya Chelsea kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Atletico Madrid. Baada ya Hazard kuzungumza katika moja ya vyombo vya habari vya Ufaransa kwamba Chelsea haikuwa imejiandaa kucheza mpira, Mourinho alifyatuka na kujibu kwa maneno anayofahamu yeye, hadharani akisema.

“Ni kweli kwa sababu yeye si mchezaji ambaye yupo tayari kujitolea mhanga kwa asilimia 100 kwa ajili ya timu na wachezaji wenzake. Eden si mchezaji ambayo amepevuka kiakili kuwa na mawazo ya kumtazama beki wa upande anaocheza ili kumsaidia kumpunguzia majukumu ya ndani ya uwanja.”

Joe Cole

Kiungo huyo mchezeshaji wa Kingereza aliaminika ni kizazi matata kabisa cha soka kilichowahi kutoka ndani ya England hasa kwa kipindi chake alichokuwa akicheza West Ham United. Chelsea ilimsajili mwaka 2003 kwa ada ya Pauni 7 milioni baada ya Bilionea Roman Abramovich kuanza kuimiliki klabu hiyo ya Stamford Bridge. Joe Cole alianza maisha yake ya Stamford Bridge vizuri akifunga bao muhimu kwenye mechi dhidi ya Liverpool. Joe Cole aliyekuwa anayependa kushambulia, lakini hakuwa mzuri kwenye kuzuia, hilo halikumfurahisha Mourinho na hapo akaamua kumpiga chini.

“Ana mengi ya kujifunza,” alisema Mourinho kuhusu Joe Cole na kuongeza. “Nadhani ana sura mbili, moja nzuri sana nyingine siipendi. Abaki na moja na nyingine aibadilishe. Yeye akiwa amefunga bao tu, basi mechi kwake imekwisha. Hajishughulishi kuzuia hilo bao alilofunga lisirudi. Hivyo, timu inakuwa imebaki na watu 10 tu uwanjani, si 11.”

Bastian Schweinsteiger

Licha ya kuwa na uzoefu mkubwa kutokana na kucheza mechi nyingi kubwa na kubeba mataji makubwa akiwa na Bayern Munich na Ujerumani, Schweinsteiger haukuwa usajili wa maana kwenye kikosi cha Manchester United wakati aliponaswa na Kocha Louis van Gaal mwaka 2015. Matatizo ya majeruhi yalimtibulia nyakati zake za mwisho akiwa na Bayern na ndizo zilizomfanya aondoke mapema Old Trafford baada ya msimu wake wa kwanza kucheza nusu tu. Mourinho akaja kumrithi Van Gaal mwaka uliofuatia na ghafla tu akaanza kumpiga chini kiungo huyo wa Kijerumani. Mourinho alimwambia staa huyo na uzoefu wake wote aende akafanye mazoezi na timu ya vijana na mwaka uliofuata akaamua kwenda zake Chicago Fire ya Marekani.

Hata hivyo, Mourinho alionekana kujutia namna alivyomfanyia staa huyo na kusema: “Ni aina ya wachezaji ambao najisikia vibaya kwa nilichomtendea. Nataka kumzungumzia kiprofesheno, kama mwanadamu pia. Hicho ndicho kitu cha mwisho nilichomwambia kabla hajaondoka, sikuwa sawa na wewe huko nyuma, nimekuwa sawa na wewe wakati huu.”

Kevin De Bruyne

Staa, Kevin De Bruyne anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kiwango chake matata kabisa huko Manchester City na hakika jambo hilo linaifanya Chelsea ijichukie yenyewe kutokana na kumwaachia Mbelgiji huyo aondoke kwenye kikosi chake miaka minne tu iliyopita.

Tangu alipoondoka Chelsea mwaka 2014, De Bruyne ameweza kuboresha kiwango chake cha uchezaji na kuwa mkali zaidi baada ya kuwa chini ya Pep Guardiola huko Man City, wakati Mourinho hakutaka kabisa kumpa muda wa kutosha mchezaji huyo walipokuwa pamoja Stamford Bridge.

“Kuhusu De Bruyne, kama unakuwa na mchezaji ambaye kila siku anakufuata ofisini kwako na kulia akitaka kuondoka, unapaswa kuchukua uamuzi. Kwa wakati ule, Chelsea ilikuwa inafanya vizuri,” alisema Mourinho mwaka 2015 na kuongeza: “Lakini, kama angeendelea kubaki Chelsea, asingeenda Wolfsburg, asingefikia kiwango alichofikia kwa sasa. Kipindi kile hakuwa tayari kupigania namba. Alikuwa kijana mwenye mawazo, mazoezini alikuwa hivyo.”

Romelu Lukaku

Kwa sasa wako vizuri na jambo zuri hawakuwa wametibuana sana hasa baada ya Lukaku mwaka jana kukubali kusaini kuichezea Man United inayonolewa na Jose Mourinho. Lakini, mwaka 2013, wakati wawili hao walipokuwa Chelsea, Mourinho wala hakuona shida kumkosoa Lukaku hadharani na kumpeleka kwa mkopo Everton.

“Romelu anapenda kuongea. Ni kijana mdogo anayependa kuongea,” alisema Mourinho akijibu moja ya malalamiko ya Lukaku katika moja ya mahojiano yake aliyoyafanya kabla ya mechi na kuongeza. “Lakini, kitu pekee ambacho hakutaka kusema ni kwanini ameenda kwa mkopo Everton. Hicho ndicho kitu ambacho hatakisema. Mara yangu ya mwisho kuwasiliana naye, ilikuwa nilipomwambia: ‘Kwanini huwaambii watu sababu ya kukufanya usiwe Chelsea?’.”

Alichojaribu Mourinho ni kutaka kuutaarifu umma kwamba hakuhusika katika mchakato mzito wa Lukaku kupelekwa Everton kwa mkopo.

Cristiano Ronaldo

Mourinho alikuwa na nyakati ngumu Real Madrid, wakati alipojaribu kuondoa utawala wa Barcelona na kujaribu kumwingiza supastaa Cristiano Ronaldo kwenye mipango yake.

Jambo hilo halikuwa na mapokeo mazuri baada ya Mourinho kumwambia Ronaldo anapaswa kuwa mwelewa kwenye mbinu za mchezo na hapo kupigilia misumari kwenye jeneza lake.

“Nina tatizo moja tu na Ronaldo,” alisema Mourinho mwaka 2013. “Ni kitu rahisi sana, kocha anapomkosoa mchezaji kwa mtazamo wa kujaribu kuboresha mbinu, kwa mtazamo wangu mchezaji husika anapaswa kujitathmini.” Hayo yalikuwa maneno ya Mourinho yaliyomlenga Ronaldo ambayo aliyasema hadharani mbele ya waandishi wa habari.