Yanga yamtibulia dili Wanyama

NAHODHA wa Kenya na kiungo fundi wa Tottenham Hotspurs amepanga kurejea tena nchini wiki mbili zijazo kushuhudia mashindano ya Kombe la Kagame, lakini huenda atashindwa kushuhudia mechi ya watani wa soka Tanzania, Simba na Yanga baada ya Vijana wa Jangwani kuchomoa kushiriki.

Wanyama yuko mapumzikoni nchini akizunguka katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam na Visiwa vya Zanzibar na leo anatarajiwa kurejea kwao Kenya, baada ya juzi kuhudhuria uzinduzi wa Ndondo Cup.

Wanyama ambaye mapumziko yake yatamalizika mwezi ujao kabla ya kurejea England kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya nchini humo, amefichua atarejea nchini kushuhudia mechi za Kombe la Kagame ambalo halikuchezwa kwa miaka miwili mfululizo iliyopita kutokana na changamoto ya ukata.

“Naenda Kenya lakini nitakuja tena kuangalia Kombe la Kagame ambalo litafanyika hapa Tanzania mwezi ujao. Baada ya hapo nitarudi England kwa ajili ya kuanza programu za maandalizi ya mwanzoni mwa msimu. Napapenda Tanzania hasa Zanzibar kwa sababu kuna utulivu na mambo mengi ya kuvutia,” alisema Wanyama.

Hata hivyo, Wanyama huenda akapata bahati mbaya ya kutoshuhudia mechi baina ya Simba na Yanga ambazo zimepangwa kundi moja la mashindano hayo, baada ya Yanga kutangaza uamuzi wa kujitoa kwa kile wanachodai kubanwa na ratiba za mashindano mengine.

“Ni kweli barua ya sisi kujitoa Kagame Cup imepelekwa TFF na katibu mkuu, ni kweli hatutoshiriki michuano hiyo kwa sababu mbalimbali, kwanza kwa sababu ya kuwa na ukaribu wa mashindano mengi sana”, alinukuliwa Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten akitangaza uamuzi huo wa kujitoa.