Yanga yanasa mashine mpya

Muktasari:

  • Rekodi tamu za Mugalu katika Ligi Kuu ya Zambia ndio zimewashtua viongozi wa Yanga na kuamua kuanza mchakato wa kunasa saini yake haraka tena kwa kushtukiza.

MABOSI wa Yanga wanafanya mambo kimya kimya na sasa wako kwenye harakati za kunasa saini ya straika matata wa Zambia, Chriss Mugalu ambaye ujio wake unaweza kuwaondoa kikosini baadhi ya nyota wa kigeni akiwemo Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Rekodi tamu za Mugalu katika Ligi Kuu ya Zambia ndio zimewashtua viongozi wa Yanga na kuamua kuanza mchakato wa kunasa saini yake haraka tena kwa kushtukiza.

Hata hivyo, Yanga inaweza kukupambana na vita ngumu kunasa saini ya Mugalu kutokana na straika huyo wa Lusaka Dynamo kutakiwa na klabu nyingi za Zambia.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga wamejipanga kuhakikisha wananasa huduma ya Mugalu kwa ajili ya kumtumia kwenye michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara.

Katika msimu uliopita, Mugalu alifunga mabao 20 na kuibuka kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Zambia, na sasa anataka kuondoka kwenye ligi hiyo jambo linalowapa mzuka mabosi wa Yanga kuwa na uhakika wa kumnasa. Straika huyo raia wa DR Congo ameshapachika mabao 19 msimu huu akichuana na straika Mkenya, Jesse Were anayekipiga Zesco United.

“Tumemuangalia mara kadhaa ni mshambuliaji mzuri sana, atatusaidia katika michuano ya kimataifa na VPL. Mchakato unakwenda vizuri sana, lakini hatuwezi kuzungumza sana hadi mambo yakamilike,” alisema bosi mmoja wa Yanga.

Hata hivyo, inaaminika kuwa Yanga inataka kutumia kocha wake aliyeondoka klabuni hapo, George Lwandamina kufanikisha usajili huo kutokana na wawili hao kuwa na uhusiano mzuri.

Kocha wa zamani wa Simba, ambaye anakinoa kikosi cha Lusaka Dynamos, Patrick Phiri amefichua kuwa, Mugalu ni miongoni mwa wachezaji matata aliowahi kuwafundisha. Hata hivyo, taarifa za kuondoka kwa Mugalu zimekuwa zikimvuruga kichwa kutokana na kumtegemea zaidi kufanya kazi yake ya kupasia vyavuni kwa wapinzani. Lusaka Dynamos iko nafasi ya 11 kwenye msimamo na Mugalu ana kiu ya kucheza michuano ya kimataifa hivyo, kuipa nguvu Yanga kumwania kwa kasi.

Mbali na Yanga na klabu za Zambia, Azam FC pia imetajwa kutaka huduma ya Mugalu na kwamba, imeweka mezani ofa ya Dola 60,000 huku thamani yake halisi ikitajwa Dola 1milioni.

Tshishimbi ANA DILI

Kiungo wa Yanga, Pappy Kabamba Tshishimbi anafahamu kabisa kikosi chake kinakabiliwa na uhaba wa washambuliaji kutokana na Tambwe na Ngoma kuwa majeruhi hivyo, kubaki na Obrey Chirwa pekee. Hilo limemshtua na kuwauma sikio mabosi wake akiwashauri kufanya haraka kusajili mshambuliaji matata ili kuongeza mabao.

Tshishimbi amesema kuwa, kama Yanga itasajili straika matata basi kikosi chao kitatisha zaidi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Yanga tuna kikosi imara na matatizo ya kiuchumi yakipatiwa ufumbuzi basi tutakuwa na kikosi matata sana. Ili kupata mafanikio katika michuano ya kimataifa ni muhimu kuwa na kikosi imara chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Tshishimbi na kuongeza:.

“Unajua Yanga ni imara sana na tunaweza kushindana na timu yoyote Afrika kama tukiboresha kidogo kikosi chetu hasa eneo la ushambuliaji.”