Zahera awajaza upepo nyota Yanga

Muktasari:

  • Zahera alitimkia akiwa Rwanda wakati Yanga ikifa kwa bao 1-0 mbele ya Rayon Sports katika mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika na juzi jioni vijana wake walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya African Lyon na kushinda bao 1-0.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera mjanja sana wakati anatimka zake kwenda DR Congo kwa majukumu ya timu ya taifa ya nchi yake, huku nyuma aliamua kuwajaza upepo nyota wake ili akirudi kila kitu kiwe sawa.

Zahera alitimkia akiwa Rwanda wakati Yanga ikifa kwa bao 1-0 mbele ya Rayon Sports katika mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika na juzi jioni vijana wake walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya African Lyon na kushinda bao 1-0.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Yusuf Mhilu aliyeingia akitokea benchi akimpokea Mrisho Ngassa na Kocha Msaidizi, Noel Mwandila alifichua, bosi wake alitaka wachezaji mechi za kirafiki ili kujiweka fiti na akija mambo yawe mambo.

Kocha Mwandila alisema Zahera alitaka Yanga icheze mechi za kirafiki ili amuangalie kila mchezaji alipofikia kwa kile anachowaelekea mazoezini, ili atakaporudi asiwe na kazi kubwa ya kufanya kabla ya mechi zao za Ligi Kuu Bara wikiendi hii.

Mwandila alisema katika mapumziko mafupi ya Ligi ili kupisha mechi za kimataifa za timu za Taifa Kocha Zahera alitaka wachezaji wafanye mazoezi mepesi na mbinu nyingi ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake kutokana na nafasi yake.

"Kumekuwa na mapokeo makubwa ya kile ambacho Zahera alikuwa anahitaji niwape wachezaji, lakini tutaimarika zaidi pale wachezaji waliokuwa timu ya taifa wakijiunga na wenzao.

"Kile ambacho Zahera aliniachia niwape wachezaji nimewapa na kuelekea mechi ya Jumapili dhidi ya Stand United nadhani tutakuwa na kikosi kizima chenye kiu ya kuhakikisha tunapata pointi tatu uwanja wa nyumbani

"Kesho Jumanne tutaendelea na mazoezi uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, nadhani nyota waliokuwa na Stars watakuwa miongoni mwetu," alisema Mwandila.