Yanga yafanya mazoezi ya kutembea

Muktasari:

Mabingwa hao Tanzania wanahitaji sare au kufungwa bao 1-0 ili kusonga mbele kwa hatua ya makundi

Awassa, Ethiopia. Wachezaji wa Yanga leo asubuhi wamefanya mazoezi ya kutembea umbali mrefu mji Awassa ikiwa ni mbinu ya benchi la ufundi ili kuwawake fiti kabla ya mazoezi ya jioni.

Yanga ipo Ethiopia kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi ya mashindano.

Katika mchezo wa kwanza Yanga ilishinda wa mabao 2-0 dhidi Wolaitta Dicha hivyo mabingwa hao wanahitaji sare yoyote ili kusonga mbele.

Yanga iliwasili Uwanja Ndege wa Bole jijini Addis Ababa baada ya safari ya saa nne ambako ililazimika kupoteza saa tatu uwanjani hapo kukamilisha masuala ya uhamiaji.

Msafara wa Yanga ulikuwa na watu 35, waliotakiwa kuingia ni 21 tu, lakini baada ya majadiliano marefu hatimaye wote walipewa viza ya kuingia nchini humo.

Yanga imesafiri na wachezaji 25 na viongozi watano huku mashabiki na wadau wao wachache watano walitengeneza jumla ya watu 35.

Safari ya basi

Uongozi wa Yanga waliamua kuchukua uamuzi wa kusafiri kwa basi baada ya kuambiwa hakuna ndege katika Jumapili itakayowapeleka jijini Awassa utakapochezwa mchezo huo.

Viongozi hao wakingozwa na mkuu wa msafara wa klabu hiyo Salum Mkemi na Mkuu wa Msafara kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Lameck Nyambaya walilazimika kubadili akili wakishirikiana na Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani aliyetangulia mapema nchini hapa ambaye tayari alishandaa basi la kisasa lililotumika kuipeleka timu hiyo Awassa.

Kikosi hicho licha ya wachezaji kuonyesha kuchoka kilitumia saa tano kusafiri kwa basi  na kufanikiwa kufika Awassa na kuweka kambi katika hoteli moja ya kisasa ya Rori iliyopo hatua 45 kufika uwanja ambao utatumika kuchezewa mechi ya Aprili 18.

Hata hivyo, kitendo cha kusafiri kwa basi Yanga illazimika kuvunja ratiba yao ya awali ya kufanya mazoezi siku ya jana jioni baada ya kufika wakiwa wamechelewa huku pia wachezaji wao wakionekana kuelemewa na uchovu.