Zahera ashusha nondo mpya

Muktasari:

  • Zahera aliianza kazi hiyo juzi Alhamisi jioni ambapo kama wachezaji wake watashika kile anachowaelekeza, basi itakuwa kazi kubwa kuipita ngome ya Yanga na kulifikia lango lao.

KOCHA, Mwinyi Zahera, ameendelea kukisuka kikosi chake cha Yanga sasa akigeukia mifumo na ameanza kujaribu mifumo miwili hatari itakayowasumbua wapinzani.

Zahera aliianza kazi hiyo juzi Alhamisi jioni ambapo kama wachezaji wake watashika kile anachowaelekeza, basi itakuwa kazi kubwa kuipita ngome ya Yanga na kulifikia lango lao.

Katika mazoezi hayo, Mkongomani huyo alianza kwa kuwatengeneza wachezaji wake kwa mfumo wa 4-4-1-1 ambao unahitaji viungo wengi kati.

Katika mfumo huo, Zahera anataka kuona kila mchezaji akikaba kwa nguvu na kuleta ugumu mabeki kufikiwa kirahisi.

Kocha huyo alionekana kuwapa kazi ya kukaba zaidi wachezaji Deus Kaseke, Raphael Daudi, Mrisho Ngassa, Pappy Tshishimbi na Feisal Salum.

Hata hivyo, wachezaji hao walitakiwa kubadilika kwa haraka kwa kukimbiza na kusaidia kutengeneza mashambulizi mara wanaponasa mipira.

Mfumo mwingine ambao kocha huyo alionekana kuujaribu jana Ijumaa ni ule wa 4-5-1 ambao mara nyingi umekuwa ukijitokeza wakati timu hiyo inaposhambuliwa.

Akizungumzia hilo, Zahera alisema bado kazi hiyo inaendelea lakini kuhusu mifumo kamili ataijaribu katika mchezo wa kesho dhidi ya Mawenzi utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri.

Lakini alisema ana imani timu yake itakuwa na mabadiliko makubwa msimu mpya.