Yanga wampa ulaini Maxime

KAGERA Sugar ipo katika hatua za mwishoni kupata msaada kutoka Yanga wa kupewa mshambuliaji, Matheo Athony, anayezitoa klabu udenda klabu kadhaa.

Kocha Mkuu wa Kagera, Mecky Maxime, amesema wamekuwa katika mazungumzo ya muda mrefu na Yanga katika kumpata Matheo na sasa mambo yanaenda vizuri kwao.

“Namjua Matheo, ni mshambuliaji mdogo na mwenye kipaji, sidhani kama Yanga hafai lakini amekuwa akikosa nafasi na nimewaomba wanipe kwa mkopo ili aje huku kuboresha uwezo wake, nashukuru tumekubaliwa,” alisema Maxime.

“Kwa sasa tumeshapewa ruhusa ya kuzungumza kimaslahi na mchezaji mwenyewe, nafikiri akija hapa atapata nafasi nzuri, lakini pia kwa kipaji chake ataweza kuboresha uwezo wake zaidi.”

Mbali ya Kagera Sugar, pia klabu za Lipuli na Njombe Mji nazo zilikuwa zikimwania mshambuliaji huyo ambaye hajafanikiwa kuanza hata katika mchezo mmoja msimu huu.

HALI YA MCHEZO

Maxime anasema kama kuna mzunguko mgumu katika Ligi Kuu Bara basi ni wa pili ambao kila timu huwa na presha ya kutimiza malengo, baadhi zikiwania ubingwa, nyingine nafasi za juu na zile zinazokuwa zinajikwamua na kushuka daraja.

“Ni wakati wa wachezaji kujituma ili kuonyesha uwezo dhidi ya wapinzani, tunahitaji kuwa kwenye nafasi itakayotutengenezea mazingira mazuri,” aliongeza Maxime, nahodha wa zamani wa Stars aliyestaafu kwa heshima.