Yanga yaweka mtego Simba

Muktasari:

Yanga inaanza kibarua cha kucheza mechi hizo 11 mfululizo jijini ikiwa na rekodi tamu ya kutopoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu dhidi ya timu tofauti na Simba au Azam pindi inapocheza nayo Dar es Salaam

Dar es Salaam.YANGA imezitegea bomu kubwa Simba na Azam ambazo kama zikishindwa kulishtukia na kujipanga vyema, zitausikia ubingwa wa Ligi Kuu Bara hewani.
Ratiba ya kucheza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu ikiwa hapa jijini, ni mtego ambao unaweza kuibeba Yanga kwenye mbio za ubingwa mbele ya Azam na Simba ukichagizwa na rekodi moja ya kibabe ambayo vijana hao wa Jangwani wameiweka kwa miaka tisa mfululizo.
Yanga inaanza kibarua cha kucheza mechi hizo 11 mfululizo jijini ikiwa na rekodi tamu ya kutopoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu dhidi ya timu tofauti na Simba au Azam pindi inapocheza nayo Dar es Salaam.
Michezo hiyo mfululizo ya ligi ambayo Yanga itacheza ikiwa Dar es Salaam ni dhidi ya Stand United, Coastal Union, Singida United, Mbao FC, Alliance, Lipuli na Ndanda ambayo watakuwa uwanja wa nyumbani pamoja na ile dhidi ya Simba, JKT Tanzania, KMC na African Lyon ambayo watahesabika kama wapo ugenini.
Rekodi za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kuwa ni Azam na Simba tu ambazo zimeonja ladha ya kuifunga Yanga pindi mechi ya ligi inapochezwa hapa jijini huku ushindi pekee kwa timu nyingine ukiondoa hizo mbili, ni sare tu.
Ingawa baadhi ya timu zimekuwa zikiibuka na ushindi pindi zinapocheza na Yanga, kwenye viwanja vyao vya nyumbani huko mikoani, mambo ni tofauti zinapokutana nayo ama kwenye Uwanja wa Taifa ama Uhuru jijini.
Tangu ilipopoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Villa Squad, Aprili 27, 2009 kwa mabao 5-4, Yanga imetimiza siku 3,429 bila kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya timu nyingine tofauti ya Azam FC na Simba ambapo, imekuwa ikiibuka na ushindi mara kwa mara au kutoka nazo sare.
Rekodi hiyo inazilazimisha Simba na Azam kuhakikisha zinavuna pointi ambazo zitakwenda sambamba na Yanga hadi pale itakapomaliza ratiba ya kucheza mechi hizo mfululizo jijini, vinginevyo itakula kwao.
Wakati Yanga wakila raha jijini, Azam na Simba zenyewe zitalazimika kusafiri kwenda mikoani kucheza baadhi ya mechi za ligi ambapo katika mechi 11, Simba itacheza ugenini dhidi ya timu za Ndanda, Mbao na Mwadui wakati Azam yenyewe itaenda ugenini kucheza na Mwadui, Biashara United, Alliance, Singida United na Kagera Sugar.
Matokeo mazuri katika mechi za Ligi Kuu ambazo imekuwa ikicheza jijini, yamekuwa na neema kwa Yanga kwani kwa kiasi kikubwa ndio hutoa mchango mkubwa kwao kutwaa ubingwa au kufanya vizuri kwenye ligi kulinganisha na yale ambayo wamekuwa wakipata kwenye mechi za mikoani.
Katika msimu uliopita ambao Yanga ilimaliza kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 52, pointi ambazo ilivuna kwa mechi ilizocheza hapa jijini zilikuwa 34, zilizotokana na ushindi wa mechi 9, sare 7 na kufungwa michezo miwili tu kati ya 18 iliyocheza.
Mechi hizo mbili ambazo Yanga ilifungwa zilikuwa dhidi ya Azam FC walipopoteza kwa mabao 3-1 na dhidi ya Simba walipofungwa bao 1-0.
Kati ya mabao 44 ambayo Yanga iliyafunga msimu uliopita, 31 iliyapata kwenye mechi ilizocheza jijini na kati ya mabao 23 iliyofungwa, 13 iliyoruhusu pindi ilipocheza Dar es Salaam.
Msimu wa 2016/2017 ambao Yanga ilitwaa ubingwa, ilikusanya jumla ya pointi 68 ambapo kati ya hizo, 51 ilizipatia jijini ikishinda mechi 16 kati ya 20, ikitoka sare mitatu na kufungwa mmoja huku 17 tu ikizivuna mikoani.
Hata hivyo, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema timu yake inajipanga kuhakikisha inapata ushindi kwenye mechi hizo na suala la rekodi halipi kipaumbele.
"Tumerejea kwenye mechi za ligi na mtihani ulio mbele yetu ni kushinda mechi zilizo mbele yetu hivyo jambo la muhimu ni kuwa na maandalizi mazuri ili tuweze kutimiza lengo tulilojiwekea.
Sitaki kuangalia sana kilichotokea nyuma kwani wapinzani wanabadilika hivyo kinachotakiwa ni sisi kuwa fiti kuhakikisha hatupotezi mchezo wowote," alisema Zahera.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameitamaza ratiba ya Yanga na kutamka kuwa haimpi shida kwani, anatazama zaidi mechi zake.  
Aussems alisema ratiba imepangwa hawezi kubadilisha chochote ila atakachokifanya ni kukiandaa vyema kikosi chake.
"Nikifanikiwa kushinda kila mechi na wanaocheza nyumbani wakashindwa kufanya vizuri watakuwa hawana faida ya kutumia uwanja huo hapo unapokuwa uwanja wa nyumbani unapata faida nyingi kama uwepo wa mashabiki wa uwanja mzuri.
"Kwangu sioni sababu ya kuwaangalia zaidi wapinzani kuliko kuandaa timu yangu na ratiba hayo ni mambo ya viongozi wa Shirikisho, " alisema Aussems.