Yondani aivua ubingwa Simba mapema

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti Yondani alisema anajua kikosi chao kinadharaulika, lakini Yanga ina timu imara ambayo itawashangaza watu mwishoni mwa msimu.

BEKI Kelvin Yondani amefungua kinywa chake na watani wa Yanga, Simba lazima wasikilize kwa makini kwa sababu jamaa amewatoa hofu mashabiki wa Jangwani akiwaambia wasiwe na wasiwasi ubingwa msimu ujao lazima urejee Jangwani.

Yondani aliyewahi kuichezea Simba kabla ya kutua Yanga mwaka 2012, amesema mabosi wa Yanga wakifanya jambo moja tu la kuongeza mtu mmoja tu katika dirisha dogo, basi watani zao hawana chao katika Ligi Kuu Bara 2018-2019.

Akizungumza na Mwanaspoti Yondani alisema anajua kikosi chao kinadharaulika, lakini Yanga ina timu imara ambayo itawashangaza watu mwishoni mwa msimu.

Nahodha huyo alisema kusajiliwa kwa Feisal Salum na Mohamed Issa ‘Banka’ katika kiungo na kuongezwa kwa Deus Kaseke na Mrisho Ngassa basi timu yao itafanya makubwa.

Yondani alisema hatua ya wao kudharaulika itawapa akili kubwa kuhakikisha wanafanya kazi bila presha ambapo macho yote yatakuwa kwa Simba wanaoonekana wako sawa.

Beki huyo alisema kilichosalia katika timu yao ni kuongezwa kwa straika mmoja mwenye nguvu mithili ya Obrey Chirwa atakayesaidiana na Heritier Makambo katika safu yao ya ushambuliaji.

“Watu wanaamini Simba ina timu bora, inawezekana lakini tunataka kutumia nafasi hii ya kubezwa ili tufanye vizuri, wachezaji walioongezwa naamini watatubeba,” alisema.

“Ukiangalia mazoezi tunayofanya sasa na jinsi watu wanavyopambana tutafanya kitu tofauti ambacho hakitarajiwi na watu, ninachowaomba mashabiki wawe nyuma yetu.”

Vijana wa Zahera wampiga mtu mkono

YANGA imecheza mchezo wake wa kwanza jana Jumatani ikitesti mitambo chini ya Kocha Mwinyi Zahera na yale maneno ya beki Juma Abdul yametimia baada ya kumpiga mtu mabao 5-1, huku kocha wao akitaka mechi ngumu zaidi.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Kanisa Bigwa, Yanga ilichezesha vikosi viwili kimoja kila kipindi na mpaka dakika 45 za kwanza tayari walishapachika mabao 4-1.

Mabao hayo yalifungwa na winga mkongwe Mrisho Ngassa aliyepiga bao safi dakika saba tu kabla ya jamaa Tanzanite Akademi kusawazisha dakika tatu baadaye.

Jamaa wakacharuka na kurudi tena kuongoza wakipata bao safi dakika 15 likifungwa kwa shuti kali na kiungo Deus Kaseke huku Heritier Makambo akifunga la tatu dakika ya 28 akigongeana vyema na Ngassa.

Pius Buswita aliipatia Yanga bao la nne akitengenezewa na Ngassa kufuatia Makambo kumtoka kipa na kumpa pasi safi Ngassa na kikosi chao kumaliza na ushindi huo.

Kocha Mwinyi Zahera alianza na kikosi chenye nyota kama Benno Kakolanya, mabeki Juma Abdul, Mwinyi Haji, Andrew Vincent, Abdallah Shaibu, viungo wakiwa Feisal Salum, Deus Kaseke, Pius Buswita, Heritier Makambo, Mrisho Ngassa na Raphael Daudi kilichomaliza na ushindi huo.

Kipindi cha pili Zahera alibadilisha kikosi kizima ambacho nacho kilitengeneza bao moja pekee lililofungwa na Emmanuel Martin akimalizia kazi safi ya kiungo Edward Maka.

Kikosi hicho kilikuwa na nyota Klause Kindoki, Juma Mahadhi, Gadiel Michael, Pato Ngonyani, viungo wakiwa Thabani Kamusoko, Jafary Mohamed aliyetolewa na kuingia Maka, Said Juma, Yusuf Mhilu aliyetolewa na kuingia Martin wakati washambuliaji wakiwa Amissi Tambwe na Matteo Anthony

Daktari Yanga amficha Tshishimbi

BEKI aliye pia nahodha wa Yanga, Yondani aliukosa mchezo wa kwanza jana baada ya kupata malaria huku kiungo Papy Kabamba Tshishimbi naye akiwekwa chini ya uangalizi wa daktari wa timu hiyo, Dk. Edward Bavu.

Yondani juzi alifanya mazoezi vizuri lakini alipofika hotelini alijikuta akiugua ghafla na kukimbizwa hospitalini, lakini hata hivyo jana alionekaa kuanza kuwa sawa.

Mbali ya Yondani, Tshishimbi naye aliukosa mchezo huo dhidi ya Tanzanite Akademi kufuatia kupata maumivu ya nyama za paja.

Tshishimbi alipata maumivu hayo juzi jioni wakati akiwa katika zoezi la kupiga mashuti makali walilokuwa wanafanya kikosi kizima.

Baada ya zoezi hilo kiungo huyo alishindwa kuendelea na wenzake na kutoka nje ambapo alianza kupatiwa matibabu na Dokta Bavu.

Kaimu Msemaji wa Yanga, Godlisten Anderson ‘Chicharito’ alisema maumivu hayo si makubwa kwa mujibu wa daktari wao na tayari amepatiwa matibabu huku akifuatiliwa kwa karibu.

“Tshishimbi amepata maumivu ya nyama, ila jana (juzi) ileile alitibiwa na sasa yuko sawa, lakini madakari wamemtaka apumzike leo (jana) ili awe sawa zaidi hata Yondani naye ameamka na malaria naye anaendelea vyema,” alisema Chicharito.

Mkongo ataka tatu ngumu amalize kazi

KOCHA Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kuanzia kesho ameagiza atafutiwe mechi tatu ngumu kaba ya kukutana na Waarabu wa USM Alger.

Akizungumza na Mwanaspoti Zahera amesema baada ya mechi ya jana anataka kutafutiwa mechi tatu ikiwezekana hata kama kuna timu tatu katika mkoa mmoja ziungane.

Zahera alisema kikosi chake sasa kinahitaji mechi ngumu ambazo zitamsaidia kujua ubora wa wachezaji wake kabla ya kukutana na USM Alger Agosti 19.

Kocha huyo alisema ameambiwa anaweza kupata mechi mbili hapa mkoani Morogoro lakini bao hazitoshi kulingana na ubora wa timu a hapa.

“Tumeshinda lakini sio aina ya timu niliyokuwa nataka hii ni nyepesi sana nimewaambia wanitafutie zingine tatu ngumu,” alisema Zahera.

“Tunahitaji mechi hizo kujua ubora zaidi wa wachezaji wetu ikiwezekana hata kama kuna mkoa una timu tatu basi ziungane tupate moja ngumu na kwingine moja,” alisema Zahera aliyetua Jangwani hivi karibuni akitokea DR Congo.